Search This Blog

Sunday, January 13, 2013

Mbunge, Magufuli wampinga Mwakyembe

MBUNGE wa Ilemela mkoani Mwanza, Highness Kiwia (CHADEMA), ameungana na Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, kupinga agizo la Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe kuhusu kufungwa barabara kuu ya Igombe-Kayenze iendayo katikati ya Jiji la Mwanza.

Akizungumza kwa simu na gazeti hili jana, Kiwia alisema kauli ya Waziri Mwakyembe kutaka barabara hiyo ifungwe ili kupisha upanuzi wa uwanja wa ndege wa jijini hapa, haina tija kwa wananchi kwani hadi sasa hakuna maandalizi yoyote ya upanuzi yanayoendelea.

Alisema kuwa ili barabara hiyo ifungwe, ni lazima serikali ijenge njia nyingine mbadala kwa ajili ya wananchi, na kwamba ni vema wizara hizo mbili za Uchukuzi na Ujenzi zikalipatia ufumbuzi wa haraka sana suala hilo.

Kauli ya Kiwia imekuja siku mbili baada ya Waziri Magufuli aliyefanya ziara ya siku moja jijini hapa, kupinga agizo la Waziri Mwakyembe ambaye hivi karibuni naye alifanya ziara kukagua mradi huo kisha kuagiza barabara hiyo ifungwe mara moja ili kupisha upanuzi huo unaotarajiwa kuchukua muda wa miezi 24.

"Mimi kama mbunge wa Ilemela, naungana na Waziri wa Ujenzi, Dk. Magufuli kupinga agizo la Waziri wa Uchukuzi, Dk. Mwakyembe kuhusu kufungwa kwa barabara ya Igombe-Kayenze ili kupisha upanuzi wa uwanja, lakini pia nashangaa mawaziri hawa wanakuja bila kunishirikisha mbunge wa eneo husika,” alisema.

Alisema anamwomba Waziri Mwakyembe asimuelewe vibaya kwa kuwa hapingi kauli yake kwa nia mbaya, bali anakataa barabara kufungwa bila kujengwa njia mbadala ya kuwawezesha wananchi kupita.

Kiwia pia alieleza kushangazwa na mgongano huo wa wizara mbili kuhusu barabara hiyo, akisema inawezekana serikali imetenga fedha za upanuzi wa uwanja huo kisha kusahau kutenga bajeti ya ujenzi wa barabara mbadala wakati wa upanuzi.

Kuhusu mkandarasi wa Kampuni ya Beijing Construction Engineering Group (BCEG) aliyepewa kazi ya upanuzi wa mradi huo kuchelewa kuanza kazi kwa mujibu wa mkataba, Kiwia aliitaka Bodi ya Makandarasi nchini (TRB) kwa kushirikiana na serikali kumchukulia hatua za kisheria.

Akiwa jijini Mwanza juzi, Waziri Magufuli alisema licha ya serikali kumlipa mkandarasi huyo zaidi ya sh bilioni 8 kwa ajili ya kazi hiyo, lakini hadi sasa maandalizi yake ni asilimia 30 tu

Dk. Slaa afunguka

• Afafanua chimbuko la mkataba kati ya makanisa, serikali

KWA mara ya kwanza, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, ameweka bayana chimbuko la mkataba wa makubaliano kati ya serikali na makanisa, huku akiwasihi Watanzania kujiepusha na malumbano yenye hisia za udini.

Dk. Slaa alitoa tahadhari hiyo jana katika ufafanuzi wake aliouandika kwenye mtandao wa kijamii wa Jamii Forum, kuhusu mkataba huo (Memorandum of Understanding - MOU) kati ya Baraza la Kikristo Tanzania, Baraza la Maaskofu Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alisema kuwa amelazima kutoa ufafanuzi baada ya kuona mkataba huo umewekwa kwenye mtandao wa kijamii, huku watu wengi wakiwa wanauzungumzia kwa kupotosha ukweli wa jambo hilo, na kulihusisha na masuala ya udini.

“Kama mnavyoona, mimi nilikuwa nafahamu historia yote, nafahamu MOU, lakini sikuwa nayo. Mtu huwezi kujua kila kitu, na au kuwa na kila kitu, ‘we need to complement each other’.

“Ninarudia kuwaomba wenzangu, tumetumia muda mrefu sana kujadiliana kwa hisia ya aina mbalimbali. Watanzania hatukuzoea huko nyuma kuulizana dini zetu, wala kabila, wala ukanda. Haya mambo tukiyaendekeza taifa letu litakuwa hatarini,” alisema.

Alisema Watanzania wanapaswa kutambua kuwa, kubomoa ni kazi nyepesi, lakini kujenga tena inachukua muda mrefu, na ni kazi ngumu, na wakati mwingine hata ukifanikiwa huwezi kujenga kama ilivyokuwa.

Akifafanua historia ya jinsi na kwanini MOU hiyo ilizaliwa, Dk. Slaa alisema kuwa huko nyuma serikali ilitaifisha shule nyingi za madhehebu ya dini.

Kwamba utaifishaji huo uliendana pia na ardhi, hasa ikizingatiwa kuwa wakati huo shule zilijengwa kwenye maeneo ya madhehebu ya dini na papo hapo kukiwa na kanisa, nyumba za mapadre na vitu vingine.

Alisema kuwa kwenye miaka ya 1980, madhehebu yakataka warudishiwe ardhi yao, hasa ambayo ina majengo mengine yasiyohusiana na shule hizo.

Dk. Slaa alifafanua kuwa, mchakato wa mjadala ulishika kasi mwaka 1986 Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC), lilipopitisha azimio rasmi na kumtaka Katibu Mkuu, awasiliane na serikali kuanzisha mchakato wa kufanya upembuzi na kutenga ardhi ya shule rasmi, kutoka kwenye ardhi inayotumika kwa huduma nyinginezo za madhehebu ya dini.

“Wakati huo mimi (Dk. Slaa), ndiye nilikuwa Katibu Mkuu wa TEC baada ya kupokea rasmi kazi hiyo Desemba1985. Wakati huo madhehebu yaliishakudai yarudishiwe shule zao kwa kuwa zimegeuka kuwa aibu kwa kukosa ukarabati, na ziko kwenye hali mbaya sana,” alisema.

Aliongeza kuwa serikali ilikuwa imekataa ombi hilo kwa lengo la kuwa, shule hizo zinawahudumia Watanzania wote bila ubaguzi, jambo ambalo ndilo lilikuwa lengo kuu la utaifishaji, na sababu ya utaifishaji ilikuwa bado inaendelelea.

Dk. Slaa aliongeza kuwa, mawasiliano yalipoanza na serikali, wakati huo kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Elimu, serikali iliomba TEC na madhehebu ya dini kwa ujumla, kama yanaweza kusaidia ukarabati wa shule hizo kwa kuwa ziko kwenye hali mbaya na hali ya uchumi wa nchi haikuwa nzuri.

“Wakati mchakato huo kwa upande wa elimu umeanza, kulikuwa pia na mgogoro kati ya serikali na TEC baada ya serikali kuichukua Hospitali ya Bugando kwa utaratibu huo huo wa kuitaifisha,” alibainisha.

Kwamba hospitali hiyo ilikuwa kwenye awamu ya pili ya ujenzi kwa msaada mkubwa wa Shirika la la Maendeleo la Baraza la Maaskofu Katoliki la Ujerumani (Misereor).

Alisema kuwa Katibu Mkuu wa TEC alipowasiliana na wahisani, walikataa katakata kujihusisha tena na ujenzi au ukarabati wa shule au hospitali, vituo vya afya na zahanati, kwa kuhofia kuwa Serikali ya Tanzania imekuwa ikitaifisha huduma hizo bila majadiliano ya aina yoyote.

Wahisani hao walisema hawawezi kuwekeza fedha za walipakodi wao (Ujerumani), lakini walikuwa tayari kuendelea na huduma mbalimbali za kusaidia dawa na elimu kwa shule ambazo bado ziko chini ya madhehebu ya dini kwa kuwa hawawezi kuwaadhibu wananchi na watoto.

Kwa mujibu wa Dk. Slaa, kwa kuwa shughuli zote za Bugando zilikuwa zinaelekea kusimama, na kulikuwa na mgomo kila siku kwa madaktari, manesi na watumishi, serikali ikaomba wajadiliane upya juu ya mambo makubwa mawili.

Mambo hayo ni utoaji huduma katika sekta za huduma za jamii, na kuwa na chombo cha mawasiliano na majadiliano kati ya Ikulu na madhehebu ya dini.

Lakini kwa kuwa madhehebu ni mengi, wakaomba chombo hicho kiundwe na viongozi wakuu wa madhehebu yaliyokuwa yanajulikana kwa mujibu wa sheria.

Hivyo, Waislamu wakawakilishwa na Bakwata, TEC na CCT (kwa madhehebu zaidi ya 60 yaliyoko chini ya Christian Council of Tanzania), na baada ya mashauriano waliunda chombo hicho.

Alifafanua kuwa kutokana na hali mbaya ya shule, serikali iliomba madhehebu ya dini kusaidia ukarabati kwa zile zilizoonekana zitafungwa kutokana na hali mbaya.

“Nasi kwa upande wetu, kwa nia njema ya kuisaidia serikali, lakini pia kuwahudumia Watanzania, tuliwasiliana na wahisani ambao walikazia msimamo wao kuwa hawako tayari kuingia kwenye shughuli za ujenzi wala ukarabati kwa kukosa msimamo wa wazi na wa kisheria wa Serikali ya Tanzania kuhusiana na utaifishaji wa huduma hizo,” alisema.

Katibu huyo aliongeza kuwa, serikali ilipojulishwa ilichukua hatua ya kuanzisha mchakato mzima wa kupata suluhu ya jambo hilo. Ndipo akapewa jukumu hilo, Anne Makinda, wakati huo akiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu.

“Hatimaye, serikali ilikubali kuwa haitataifisha tena na kwa kuthibitisha hivyo, ikawa tayari kuwekeana mkataba na madhehebu ya dini. Ndipo tukaanzisha mchakato wa majadiliano na wahisani, nao katika umoja wao kati ya dhehebu la kikatoliki Ujerumani na Kilutheri pia la Ujerumani, tukaanzisha mchakato wa namna bora ya kutoa huduma za jamii,” alisema.

Hatimaye, makubaliano yalifikiwa na ndipo kikazaliwa chombo kipya, Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii (CSSC), chenye sekretarieti yake, hivyo huduma ya Christian Medical Board ya TEC na CCT, ikavunjwa na kuwekwa chini ya CSSC.

Dk. Slaa aliongeza kuwa, kwa upande wa serikali aliweka saini Edward Lowassa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu wakati huo. Kwamba TEC na CCT nazo zikawekeana na wahisani mikataba yao ya ndani ili kupata misaada ya ujenzi, ukarabati na uendelezaji wa huduma zote za jamii

Wednesday, January 9, 2013

Magufuli amsimamisha kazi mkandarasi Tabora

WAZIRI wa ujenzi, John Magufuli ametangaza kumsimamisha kazi mkandarasi wa kampuni ya Progressive Constructions Ltd - Higleig Joint Venture anayejenga barabara ya Songea – Namtumbo – Kilimansera hadi Matemanga.

Magufuli alifikia uamuzi huo jana wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa miradi minne mikubwa iliyozinduliwa na Rais Jakaya Kikwete ambayo inajengwa kwa kiwango cha lami mkoani Tabora.

Magufuli alisema kuwa Mkandarasi Progrissive ameshindwa kutekeleza kazi kwa mujibu wa mkataba, hivyo amesimamishwa huku vifaa vyake vikizuiliwa.

Aidha Rais Kikwete alizindua ujenzi wa miradi hiyo ikiwa ni pamoja na barabara ya Nzega – Puge – Tabora yenye urefu wa kilometa 114.9 inayounganisha mji wa Nzega na makao makuu ya mkoa huo ambao unaunganisha Tanzania na nchi jirani za Uganda, Rwanda na Burundi Rais Kikwete alisema kuwa Serikali katika mkoa huo inatekeleza jumla ya miradi mikubwa ya barabara minne yenye urefu wa kilometa 293.9 pamoja na mradi wa ujenzi wa daraja la Mbutu.

Naye Mtendaji Mkuu wa Tanroads Injinia Patrick Mfugale, alisema mradi huo unagharimu kiasi cha sh. bilioni 135 na unajengwa na Kampuni za ‘China Communications Construction Company Ltd (CCCC) kwa sehemu ya Nzega-Puge yenye urefu wa km 58.8.

“Huku kampuni ya ‘Sinohydro Corporation Ltd’ inajenga sehemu ya Puge – Tabora yenye urefu wa km 56.10 zote za kutoka nchini China zinazosimamiwa na Kampuni ya ‘SMEC International (PTY) Ltd’ ya Australia,” alisema.

Alisema mradi mwingine uliozinduliwa ni ujenzi wa sehemu ya barabara inayotokea Itigi mkoani Singida kupitia Tabora hadi Urambo ambayo inaenda hadi Kigoma.

“Pia barabara nyingine iliyozinduliwa ni kuanzia Nyahua kupitia Tabora hadi Ndono yenye urefu wa kilometa 127 ambayo inajengwa na makandarasi wawili kwa gharama ya Sh. bilioni 151,” alisema.

Alisema kuwa barabara hizo zitaondoa kilio cha wakazi wa eneo hilo cha kukosa mawasiliano yenye uhakika kwa njia ya barabara za kuwaunganisha na mikoa mingine jirani.

CHADEMA si kuvaa ‘kombati’

NIMEGUSWA sana na mfululizo wa makala za Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Kabwe Zitto, zinazoendelea kutolewa katika gazeti hili.

Katika mfululizo huo, Jumalipili iliyopita aligusia misingi ya chama hicho akisema ‘fuata misingi; Ujenzi wa CHADEMA imara. Humo alijaribu kugusia ni wapi chama hicho kimetoka kiasia hadi kufikia hatua hii ya kuvuma kila kona ya nchi.

Zitto ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Kaskazini, anajaribu kueleza jinsi chama hicho kilipigana na kushiriki chaguzi zote tangu mwaka 1995, lakini kikishirikiana na vyama vingine kwenye nafasi ya urais hadi mwaka 2005 ambapo, Freeman Mbowe, aligombea kiti hicho.

Alisema mazingira hayo ya chama cha tano kwa wingi wa kura katika vyama vyote vya siasa nchini ndiyo mazingira iliyoingia nayo CHADEMA katika uchaguzi wa mwaka 2005.

“Mazingira ya kukatisha tamaa, kwani ujanja mjini haukuwa kwa CHADEMA; bali CUF au TLP na zaidi CCM. Mazingira ya kijana ukisema upo CHADEMA vijana wenzako wanakuangalia jicho la mshangao na hata kuchekwa,” anasema Zitto.

Kwamba hayo ndiyo mazingira ambayo alirithi Freeman Mbowe, kama mwenyekiti wa CHADEMA.

Alianza harakati zake za kuimarisha CHADEMA kwa kukusanya vijana mbalimbali, wanachama na wasio wanachama.

Vijana hao walitoka makundi mbalimbali ya jamii kama wanafunzi wa vyuo vikuu, waandishi wa habari, wanasiasa kutoka vyama vingine na hata vijana wanaharakati katika NGOs na kwingine.

Zitto anasema mwaka 2004 mwezi Machi, Mbowe akachaguliwa kuwa mwenyekiti wa tatu wa CHADEMA, hivyo kuwa na mamlaka zaidi ya kuleta mabadiliko katika chama.

Kwamba wanasiasa wanataaluma wa kila aina nao pia walijiunga na CHADEMA kipindi hicho. “Kuna kipindi tulikuwa tunajiita ‘Real Madrid’ maana tulikusanya ‘mastaa’ wote kutoka vyama vya upinzani.”

Freeman Mbowe aliifanya kazi hii ili kutoa fursa kwa Watanzania wengine kujenga chama imara cha siasa nchini ili si tu kuimarisha demokrasia nchini, bali pia kutoa mbadala kwa chama tawala na hata vyama vingine vya upinzani.

“Utekelezaji wa msingi huu wa chama umelipa. Haikuwa kazi rahisi, bali ni kazi makini yenye ujasiri wa kuepuka kujifanya Mbowe ndiye chama na badala yake kujenga chama taasisi ambapo wanachama wanaweza kusema demokrasia ndiyo CHADEMA.

Kwamba chini ya uongozi wake, Mbowe ameshirikiana na viongozi wenzake kupandisha chama kutoka chama cha tano mwaka 2000 mpaka chama cha pili mwaka 2010.

Zitto ni miongoni mwa vijana na Watanzania waliopata fursa ya kuchangia mabadiliko katika nchi kupitia juhudi hizi za Mbowe, hivyo kuifikisha CHADEMA hapa ilipo leo.

Anasema kuwa chama kilichojaa ufuasi wa watu kitapasuliwa na nyufa za uongo, fitna, chuki, majungu na kujipendekeza. Chama cha misingi ndiyo chama tunachopaswa kujenga na kujivunia nacho.

Ni ujasiri wa kufuata misingi ndiyo unaweza kumfanya kiongozi mwenye timu iliyojaa watu wenye vipawa mbalimbali na uwezo mkubwa wa kuvutia ‘wafuasi’ kama CHADEMA kumudu jahazi na kuliendesha vema.

Nimeanza kwa kumnukuu kaka na rafiki yangu Zitto ili kujenga msingi wa mada yangu leo.

Ninachojaribu kusema ni tofauti ya wanasiasa makini vijana ndani ya chama na wafuasi wanotaka kuonekana ili kukidhi maslahi.

Hoja ya Zitto iko wazi kuwa mafanikio ya kisiasa ni kujitoa kwa kila namna, waweza kudharaurika, kuzushiwa, kutuhumiwa na kutukanwa lakini kama unafanya jambo la msingi kwa manufaa ya wengi, utafanikiwa.

Kwa bahati mbaya, CHADEMA inakoelekea inaanza kuzingirwa na vijana wengi wasio na sifa za misingi alizozieleza ndugu yangu Zitto. Wengi wanaoingia huko wamekata tamaa na mfumo wa utawala wa CCM.

Vijana hawa wa kileo wanaingia CHADEMA kama tumaini, lakini bado wanahitaji kufundwa waijue misingi na maelngo ya chama kuwa si kuvalia ‘kombati’ kutoa matamko kila kukicha na kugombania vyeo na fedha.

Kasoro hii ndiyo imeanza kuwatafuna baadhi ya viongozi wa Baraza la Vijana Taifa la CHADEMA (BAVICHA), hivyo kukubali kutumika kama mawakala wa mafisadi kukihujumu chama chao kwa bei ndogo.

Laiti hawa wangekuwa na misingi anayoileza Zitto wangikuwa nawashinda kwenye mitandao ya kijamii wakijaribu kuandika taarifa za kuwakashifu viongozi wao wakuu kwa kutumia majina ya bandia, badala yake wangekuwa kama Mbunge wa Arusha Mmjini Godbless Lema.

Desemba 30 mwaka jana, niliandika makala yenye nikisema CHADEMA iwafunde BAVICHA mwaka 2013.

Nileleza kuwa mwaka 2012, ulikuwa na hekaheka nyingi kila nyanja lakini nikampongeza Godbless Lema, ambaye kwangu namwona kama mkomavu kisiasa.

Nikasema kuwa laiti CHADEMA ikipata vijana makini 20 kama Lema ikawasambaza mikoani kuwatia wananchi matumaini kuwa ukombozi mpya unawezekana bila kulaghaiwa kwa fedha na kurahisisha kazi ya kueleke Ikulu 2015.

Nilikumbusha jinsi Lema alivyovuliwa ubunge na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha Aprili 5, mwaka huu lakini kwa takribani miezi tisa aliyokaa nje ya Bunge akisubiri uamuzi wa rufaa yake katika Mahakama ya Rufaa Tanzania, alihangaika kukisambaza chama kwa umma.Darasa la Lema limetosha kuwafunda vijana wa CHADEMA kufuata misingi alioieleza Zitto, hivyo kujitathmini na kujipima kama wanaweza kasi ya chama hicho kuwa ni kuwatumikia wananchi bila kutanguliza ubinafsi.

Hizi kasoro tulizozisikia kwa BAVICHA kuwa wanatumiwa na mamluki kukisambaratisha CHADEMA, zinatokana na vijana husika kutokulia kwenye misingi ya uwazi. Hawa wametanguliza ubinafsi na tamaa ya mali na vyeo.

Kumbe iko kila sababu ya Mbowe kuendeleza darasa lake la misingi ya chama ili wafuasi wao wajue kuwa CHADEMA si kuvaa ‘kombati’ na kupayuka kwa kukinzana wenzako.

Anayefanya sarakasi za ajabu kama baadhi ya vijana hao wa BAVICHA waliotimuliwa uanachama, huyo atambue kuwa ndani ya CHADEMA kumbe anakuwa amepotea njia, bora akabaki CCM ili atumike vizuri kuvuruga vuguvugu la mabadiliko.

Wito wangu kwa vijana wapenda mabadiliko walioko ndani ya CHADEMA na vyama vingine, nawasihi watambue kuwa siasa ya leo ni ngumu hasa kwa yule anayeifanya bila kukubali kuwa kibaraka wa watafuta vyeo na madaraka. Tafakari

Tuesday, January 8, 2013

Mtuhumiwa kesi ya Dk. Ulimboka atoa siri nzito

• Azungumza na simu kwa kificho kutoka Gereza la Keko

SIKU moja baada ya Jeshi la Polisi Makao Makuu na Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kutoa kauli tata kuhusu uchunguzi wa tukio la kutekwa, kuteswa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka, mtuhumiwa pekee katika kesi hiyo hadi sasa, raia wa Kenya, Joshua Mulundi, ameibuka na kutoa kauli na siri nzito ya tukio hilo.

Mtuhumiwa huyo ambaye yuko mahabusu, ameliambia gazeti hili kuwa anataka upelelezi wa kesi yake ukamilike haraka ili atendewe haki, lakini kubwa kuliko yote ameitaka serikali imlete Dk. Ulimboka mahakamani ili aweze kumtambua.

Akizungumza kwa kificho kwa njia ya simu kutoka ndani ya Gereza la Keko alikohifadhiwa, raia huyo wa Kenya alisema ameamua kutoa kauli hiyo baada ya kusoma taarifa ya gazeti hili juzi ilikionesha polisi wakirushiana mpira na kutoa kauli zinazopingana kuhusu tukio la Dk. Ulimboka.

Alisema hadi sasa haoni maendeleo ya kesi hiyo kwani kila ikifika mahakamani, upande wa mashitaka hutoa hoja ya kutaka iahirishwe kwa madai kuwa upelelezi haujakamilika.

“Kila ninapoenda mahakamani naiomba mahakama imlete Dk. Ulimboka anitambue, nahoji kwanini upelelezi haujakamilika. Kwa bahati mbaya sana siku hizi kesi hii inapokuja mahakamani, hata vyombo vya habari havijulishwi. Nashukuru Mungu nimepata namba zenu za simu kutoka kwenye gazeti lenu ili nitoe ya moyoni...

“Naomba Dk. Ulimboka aletwe mahakamani ili anitambue, kama atasema mimi ndiye niliyemteka na kumtesa, basi kesi iendelee na sheria ichukue mkondo wake, kama atasema sikuhusika, basi kesi iishe maana sioni sababu ya mimi kuteseka hapa gerezani kwa kusubiri upelelezi ambao haujulikani utaisha mwaka gani,” alisema Mulundi.

Kwa mujibu wa mtuhumiwa huyo, amepata kutoa malalamiko kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angela Kairuki na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), akiiomba serikali imlete mbele yake, Dk. Ulimboka ili amtambue na kuhakikisha upelelezi wa kesi hiyo unafikia tamati.

Mbali ya maombi hayo, mtuhumiwa huyo wa kesi inayovuta hisia za wengi ndani na nje ya nchi, pia alisema aliwaomba viongozi hao wamsaidie kupata dhamana kwani kesi inayomkabili inaruhusu dhamana na hana wakili wa kumtetea.

“Dk. Nchimbi alipokuja hapa gerezani nilimwambia, lakini aliniangalia tu bila kujibu kitu. Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Kairuki nimemwambia, DPP nimemwandikia barua na hata Balozi wa Kenya nchini Tanzania nimemwandikia, hajanijibu wala hakuna msaada ninaopata. Naomba serikali, jamii inisaidie kesi hii imalizeke haraka,” alisema mtuhumiwa huyo.

Hata hivyo mtuhumiwa huyo alitoa siri nzito ya kile alichokieleza kuwa, ukweli kuhusu Dk. Ulimboka, jinsi alivyokamatwa, kuhojiwa na kufikishwa mahakamani katika mazingira aliyodai tatanishi, ambayo gazeti hili kwa sasa haliwezi kuripoti kwani kufanya hivyo ni kuingilia mwenendo wa kesi iliyopo mahakamani.

Wakati Dk. Ulimboka alitekwa Juni 26 mwaka jana na watu wasiojulikana, mtuhumiwa huyo alikamatwa Julai 3 na kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kitusu, Dar es Salaam Julai 13.

Dk. Ulimboka ambaye alikuwa kinara wa mgomo wa madaktari uliotikisa nchini katika nyakati tofauti mwaka jana, alitekwa, kuteswa, kupigwa hadi kung’olewa meno na kucha na kisha kutupwa katika msitu wa Mabwepande, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Baada ya tukio hilo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alitangaza kuunda tume ya wataalam kutoka ndani ya jeshi hilo, iliyoongozwa na ACP Ahmed Msangi.

Hatua hiyo ilikuja baada ya Dk. Ulimboka mwenyewe kuwataja baadhi ya watu aliodai kuwa ndio walihusika kumteka na kumtesa, lakini hadi sasa Mulundi, ndiye mtuhumiwa pekee aliyekamatwa.

Hata hivyo, tume hiyo haijawahi kutoa ripoti yake kama Kova alivyoahidi pamoja na kwamba hata majeruhi mwenyewe, Dk. Ulimboka hajawahi kuhojiwa, huku vigogo wa jeshi hilo wakitupiana mpira kuhusiana na sakata hilo.

Katika hatua ya kushangaza, juzi jeshi hilo kupitia kwa msemaji wake, Advera Senso, limekanusha kuwepo kwa tume hiyo likisema kuwa walioteuliwa ni polisi ambao watafanya kazi za kiuchunguzi kwa taratibu za polisi.

Kauli ya Senso ilipingana na ile ya Kova, ambaye juzi alikiri kuwepo kwa tume hiyo, lakini akasema hawezi kulizungumzia suala hilo kwa vile taarifa zake alishazipeleka kwa wakubwa wake makao makuu baada ya kukamilisha wajibu wake.

“Hili suala lipo mahakamani kwanza, na kuhusu kuhojiwa au kutokuhojiwa kwa Dk. Ulimboka hilo lipo kwa mkubwa wangu, sasa unataka mimi niseme kama amehojiwa au la wakati sijui kinachoendelea huko?” alisema Kova.

Lakini Senso alisema kuwa, hakukuwepo na tume hiyo na kwamba walioteuliwa ni polisi ambao walifanya kazi za kiuchunguzi kwa taratibu za jeshi hilo.

Alisema Jeshi la Polisi lisingeweza kuunda tume katika suala la Dk. Ulimboka kwa kuwa kilichotokea ni uhalifu kama mwingine na litashughulikiwa kwa mujibu wa jeshi hilo.

“Kwanza hilo ni suala la mwaka jana na sisi ripoti za mwaka huo tumeshafunga, labda nianze kufuatilia sasa hivi kujua limefikia wapi,” alisema Senso.

Wakati vigogo hao wakisigana katika kulifafanua sakata hilo, Dk. Ulimboka mara kadhaa amekuwa akieleza kuwa yupo tayari kutoa maelezo yake kama kutakuwa na tume huru ambayo si hiyo iliyoundwa na polisi.

Katika tamko lake mwishoni mwa mwaka jana lililosomwa kwa niaba yake na wakili wa kujitegemea, Nanyoro Kicheere, akimwakilisha mwanasheria wake, Dk. Ulimboka alisema wapo watu ambao hawatapenda kusikia siri iliyojificha katika tukio zima la kutekwa kwake na kwamba hana jinsi zaidi ya kueleza ukweli.

Alisema kuwa tukio la kutekwa kwake, kusukumizwa kwenye gari, kupigwa, kufungwa mikono na miguu, kunyofolewa kucha na kutolewa meno, na hatimaye kutupwa katika msitu wa Mabwepande, lilitokea wakati akiwa kikao na ofisa aliyetambulishwa kwake ni ofisa wa Ikulu, Ramadhani Abeid Ighondu

Lema: Kiti cha Meya Arusha kinanuka damu

UMATI mkubwa wa wakazi wa Jiji la Arusha, jana walijitokeza kwenye Uwanja wa mpira wa Ngarenaro, kuadhimisha kumbukumbu ya miaka miwili ya mauaji ya watu watatu waliouawa na polisi wakati wa maandamano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Maandamano hayo yaliyofanyika Januari 5 mwaka 2011, yakiongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa na wabunge kadhaa wa chama hicho, yalilenga kupinga uvunjwaji wa sheria, kanuni na taratibu zilizotumika kumweka madarakani Meya wa Jiji la Arusha, Gaudence Lyimo.

Wanaodaiwa kuuawa siku hiyo kwa kupigwa risasi na polisi wakiwa kwenye maeneo mbalimbali ya Jiji la Arusha ni Denis Shirima, Omary Ismail na raia wa Kenya, Paul Juguna.

Awali kabla ya mkutano huo wa jana kuanza majira ya saa nne asubuhi, viongozi wa CHADEMA wilaya na mkoa na Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema walitembelea vituo mbalimbali vya yatima na kutoa msaada wa mchele kilo 20 na mafuta ya kula lita tano kwa kila kituo.

Katibu wa CHADEMA wilayani hapa, Martin Sarungi alisema wamepanga kuendelea na kazi hiyo hadi Januari 21 ambapo kwa siku ya jana walifanikiwa kutembelea kituo cha Huruma Group kilichopo Kata ya Ngarenaro kinachohudumia waathirika wa virusi vya ukimwi, kituo cha watoto yatima cha Ansaar Muslim Youth Center kilichopo Kata ya Sombetini kinachohudumia watoto wa kike zaidi ya 30, kituo cha watoto yatima cha Kibowa kilichopo Kata ya Lemara na kile cha Karama kilichopo Kata ya Olorien.

Sarungi alisema kuwa katika kipindi hicho wanatarajia kutembelea jumla ya vituo vya watoto yatima 12, wafungwa na mahabusu kwenye gereza kuu la mkoa la Kisongo na wagonjwa kwenye Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru kwa lengo la kuwasaidia, kuwafariji na kuwatia moyo.

Kwa upande wake diwani wa viti maalum, Viola Likindikikoki (CHADEMA) alisema kuwa yeye na madiwani wenzake wataendelea na msimamo wa kutomtambua meya kwani licha ya kuingia kwenye wadhifa huo kinyume na sheria, pia kiti anachokalia kinanuka damu ya wananchi watatu wa Jiji la Arusha waliouawa bila sababu.

Naye kiongozi wa madiwani wa CHADEMA kwenye Halmashauri ya Jiji la Arusha, Isaya Doita aliwataka wananchi wa jiji hilo kuhakikisha wanashiriki kwenye vikao vya shule wanazosoma watoto wao ili waweze kuzibana bodi za shule na walimu wakuu juu ya michango mbalimbali wanayokusanya, lakini haina tija.

Alisema kuwa walimu wakuu wamejikita kwenye kukusanya michango pekee na kusahau majukumu ya kufundisha jambo linalothibitishwa na matokeo mabaya ya matokeo ya mitihani ya taifa ya darasa la saba na yale ya kidato cha pili ambapo amewataka wazazi kuwa wakali kuhoji fedha wanazochanga zinafanya nini kwani hazisaidii kuboresha taaluma kwenye shule hizo.

Doita ambaye pia ni diwani wa Kata ya Ngarenaro alitaka wananchi wanaofanya biashara chini ya miti wasitozwe ushuru kwani hawapati huduma yoyote kwenye maeneo hayo, hivyo hakuna sababu za msingi za kuwatoza kodi.

“Ebu tumchokoze Mungu kwa kutoa sadaka kwa yatima na wajane ili Mungu aamue kama Gaudensi anatakiwa kuendelea kukaa pale au hastahili, tunafanya jambo hili kwa uoga kwani ni gumu mno mpaka naomba Mungu amrudishie akili aweze kutubu na kugundua aliingia kwa hila ili baraka hizi tunazompa zisigeuke laana kwake,” alisema.

Alisema hata kama leo wakikubaliana na Lyimo kukaa madarakani, haimaanishi kuwa itabadili mfumo wa wananchi wa Arusha kuhudumiwa na serikali yao, bali itaendelea kujenga mfumo mbovu wa kuchakachua haki na sheria nchini kwani ni haki kwa serikali kuhudumia wananchi wake, hivyo haki hiyo wataendelea kuipata wakati wakiendelea kupinga uovu wa uvunjifu wa sheria za nchi bila aibu.

Kwa upande wake Katibu wa CHADEMA mkoani hapa, Amani Golugwa alisema inasikitisha polisi kuua raia wasio na hatia ambao hata hawakuwa kwenye maandamano ya CHADEMA, huku ikiwaacha wengine wakiwa na ulemavu wa kudumu na kutolea mafano wa raia wa Kenya, Njuguna ambaye anadaiwa kuuawa muda mfupi baada ya kushuka kwenye basi.

“Baada ya kumuua, walimchukua wakampeleka kwenye chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya Mount Meru na kumbandika jina Chacha Mwita, lakini mimi na Lema tulipokwenda kuikagua maiti hiyo tulimkuta na kitambulisho kinachoonesha kuwa ni Paul Juguna kutoka Kajiado nchini Kenya,” alisema.

Naye katibu wa CHADEMA wilayani Arusha, Sarungi alisema kuwa wameanza maandalizi ya kupata ushindi kwenye chaguzi mbalimbali zijazo kwa kuanza kuorodhesha majina ya wanachama wake kwenye maeneo ya Jiji la Arusha.

Kwa upande wake, Mbunge Lema amesema kuwa hayuko tayari kuona Meya Lyimo akiongoza kikao wakati kuna watu walikufa, kuna yatima wameachwa, kuna wajane wameachwa kutokana na maandamano ya kumpinga.

“Tukiacha hili lipite wanaweza kufikia hatua ya kunyang’anya wananchi mali zao. Msivunjike moyo katika harakati za kupigania haki kwani hata Nelson Mandela alivumilia kukaa jela, leo tunaona Afrika Kusini iko huru basi na nyie msikate tamaa ili haki iweze kutendeka ndani ya taifa hili,” alisema Lema.

Alisema kuwa kuanzia sasa atahakikisha hakuna kikao cha baraza la madiwani wa jiji kinaitishwa bila wananchi kutangaziwa kama sheria inavyotaka ili waweze kuhudhuria kusikia kile kinachojadiliwa kwa mustakabali wa maendeleo ya jiji la Arusha jambo lililoamsha shangwe kwa wananchi hao

BAVICHA yaanika hujuma za CCM


BAADHI ya vigogo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kushirikiana na viongozi waandamizi wawili wa CHADEMA wamedaiwa kufadhili vijana wa BAVICHA kuhujumu chama hicho.

Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Taifa wa Baraza la Vijana La CHADEMA (BAVICHA), John Heche, wakati akizungumza na waandishi wa habari kueleza sababu za kuwavua uongozi baadhi ya wanachama wao na kusimamishwa wengine kutokana na usaliti.

Heche, hata hivyo, hakuwataja kwa majina viongozi hao wa CHADEMA akisema kuwa wako nje ya mamlaka ya baraza analoliongoza, ingawa vyanzo vyetu vya ndani vilibaini kuwa ushahidi wa moja kwa moja ulimtaja Mbunge wa Maswa Mashariki, John Shibuda.

Kwa upande wa viogogo wa CCM, Heche alimhusisha moja kwa moja Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira, kuwa nyuma ya watu waliokuwa wakikichafua chama.

Alisema mwaka jana Wasira alikuwa akitoa kauli ya mara kwa mara kuwa mwaka 2013 CHADEMA itakufa kwa kuwa alikuwa anajua kuna watu atawatumia ndani ya CHADEMA kwa ajili ya kutaka kujaribu kufanikisha kauli yake hiyo.

“Sisi tulijiuliza huyu anapata wapi ujasiri wa kusema CHADEMA itakufa wakati ndiyo kwanza inazidi kunawiri? Tukajua mwenye uwezo wa kujua hiki chama kitakufa lini ni mwenyezi Mungu.

“Kumbe mwenzetu alikuwa na watu wake ndani ya chama waliomhakikishia kifo hicho, sasa tumewatimua akaanze upya,” alisema.

Heche alifafanua kuwa hivi karibuni kamati ya utendaji ya BAVICHA ikikutana jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kupokea na kujadili taarifa za utendaji kazi na uhai wa baraza nchi nzima kutoka mikoa yote ya kichama.

Aliongeza kuwa miongoni mwa maazimio ya kamati hiyo yalikuwa ni kupokea na kujadili taarifa ya kamati ndogo ya BAVICHA iliyopewa kazi ya kuchunguza tuhuma za baadhi ya viongozi na wanachama wake.

Baada ya kupokea taarifa hiyo walibaini kuwa baadhi ya viongozi na wanachama wana hatia na kuwachukulia hatua zilizostahili kwa mujibu wa katiba ya BAVICHA.

Alimtaja kiongozi aliyevuliwa madaraka na ambaye pia atakuwa amepoteza sifa ya kuwa mwanachama wa CHADEMA kuwa ni aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wao, Juliana Shonza, huku wanachama wa kawaida waliovuliwa uanachama wa BAVICHA wakiwa Habib Mchange na Mtella Mwampamba.

Wanachama waliopewa onyo ni Gwakisa Mwakasando, Joseph Kasambala ambaye ni mwenyekiti wa BAVICHA mkoa wa Mbeya pamoja na Ben Saanane.

Hata hivyo, Wilson Makala wa Babati, hakuwa miongoni mwa wanachama waliosimamishwa kwa muda kama ilivyoripotiwa kimakosa na gazeti hili.

Heche alisema Shonza katika nafasi yake ya Makamu Mwenyekiti, alikuwa akishirikiana na baadhi ya watu kupanga njama na kufanya usaliti dhidi ya BAVICHA, chama na vijana wenzake wapenda mabadiliko.

Alisema katika mikutano hiyo ya siri kwa manufaa ya CCM, Shonza alikuwa akiwakusanya vijana wanafunzi wa vyuo vikuu mbalimbali waliosimamishwa masomo au kufukuzwa vyuoni ambao ni wanachama wa Shirikisho la Wanachadema wa Vyuo Vikuu (CHASO) na kuwarubuni.

“Juliana alifanya kazi yake hiyo kwa ushawishi wa hongo, ili wakubali kuitisha mikutano na waandishi wa habari, watoe matamko machafu dhidi ya CHADEMA na viongozi wake wakuu, akiwamo Dk. Willibrod Slaa na Freeman Mbowe,” alisema.

Alitaja moja ya mikutano hiyo kuwa ni ile iliyofanyika katika Bar ya Highland Makumbusho na kuwaita viongozi wa CHASO na kuwashawishi kuwa watakuwa na maisha mazuri, watarudishwa vyuoni na kutunzwa vizuri hapa mjini kama anavyoishi yeye endapo wangelikubali kufanya kazi hiyo.

Heche aliongeza kuwa Juliana alishiriki kikao kingine kwa ajili ya kuihujumu CHADEMA cha Desemba 6 mwaka jana katika Hoteli ya MIC kuanzia saa 12 jioni akiwa na baadhi ya wasaliti wengine.

Pia alisema Juliana alikaa na kushiriki vikao vya kuanzisha chama kipya kinachoitwa Chaumma, kushiriki katika makundi yaitwayo Masalia na PM7 ambayo yote yalikuwa na lengo la kuvuruga chama na kuwakosanisha wanachama.

“Kama tutashindwa kuwajibishana wenyewe kwa wenyewe katika makosa yenye ushahidi kama huu basi tutakuwa hatuna sababu ya kupewa nchi mwaka 2015 kwa kuwa hawa wasaliti hawawaathiri Wanachadema tu bali kila Mtanzania mpenda mabadiliko,” alisema