Hotuba ya kwanza ya Nyerere
Hotuba ya kwanza ya Mwalimu Julius Nyerere mara tu baada ya kuwa
Waziri Mkuu kufuatia ushindi wa TANU ambao ulikipa ridhaa chama hicho
kuunda Baraza la Kwanza la Mawaziri wa Serikali ya Tanganyika mwaka
1961.
Wazee wangu.
Ndugu zangu.
NADHANI ni wajibu wangu kusema nanyi tena katika jioni hii ya kwanza,
baada ya kushika mzigo wa kuwa Prime Minister (Waziri Mkuu) wenu wa
kwanza.
Labda mtafikiri kuwa kubadili jina tu kutoka Chief Minister na kuitwa
Prime Minister, si jambo la maana sana. Kwa kweli, kubadili jina peke
yake si jambo la maana sana.
Lakini natumaini kuwa wote mnaelewa, maana ya jambo hili. Lilielezwa
vizuri sana wakati wa mkutano wa Machi kwamba kubadili jina huku,
kunafuatana na mabadiliko katika utawala wa nchi yetu, ambayo
Watanganyika wote tunashahili kujivunia.
Mabadiliko haya ya leo, yamekamilisha serikali yetu ya wananchi, Bwana
Gavana, ambaye ametusaidia sana alipokuwa Chairman wa Baraza la
Mawaziri la sasa, kuondoka katika Baraza hilo.
Tangu sasa, mimi nitasimamia Baraza la Mawaziri ambao wote 11,
nimewachagua mimi mwenyewe.
Nawaelezeni jambo hili kwa unyenyekevu mkubwa, kwa sababu mimi na
wenzangu, ni watumishi wenu ninyi mnaonisikiliza. Tunajua kuwa
mnatuamini, nanyi tunawaamini. Na ni ninyi tu mnaotupa nguvu zetu,
tunazozihitaji kwa kazi kubwa iliyo mbele yetu.
Kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, na imani mliyonayo juu yetu, tunapata,
na tutazidi kupata nguvu za kuendesha serikali yenu. Lakini tunawaomba
msisahau, na mara nyingi sana, nimekukumbusheni jambo hili, kwamba
serikali haiwezi kufanya kila kitu.
Utajiri wa Tanganyika, bado uko ardhini. Hatuanzi na akiba kubwa ya
fedha kama Ghana kwa mfano, iliyoanza nayo ilipopata uhuru wake.
Hatuna mkononi fedha walizonazo ndugu zetu wa Nigeria. Kwa kweli,
elimu yetu iko nyuma zaidi kuliko Kenya na Uganda.
Kwa hiyo, tunaanza bila ya kuwa na wananchi wa kutosha, wenye elimu ya
juu, tunayohitaji katika jitihada zetu za kujenga utajiri wa nchi hii.
Lakini matatizo haya, hayanitishi mimi, hayawatishi wenzangu, na wala
hatuombi kwamba yawatisheni ninyi. Tunayaona kwamba ni jaribio tu.
Lakini jaribio hili, na umasikini, si la serikali tu, ni la kila raia
wa Tanganyika.
Mara nyingi sana, nimesema nanyi juu ya umasikini, ujinga namaradhi,
lakini kwa kweli adui yetu mkubwa ni umasikini.
Tukiweza kumshinda adui huyu, tutakuwa tumeweza kupata silaha
itakayotuwezesha kuushinda ujinga na maradhi.
Lakini ni ninyi tu, tunaoweza kupigana vita vya umasikini. Namuomba
kila raia wa Tanganyika, aape kiapo cha kuwa adui wa umasikini.
Amshambulie adui huyo mahali popote atakapoonekana.
Ukiacha pamba yako shambani bila kuichuma, ukiwa na uwezo wa kuongeza
shamba lako kwa eka moja, au nusu eka, au hata robo eka, lakini
ukaacha kwa uvivu tu.
Ukaacha rutuba ya shamba lako ikaharibiwa, ikiwa shamba lako limejaa
magugu na wewe hujishughulishi kuyaondoa, ukiwa unapuuza masharti
unayopewa na wataalamu wa kilimo au hujishughulishi kuongeza elimu
yako ya kilimo, au ukiwa unazurura tu bila kufanya kazi, ikimtegemea
mjomba au shangazi, au Prime Minister wa Tanganyika akufanyie kazi,
basi wewe ndugu yangu, si adui wa umasikini.
Wewe si adui wa ujinga, wewe si adui wa maradhi, wewe kwa kweli ni
rafiki mkuu wa maadui hao. Wewe ni adui wa Watanganyika wote
wanaofanya jitihada yao yote kumshambulia adui huyo.
Ndugu zangu, vita hivi ni vyenu, vita hivi ni vyetu wote na adui yetu
ni huyo niliyemtaja. Basi, tusipoteze wakati wetu tukishambulia maadui
ambao kwa sasa ni marehemu.
Tusidhani hata kidogo kwamba sifa yetu katika Afrika au sifa yetu
katika Dunia nzima, itategemea ukali na ufundi wa matusi tutakayotumia
kutukana ukoloni uliokufa au hata ukoloni mpya utakaojaribu kuanzishwa
kwa ujanja na hila za watu wasiopenda uhuru wetu.
Sifa yetu, itategemea mambo tutakayofanya kuongeza na kudumisha nguvu
zetu ili tuwe na uwezo wa kulinda uhuru wetu wenyewe, na pia
kuwasaidia ndugu zetu wengine kupata uhuru wao na kuulinda pia.
Wala tusipoteze wakati wetu katika kugombania vyeo na fahari ya nafsi.
Kilichotufikisha hapa leo, kwa upesi hivi na kwa amani hivi, ni umoja
wa watu wa Tanganyika. Ninapoulizwa kwa mfano, ni nini mwezi wa Machi
kwa muda wa siku mbili tu, jibu langu ni moja, umoja.
Wenzangu na mimi tulikuwa kitu kimoja. Na tulikuwa kitu kimoja kwa
sababu Tanganyika yenyewe ni kitu kimoja. Na vile vile katika mambo
yetu yote ya maisha ya taifa letu.
Nani asiyejua kwamba msingi wa kufanikiwa kwa TANU, ni umoja wa TANU.
Kadhalika katika vyama vya ushirika au vyama vya wafanyakazi wanachama
wake wanaposhikana bega kwa bega, mambo yao yatawaendea vyema.
Wanachama wake wakigombana na kutengana, mambo yao na mambo ya taifa
zina yatakwenda tenge.
Ndugu zangu, huu si wakati wa kuchezea umoja wetu, tunauhitaji sasa
kama tulivyohitaji zamani kwa ajili ya kuinua hali zetu na ndugu zetu.
Lakini umoja hauhitajiwi na Tanganyika peke yake, Afrika nzima
tunahitaji umoja. Kama mnavyojua, tunahitaji umoja. Kama mnavyojua,
nilikuwa Ghana na Nigeria, huko nilikutana na ndugu zetu na wote
wanatutakia kheri na baraka.
Matembezi hayo, yameikumbusha tena uzito wa mzigo huu tulioanza
kuubeba. Tutawezaje ndugu zangu kuubeba mzigo huu?
Tunaweza kuubeba kwa kuonyesha mfano tu, mfano wa taifa lenye umoja
kamili, lenye nia moja tu, kujenga taifa letu kwa manufaa ya watu wake
wote.
Kusaidia ndugu zetu wa Afrika, popote walipo, kujenga undugu na
mapenzi, baina yetu na binadamu wote. Ikiwa ndugu zetu katika nchi za
jirani wana taabu, na tunajua wanazo taabu nyingi, wajibu wetu ni
kutumia umoja wetu kuwasaidia, na kuwaonyesha kwa mfano, jinsi umoja
unavyoweza kuwasaidia wao pia.
Kila nilikokwenda, nilipokuwa Ghana na Nigeria, nilikumbushwa faida ya
umoja. Ni wajibu wetu kuepukana na vishawishi vyote vya kuuvunja umoja
wetu au kuleta utengano baina yetu na majirani zetu.
Najua kuwa, uhuru huleta kishawishi cha kutengana na marafiki na
majirani ili kuonyesha kwamba tuna nguvu sana, japo tukiwa peke yetu.
Hiki ni kishawishi cha kuepukwa kama ugonjwa, kwa sababu
tusipokiepuka, tunaweza tukawadhuru ndugu zetu, na tukiwadhuru wao,
nasi pia tunajidhuru.
Pana haja gani ndugu zangu, kutumia uhuru wetu kwa kutamba na
kujitutumua mbele ya waafrika wenzetu? Hivyo ndivyo mataifa ya kizungu
yalivyofanya, na kwa upande wake.
Leo, Ulaya haina umoja. Wazungu wanajuta, na wanafanya kila jitihada
kuujenga tena umoja wao. Ni wajibu wetu ndugu zangu kujifunza kwa
makosa yao. Ni wajibu wetu kuchagua yaliyo mazuri, na kuacha yaliyo
mabaya.
Umoja ni jambo zuri, basi na tuudumishe umoja wetu. Lakini, kujitenga
na majirani ni jambo baya, basi na tuliepuke kosa hilo.
Basi ndugu zangu, ndiyo mawazo niliyopata kushirikiana nanyi jioni
hii. Kwanza, kazi. Kwani ni kazi peke yake itakayotuondolea umasikini
wetu. Pili, umoja. Kwani bila umoja, hatuna nguvu ya kuendelea na
jambo lolote.
Tatu, Undugu. Ili uhuru usilete utengano baina yetu na Waafrika
wenzetu au binadamu wenzetu. Katika jitihada ya kutimiza shahada hizo,
mimi pamoja na wenzangu, tutawatumikieni kwa uwezo wetu wote.
Na kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, tutajitahidi kuwatumikieni bila
kujitafutia faida zetu wenyewe au fahari ya cheo.
Ndugu zangu, wazee wangu na akina mama, tupeni msaada wenu. Asanteni
kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment