Search This Blog

Tuesday, January 8, 2013

Wananchi waua tena polisi Kagera


KWA mara nyingine Jeshi la Polisi mkoni Kagera, limepata pigo kutokana na askari wake wawili kuuawa kikatili na wananchi wilayani Karagwe wakidhani kuwa ni majambazi na kisha gari lao kuteketezwa kwa moto.

Tukio hilo linakuja zikiwa ni wiki chache tangu wananchi wenye hasira kuua askari wengine wawili wilayani Ngara na kuteketeza kituo cha polisi cha Mugoma mnamo Desemba 15, mwaka jana.

Akizungumza na Tanzania Daima, Kamanda wa Polisi Mkoa Kagera, Phillip Kalangi, alisema tukio hilo lilitokea Januari 6, mwaka huu, saa 2:30 usiku katika kijiji cha Kasheshe, kata ya Rugu, upande wa wilaya ya Karagwe wakati walipofika kijijini hapo kumfuatilia mtu mmoja aliyekuwa na meno ya tembo.

Askari waliouawa ni SGT Thomas Migiro mwenye namba E1446 mwenyeji wa mkoani Mara na Koplo Damas Kisheke mwenye namba E 8889 mkazi wa Kamachumu Muleba mkoani hapa wote wakiwa watumishi wa jeshi hilo kituo cha wilayani Ngara.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, askari walikuwa watatu ila mmoja wao, Bryston aliyekuwa na bunduki alikimbia na kuwaacha wenzake wakisulubishwa.

Habari zaidi zinasema kuwa katika tukio hilo gari la askari Damas aina ya IPSUM lilichomwa moto na wananchi hao.

Askari inasemekana walifika wilayani humo na kufanikiwa kumsaka hadi kumkamata mtuhumiwa aliyekuwa na meno ya tembo saba na kuanza kuondoka eneo la tukio.

Hata hivyo, taarifa zilizolifikia gazeti hili kutoka eneo la tukio zinadai kuwa polisi hao walikuwa na biashara yao binafsi na mmoja wa wananchi wa kijijini hapo, ambaye inasemekana kuwa walitaka kumdhulumu.

Chanzo hicho kiliongeza kuwa mwananchi huyo aliwapigia simu baadhi ya wanakijiji kuwa akiwataarifu kuwa amevamiwa na majambazi ambao wanaondoka kuelekea Ngara.

Kwamba wakati askari hao wakiwa safarini kurudi Ngara, walikuta mawe na magogo yakiwa yamepangwa barabarani huku wananchi wakiwataka washuke kutoka kwenye gari, amri ambayo waliikataa na hivyo mmoja wao kufyatua risasi iliyomjeruhi mwananchi mmoja.

Majeruhi alitajwa kuwa ni Jovinary Gabanu (35), aliyepigwa risasi katika sehemu ya kiganja cha mkono ambaye amelazwa katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Nyakahanga.

Hatua hiyo ilizua vurugu na hivyo wananchi kuanza kuwashambulia askari hao hadi kuwaua ingawa muda mfupi baadaye askari wenzao walifika eneo la tukio na kutuliza vurugu.

Baadaye Mkuu wa Wilaya hiyo, Dary Rwegasira, alifika eneo la tukio kuwataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi.

Kamanda Kalangi alisema kuwa askari Bryton aliyekimbia alipatikana usiku huo saa tisa na miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali Nyakahanga ikisubiri utaratibu wa kusafirishwa.

Dk. Slaa: Gesi ni mali ya wananchi

• Adai hawatafuti umaarufu bali wanapinga dhuluma


KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, amesema suala la gesi asili linaleta mvutano kwa sababu ya maslahi ya watu wachache.

Watu wanaoendekeza mgogoro katika sakata hilo ni wale waliofilisika kifikra, hawajui Katiba na hawajui kuwa wananchi ndio walinzi wa kwanza wa rasilimali zao.

Alisema kuwa wanaokuja na hoja ya kusema ni siasa, wanakurupuka kwani wao kama wanasiasa ni lazima kupiga kelele kupinga dhuluma inayotaka kufanywa na serikali dhidi ya wananchi hao.

Akizungumza na Tanzania Daima juzi, Dk. Slaa, alisema Katiba ya nchi pamoja na udhaifu iliyonao, imeainisha vema misingi ya kusimamia rasilimali za taifa kwa usawa bila ubaguzi wala dhuluma.

Alisema kuwa katika suala hilo hawatafuti umaarufu wowote wa kisiasa, na hivyo kuhoji ni nani anaweza kutafuta umaarufu katika shida za watu?

Dk. Slaa aliongeza kuwa Mtwara ni sehemu tu ya Tanzania, hivyo wananchi wa huko na Lindi wana haki ya kunufaika na rasilimali iliyopatikana kwao.

“Serikali inasisitiza kujenga mitambo Kinyerezi kwa kuwa wanataka kuleta gesi hiyo Dar es Salaam ili kunufaika wao kwanza, jambo ambalo ni la kiubaguzi,” alisema.

Kwa mujibu wa katibu huyo, serikali ingekuwa wazi kwa kuwaambia wananchi inalinda Katiba ipi; maana iliyopo inawapa wananchi haki ya kulinda rasilimali zao na kunufaika nazo.

Alifafanua kuwa mkazo unaopaswa kuwepo kwa maendeleo ya taifa, unazungumzia kuondoa maadui watatu yaani ujinga, maradhi na umaskini.

“Wananchi wa Mtwara ni maskini, mkoa wao umetelekezwa muda mrefu, wamekopwa korosho yao, sasa wamepata gesi na wanayo haki ya kudai wanufaike nayo ili nao wapate viwanda, shule na hospitali nzuri,” alisema.

Dk. Slaa alisema mikoa hiyo haijawahi kuwa na hospitali ya rufaa, hivyo wanaionya serikali isiendeshe shughuli za uchumi kwa maslahi ya watu wachache.

Alisisitiza kuwa hakuna sababu za kutokuwekeza mitambo ya gesi Mtwara na Lindi ili isaidie ukuaji wa maeneo hayo kiuchumi na kwamba jambo hilo wala halina siasa.

Alisema ni jukumu la kila mwananchi kulinda utajiri wa taifa lake kwani wao ndio wamiliki, hivyo hawapaswi kutegemea hisani ya serikali na badala yake serikali inapaswa kuwajibuka kwao.

Kauli hiyo ya Dk. Slaa inakuja siku chache baada ya Waziri wa Nishati na Madini kuwabeza wananchi wa Mtwara walioandamana wakiongozana na baadhi ya wanasiasa kupinga usafirishwaji wa gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam.

Desemba 27, wananchi wa Mtwara waliandamana kupinga hatua ya serikali kutaka wasafirishe gesi hadi Dar es Salam na kuwaacha wao wakiwa hawana kitu.

Januari 2, Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo, akizungumza na waandishi wa habari alipinga hatua hiyo ya wananchi na kusema jambo hilo limevamiwa na wanasiasa.

“Hiyo gesi inayowafanya wanasiasa wawashawishi wakazi wa Mtwara kuandamana haiko Mtwara wala Lindi, bali iko katika mipaka ya Tanzania ndani ya kina kirefu cha bahari na kwa hilo kila Mtanzania ana haki ya kutumia,” alisema.

Waziri Muhongo alisema ni jambo la kusikitisha kuona wakazi wa Mtwara wakiandamana kwa ajili ya gesi wakati walipa kodi wa Tanzania hawajaandamana kwa ajili ya rasilimali zinazotoka maeneo mengine kwenda kutumika Mtwara.

Alikwenda mbali na kulaumu kile alichokiita wanasiasa kujiingiza katika sakata hilo na kuwahimiza wananchi waandamane.

Monday, January 7, 2013

  • MFUMO WA UCHAGUZI KATIKA JAMHURI YA MUUNGANO

    Mfumo wa uchaguzi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania utafuata misingi ifuatayo:

    1. Kila raia wa Jamhuri ya Muungano aliyetimiza umri wa miaka kumi na nane atakuwa na haki ya kupiga kura na kugombea nafasi yoyote ya uongozi wa kuchaguliwa katika Jamhuri ya Muungano.
    ...
    2. Haki ya kupiga kura na kugombea kuchaguliwa katika nafasi yoyote ya uongozi haitafungwa na masharti yoyote yanayohusu uanachama wa chama cha siasa au mahali pa kuzaliwa kwa mgombea husika.

    3. Mamlaka husika zitaweka utaratibu wa kisheria wa kuwawezesha watu wenye haki ya kupiga kura lakini wanaishi nje ya Jamhuri ya Muungano au walioko chini ya usimamizi wa vyombo vya kurekebisha tabia za wahalifu kutimiza haki yao ya kupiga kura.

    4. Chaguzi zote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zitafanyika chini ya usimamizi wa Tume huru ya Uchaguzi ya Tanganyika na Tume ya Uchaguzi Zanzibar.

    5. Tume huru ya Uchaguzi ya Tanganyika itakuwa na Wajumbe wafuatao:

    (a) Wajumbe kumi na tano watakaopendekezwa na vyama vya siasa vyenye uwakilishi katika Bunge la Tanganyika kwa kufuata uwiano wa Wabunge katika Bunge;

    (b) Wajumbe watatu watakaopendekezwa na vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu lakini ambavyo havina uwakilishi katika Bunge la Tanganyika;

    (c) Mjumbe mmoja atakayependekezwa na Chama cha Mawakili wa Tanganyika;

    (d) Mjumbe mmoja atakayependekezwa na taasisi zisizokuwa za kiserikali;

    (e) Mjumbe mmoja atakayependekezwa na vyama vya kitaaluma vya taasisi za elimu ya juu zinazotambuliwa na mamlaka ya ithibati ya Tanganyika;

    (f) Wajumbe wawili watakaopendekezwa na taasisi za kidini;

    (g) Wajumbe wawili watakaopendekezwa na Tume huru ya Utumishi wa Mahakama ambao watakuwa majaji wastaafu wa Mahakama ya Rufani ya Tanganyika.

    6. Wajumbe wa Tume huru ya Uchaguzi watachagua Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Tume kutoka miongoni mwao, ili mradi Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti watakuwa ni watu wenye sifa ya kushikilia madaraka ya Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanganyika.

    7. Wajumbe wa Tume huru ya Uchaguzi hawatashikilia madaraka ya Mjumbe wa Tume kabla uteuzi wao haujathibitishwa na Bunge la Tanganyika.

    8. Tume huru ya Uchaguzi itakuwa na mamlaka ya kuteua mtu yeyote mwenye sifa kuna Mkurugenzi wa Uchaguzi na Mtendaji Mkuu wa Tume.

    9. Tume huru ya Uchaguzi itakuwa na mamlaka ya kuteua watendaji wake yenyewe katika ngazi zote kuanzia ngazi ya taifa, Jimbo, Wilaya na katika Majimbo ya uchaguzi. Wasimamizi wa uchaguzi katika ngazi ya majimbo, majimbo ya uchaguzi na wilaya watakuwa ni watumishi wa Tume huru ya Uchaguzi wakati wasimamizi wasaidizi na wasimamizi wa vituo watakuwa watu walioteuliwa na Tume kwa utaratibu wa wazi na kwa vyovyote vile hawatakuwa watu walioko katika Utumishi wa umma;

  • ULINZI WA HAKI ZA BINADAMU KATIKA JAMHURI YA MUUNGANO

    1. Katiba itatambua na kulinda haki na uhuru muhimu wa binadamu zinazotambulika Kama haki za binadamu za kizazi cha kwanza, yaani haki zote zilizoainishwa katika Sehemu ya Tatu ya Sura ya Kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977, na zile zilizoainishwa katika mikataba mbali mbali ya kimataifa ya haki za binadamu.

    2. Katiba itatambua na kulinda haki zote za binadamu zinazotambulika Kama haki za kizazi cha pili za binadamu kama zilivyoainishwa katika ibara ya 11 ya Katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano, na zilizoainishwa katika mikataba mbali mbali ya kimataifa inayohusu haki za kiuchumi, kijamii na kiutamaduni. Haki hizo ni pamoja na:
    ...
    (a) Haki ya Mtu kufanya kazi;

    (b) Haki ya kupata elimu;

    (c) Haki ya kupata msaada kutoka kwa jamii wakati wa uzee, maradhi au hali ya ulemavu na katika hali nyinginezo za mtu kuwa hajiwezi.

    3. Katiba itatambua kwamba Wananchi ndio wamiliki wa rasilimali asilia za maeneo wanakoishi Kama vile ardhi, madini, mafuta, gesi asilia, misitu/wanyama pori na rasilimali uvuvi na kwamba jukumu la Serikali ni kuwezesha Wananchi wa maeneo husika kunufaika na umilikaji huo wa rasilimali asilia.

    4. Wananchi hawatanyang'anywa rasilimali zao asilia na mamlaka za Serikali matumizi na watu au taasisi nyingine ya rasilimali asilia za Wananchi bila kwanza Wananchi watakaoathiriwa na unyang'anyi au matumizi hayo kutoa ridhaa yao baada ya kupatiwa taarifa zote na kamili zinazohusu matumizi yanayotarajiwa ya rasilimali hizo na athari za matumizi hayo kwa mazingira, kiuchumi na kijamii (the right of prior informed consent).

    5. Wananchi, Kama wamiliki wa msingi wa rasilimali asilia, watakuwa na haki ya kulipwa mrahaba kwa ajili ya matumizi ya watu au taasisi nyingine ya rasilimali asilia za Wananchi, wakati mamlaka za Serikali za mitaa, Majimbo na Serikali Kuu zitakuwa na haki ya kutoza kodi mapato yatakayotokana na matumizi ya rasilimali hizo.

    6. Haki za binadamu zilizotambuliwa na Katiba hazitawekewa vizingiti au kuminywa kwa kutumia sheria za kawaida za Bunge au vizingiti vilivyowekwa na Katiba yenyewe (clawback/derogation clauses) ambavyo havilingani na misingi inayokubalika ya kimataifa inayohusu haki za binadamu.


  • "Maliasili ya nchi kama madini, misitu, Mafuta na Gesi Asilia itakuwa milki ya wananchi na serikali itaweka utaratibu wa kuvuna utajiri wa nchi baada ya ridhaa ya wananchi wa eneo husika 'right of prior informed consent'" hili ndio pendekezo la Chadema kwenye Katiba mpya. Huu ndio mwarobaini dhidi ya uporaji wa utajiri wa nchi

Sunday, January 6, 2013

CHADEMA yanasa wasaliti

• Shonza, Mchange, Mwampamba watimuliwa BAVICHA

MBUNGE wa Maswa Magharibi, John Shibuda (CHADEMA), amekalia kuti kavu kutokana na kutajwa kuwa anafadhili baadhi ya viongozi wa Baraza la Vijana Taifa la CHADEMA (BAVICHA) kuleta mgogoro ndani ya chama hicho.

Siri hiyo ilifichuliwa juzi na baadhi ya vijana hao walipokuwa wakijitetea mbele ya kikao cha BAVICHA ili kuthibitisha tuhuma zilizokuwa zikiwakabili za kutumika kuwachafua viongozi wakuu wa CHADEMA.

Taarifa za uhakika kutoka ndani ya kikao hicho zilisema kuwa mmoja wa vijana hao, Fred Hatari, ambaye ni Mwenyekiti wa Shirikisho la Wanachama wa CHADEMA Vyuo Vikuu (Chaso), alitoa ushuhuda mbele ya Kamati Tendaji ya BAVICHA kuwa Shibuda amewahi kumwita mara kadhaa na kumpa fedha ili atoe matamko ya kuchafua viongozi wa chama.

Huku akionesha ujumbe kadhaa wa simu yake ya mkononi (sms) aliyodai kutumiwa na Shibuda, mwenyekiti huyo aliiambia kamati kuwa amekutana zaidi ya mara mbili na mbunge huyo na kupewa fedha ili akatoe matamko sehemu tofauti ya kumpinga Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa, na kusema kuwa ana kadi ya CCM.

“Fred aliamua kusema ukweli mbele ya kamati yetu, akaomba asamehewe kwa maelezo kuwa alifukuzwa Chuo Kikuu kwa kutetea haki, na kwamba alikuwa akiishi kwa kutangatanga, ndiyo maana alikubali kupokea fedha ya Shibuda, lakini alikataa kumkashifu Katibu Mkuu,” kilisema chanzo chetu.

Mwenyekiti wa BAVICHA Taifa, John Heche, alipoulizwa jana kuhusu sakata hili, alikataa kusema chochote kuhusiana na kikao chao, akisisitiza kuwa anapanga mkutano na waandishi wa habari ambao atautumia kuweka wazi ukweli na ushahidi wote alionao.

BAVICHA iliunda kamati ndogo ya kuchunguza mgongano uliokuwepo baina ya viongozi wake na hivyo kumteua Mwenyekiti wa baraza hilo Mkoa wa Singida, Josephat Isango, kuwa mwenyekiti.

Baada ya kamati hiyo kuwasilisha ripoti yake juzi, baraza hilo lilifanya uamuzi mgumu wa kuwafukuza baadhi ya viongozi wake akiwemo Makamu Mwenyekiti wa BAVICHA Taifa, Juliana Shonza na kuwasimamisha baadhi ya wanachama.

Katika kikao hicho ambacho kilijumuisha wenyeviti wa mikoa yote ya kichama nchi nzima, Shonza hakuhudhuria badala yake alituma barua akidai kuwa nje ya Dar es Salaam kwa shughuli za kifamilia.

Makamu mwenyekiti huyo amekuwa akidaiwa kusigana kimaamuzi na viongozi wenzake, na hivyo kutoa matamko ambayo wakati mwingine yalikuwa yakikinzana na msimamo wa chama.

Chanzo chetu kilifafanua kuwa, baada ya ripoti ya kamati ya uchunguzi kusomwa, sekretariati ya BAVICHA ilitoa mapendekezo yake kuunga mkono mapendekezo ya kamati na kisha wakaletwa mashahidi wengine waliokuwa nje ya kikao ili kuthibitisha kama yaliyosemwa ni ya kweli au la.

Katika ushahidi uliotolewa, Shonza alibainika kuwa huwa anatumiwa na Shibuda kutafuta vijana wengine wapokee fedha ili watoe matamko ya kukifedhehesha chama.

Baada ya tuhuma hizo kuthibitishwa na kujadiliwa na wajumbe, kura zote ziliazimia kuwa aondolewe uongozi na kusimamishwa uanachama wa BAVICHA.

Wengine waliotuhumiwa kushirikiana na Shonza ni waliokuwa wagombea ubunge mwaka 2010 katika majimbo ya Kibaha Mjini (Habib Mchange) na Mbozi Mashariki (Mtera Mwampamba) ambao pia wamefukuzwa uanachama wa BAVICHA.

Kikao hicho pia kilichukua uamuzi mgumu wa kuwasimamisha uanachama kwa muda wa mwaka mmoja, Gwakisa Mwakisando (Mbeya), Wilson Makala (Babati) na Joseph Kasambala (Mbeya).

Alipotafutwa na gazeti hili jana jioni kwa simu, Shibuda alikanusha kuhusika na tuhuma hizo akisema kuwa hata kijana huyo (Fred) hamfahamu.

“Hivi wewe nikikwambia Shibuda ni baba yako utakubali? Mnapaswa kujiridhisha na uzushi huo, mimi sijui mambo ya BAVICHA maana si mjumbe huko na sikuwahi kutumia fedha kumchafua Dk. Slaa kwani sina ugomvi naye,” alisema.

Aliongeza kuwa hapendi siasa za udaku na chuki, na akaahidi kulifuatilia suala hilo, huku akidai kuwa kuna watu wanataka kumchafua bila sababu.

Friday, December 14, 2012

Mnyika: Nec ifanyiwe marekebisho kabla ya 2014


















Mbunge wa Jimbo la Ubungo jijini Dar es Salaam kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika

Mbunge wa Jimbo la Ubungo jijini Dar es Salaam kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika, ameitaka Tume ya Mabadiliko ya Katiba kufanyia marekebisho katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kwanza kabla ya kukamilika kwa zoezi la kupatikana kwa katiba mpya.

Mnyika, aliyasema hayo jana jijini hapa katika viwanja vya ofisi ya kata ya Makurumla, wakati akichangia maoni yake mbele ya Tume hiyo.

“Kwa sasa Tume hii ina mapungufu hivyo haitawezekana kupatikana kwa katiba mpya na bora yenye maoni waliyoyatoa wananchi ifikapo mwaka 2014, hivyo tume iandike marekebisho kuhusu tume ya uchaguzi ili iwe na mfumo huru kwa sababu ndiyo inayosimamia kura ya maoni,” alisema Mnyika.

Alifafanua kwa ufupi baadhi ya mapungufu hayo kuwa ni Tume ya uchaguzi kuteuliwa na Rais bila kuwapo kwa mapendekezo kutoka kwa wadau pamoja na kuwatumia watumishi wa Serikali.

Aidha, Mnyika ameitaka katiba mpya isisitize kuwa Bunge ni chombo kikuu na chenye kujisimamia chenyewe katika kupandisha kodi, kutumia fedha pamoja na kupitisha bajeti bila kusimamiwa na Rais.

“Bunge limekuwa kibogoyo ambalo halina meno ikiwa namaanisha halina mamlaka kuhusu bajeti kwani haliwezi kukataa bajeti ya serikali kwa kuhofia kuvunjwa, hivyo Bunge lipewe uhuru kutoa maamuzi yake,” alisema Mnyika.

Aliendelea kwa kusema kuwa wananchi wapewe madaraka ya kumwadhibu diwani au mbunge kwa kumvua uongozi kwa kupiga kura ya maoni ya kutokuwa na imani na kiongozi huyo hata kama muda wa kutoka madarakani haujaisha