JOKATE: HUU NI MWANZO TU
BAADA ya kushiriki katika kazi mbalimbali za ujenzi wa taifa, mtangazaji wa kituo cha televisheni cha channel O Jokate Mwegelo ameibuka na kudai kuwa safari yake ndio kwanza inaanza kwani ana mambo mengi ya kulifanyia taifa la Tanzania. Kauli hiyo aliitoa mara baada ya kuzindua brand yake itakayofahamika kwa jina la Kidoti. Brand ambayo ataitumia katika shughuli zake zote za kijamii pamoja na biashara. Miongoni mwa kazi ambazo analenga kufanya ni pamoja na biashara ya nywele ambayo ameizindua wiki hii, biashara ya vipodozi pamoja na ubunifu wa mitindo. Mtangazaji huyo ambaye ameweza kujizolea umaarufu kutokana na kazi za ujasiriamali ambazo amekuwa akishiriki katika maeneo tofauti tofauti, alifunguka na kusema awali alikuwa akiumiza kichwa sana akifikiria jinsi atakavyoweza kulitumia vyema jina lake. “Naweza kusema kwa sasa ndoto yangu imetimia. Kwani baada ya kuwa katika tasnia ya urembo kwa muda mrefu nimekuwa nikitafuta njia itakayo niwezesha kupata pesa kwa ajili ya kunipeleka mbele zaidi” anasema Anasema licha ya kuwa na shahada ya sayansi ya siasa na filosofia aliona njia pekee ya kuweza kutoka kwa urahisi ni kutafuta pesa ili ziweze kumsaidia kutumia taaluma yake hiyo kuisaidia jamii. “ Na kwa mwanzo huu nina uhakika kwa uwezo wa mungu kila ninachopanga kitatimia. Kwani wakati naingia kwenye urembo sikuwahi kuwaza kama ipo siku nitaweza kubuni vazi la hadi ambalo litavaliwa na mwanamuziki mwenye hadi ya juu nchini kama Diamond lakini hili limewezekana”. “Hili pekee limekuwa likinipa faraja ya kufanya kazi kwa bidii nikiamini kuwa siku zote hakuna linaloweza kushindikana chini ya jua” anasisitiza. Jokate ambaye ni mzaliwa wa Songea na pia mshindi wapili wa taji la miss Tanzania 2006 anasema kuwa siku zote amekuwa mstari wa mbele katika kuipa hadhi fani ya urembo. Lengo lake hasa ni kuithibitishia Tanzania kuwa fani ya urembo ikitumika ipasavyo, ina uwezo mkubwa sio tu wa kuboresha maisha ya wahusika bali kuleta maendeleo na kukuza uchumi alisisitiza. Akizungumzia bidhaa zitakazo tengenezwa na chini ya chapa ya Kidoti, Jokate amesema atahakikisha bidhaa zake zote zinakuwa katika ubora unaokubalika sio tu kitaifa bali hata kimataifa. Mrembo huyu wa kitanzania anafuata nyayo za warembo kadhaa duniani ambao wamekuwa wakitumia majina yao yaliyopandishwa chati kupitia fani ya urembo kufanya biashara kitaifa na kimataifa. Miongoni mwa warembo hao ni pamoja na Imman Mohamed Abdulmajid mwanamitindo maarufu mwenye asili ya Somalia amekuwa akifanya vizuri katika kampuni kadhaa zikiwamo za urembo. Warembo wengine wanaofanya vizuri katika biashara ni pamoja na Kim Kardashan na Tyra Banks
No comments:
Post a Comment