Katiba mpya itamke aina ya elimu tunayoitaka
*Kujaza askari wa kulinda mitihani si dawaNINATAMBUA kuwa tuko katika mchakato wa kuandika Katiba mpya. Mpaka ninapoandika makala haya tume ya kukusanya maoni iko kazini ikikusanya maoni ya wananchi wa kada mbalimbali ili kutoa maoni yao juu ya maisha yao na Tanzania waitakayo.
Nikiri mapema kabisa fursa hii ni ya kipekee kwa Watanzania kutoa maoni yetu ili kufanikisha mkataba huu muhimu katika maendeleo ya nchi yetu.
Kwa kuzingatia uzito huu, nami pia napenda kutumia jukwaa hili ili kutoa maoni yangu ikiwa ni mwendelezo wa makundi mbalimbali ya wananchi kutoa maoni yao.
Eneo ambalo ningelipenda katiba ijayo itamke wazi ni namna ya utoaji wa elimu yetu, kwa kuangalia misingi ya falsafa, maadili, makuzi na mahitaji ya jamii yetu kama taifa.
Taifa lolote makini huamua aina ya mfumo wa elimu ambayo itawafaa watu wake ili waweze kujitegemea kifikra na kimtizamo. Kama ambavyo nimekuwa nikieleza katika safu hii, kuwa elimu ndiyo alama na nembo ya utambulisho kwa taifa lolote duniani.
Elimu bora ni fahari kwa taifa na elimu mbovu ni aibu kwa taifa pia. Elimu ni rasilimali muhimu ambayo inahitaji umakini na mipango madhubuti kwani hakuna kazi ngumu kama kuwekeza kwenye bongo za watu. Tukifanya makosa kuwekeza kwenye bongo za watu, ni sawasawa na kuangamiza taifa.
Nchi nyingine suala nyeti kama elimu humilikiwa na dola, kwa maana ya kwamba hakuna mtu yoyote mwenye kuweza kujiamulia namna anavyodhani inafaa kuwa. Sasa kutokana na umuhimu huo, suala la elimu lazima litamkwe kwenye Katiba mpya kwa namna ambavyo haiwezi kuchezewa na kuyumbishwa na mtu yoyote.
Tusiwe na elimu yenye kulenga ufaulu wa mitihani ya mwisho pekee yake, bali tuwe na mifumo linganifu ya kubaini uwezo wa mwanafunzi angali mapema pasipo kutegemea kipimo kimoja tu.
Nionavyo mfumo tulionao kwa sasa umechangia kwa kiasi kikubwa wizi wa mitihani na udanganyifu mbalimbali ambao huripotiwa kila kukicha. Kwa sababu kipimo pekee cha kupima uwezo wa wanafunzi wetu hasa wa elimu ya msingi na sekondari ni mitihani yao ya mwisho.
Hali hii imewafanya wanafunzi kutokuwa na bidii ya kujifunza kwa makini kwa kila mada husika, badala yake, wanajiandaa kutafuta mitihani ya wizi na udanganyifu mwingi unaofanana na huo.
Tumeshudia dhahiri mwanafunzi aliyemaliza darasa la saba hajui kusoma wala kuandika kwa ufasaha, lakini cha kushangaza yuko sekondari. Sasa unajiuliza amefaulu vipi mtihani unaompasa angalau ajue kusoma na kuandika?.
Jibu la swali hili ni rahisi kuwa mfumo tulionao hauna ulinganifu wa kubaini uwezo na maendeleo ya mwanafunzi ambao ndio unapaswa kuwa kigezo cha mwanafunzi kufaulu na wala siyo mtihani wa mwisho pekee yake.
Bila shaka mtakubaliana nami kuwa pindi mitihani inapokaribia wanafunzi wengi huhaha huku na kule wakitafuta mitihani ya kununua. Simu zinatumika kutumiana taarifa za mitihani hewa. Vijana wanachangishana nyingi fedha kwa mategemeo mkubwa ya kutafuta mitihani ya kununua. Na wanafanya hivyo, kwa sababu lengo la elimu ni kufaulu mtihani wa mwisho.
Sasa, hauwezi kukomesha hali hii kwa kujaza askari wengi wa kulinda mitihani isiibiwe bali unaweza kuzuia na kukomesha hali hii kwa kutengeneza mifumo bora na linganifu ambayo itaweza kubaini uwezo wa mwanafunzi tangu awali. Hivyo, kila mtihani wa mada husika utakuwa muhimu zaidi katika kuhitimu elimu yake ya mwisho.
Na hii lazima itamkwe ndani ya katiba yetu mpya na wala isitegemee busara ya mtu kubadilisha na kuchezea mifumo yetu ya elimu kadri awezavyo.
Sambamba na hilo Katiba mpya lazima itamke lugha ya kufundishia ni ipi. Na kama ni Kingereza basi kifundishwe kwa ufasaha na kama ni Kiswahili halikadhalika wanafunzi wafundishwe Kiswahili fasaha. Leo hii tumejenga taifa lililochanganyikiwa, wanafunzi hawajui Kingereza wala Kiswahili vizuri.
Hatuna cha kujivunia tena, wakati umefika wa kuamua jambo moja ama Kiswahili au Kingereza. Kwa mtazamo wangu, ni heri tupende cha kwetu. Tafiti zinaonyesha mtu huelewa na kujifunza vizuri anapotumia lugha anayoijua vyema.
Wanasaikolojia wanasema kuwa mtu hujifunza jambo jipya kwa kulitafakari kupitia lugha anayoielewa vyema na baadaye hufafanua kwa kutumia lugha aliyoulizwa.
Kauli hii ina maana kuwa, mada zote huwasilishwa kwa lugha ya Kingereza, lakini wanafunzi hujadili na kujisomea kwa kutumia Kiswahili. Yaani wanafundishwa kwa lugha nyingine, lakini wanajadili kwa lugha wanayoijua vyema. Sasa hali hii inathibitisha ukweli kuwa mtu huelewa vyema pindi anapotumia lugha yake ya asili.
Katiba mpya haina budi kutamka wazi kuwa lugha ya kufundishia vijana wetu ni ile inayoeleweka kirahisi kwa wanafunzi na walimu wao ili kuepuka kujenga taifa la watu wasiojua vyema kiswahili wala Kingereza.
Jambo lingine muhimu la kuzingatia katika Katiba mpya ni mitaala yetu ya elimu. Kuna aina kuu mbili ya mitaala. Mosi; ni mitaala hodhi (centralized curriculum) ambayo ndiyo inayotumika kwa sasa hapa nchini. Pili; mitaala isiyohodhi(De-centralised curriculum) ambayo hutumika nchi nyingine hususani Amerika ya Kusini.
Mitaala aina hii ya kwanza ni hodhi, kwa maana ya kwamba uamuzi wote hutoka sehemu mmoja ni uamuzi pasipo kuzingatia mahitaji ya jamii nyingine.
Kwa mfano, kijana aliyezaliwa Shinyanga vijijini, akasoma maeneo hayo hayo mpaka darasa la saba, hawezi kuwa na uelewa mzuri au wa kina juu ya mlima Kilimanjaro kama kijana aliyekulia maeneo ya Kilimanjaro tangu utotoni huku akishuhudia mandhari ya mlima huo ikibadilika. Uelewa wa vijana hawa wawili lazima uwe tofauti kabisa kuhusu kitu kilekile.
Katika mfumo hodhi huu wa elimu tulionao, si ajabu mwanafunzi wa kule Mbinga kuonyeshwa picha ya mlima Kilimanjaro iliyochorwa ubaoni, pasipo kujua yeye atadhani ile ni picha ya kofia. Kwa sababu katika maisha yake yote, hajawahi kuona mlima katika mazingira ya tharuji. Hivyo kuifanya milango ya ufahamu wake kuwa mbali kabisa.
Wataalamu wa saikolojia ya elimu wanasema kuwa mtoto hujifunza vyema kwa kuona zaidi na kuiga, sasa ni ukweli kuwa hauwezi kuiga kitu usichokiona na kinyume chake ni sahihi.
Binafsi, ningependa kuona katika Katiba mpya elimu ya msingi itolewe kwa kulingana na mazingira husika na mahitaji ya jamii husika. Kwa mfano, vijana wanaotoka maeneo ya maziwa Nyasa, Victoria, Tanganyika na Rukwa, wafundishwe namna bora ya uvuvi wa kisasa, matumizi sahihi ya rasilimali maji, mbinu sahihi za kulinda mazingira yake na namna ya kukuza uchumi wake kwa kutumia njia bora.
Hii itasaidia sana vijana wetu hasa wasiopata fursa ya kuendelea na masomo ya sekondari kuwa na uelewa wa kutosha kumudu maisha yao na kujiongezea vipato vyao kwa kutumia rasilimali inayowazunguka. Ni imani yangu kuwa kufanya hivyo kutapunguza idadi ya vijana wengi wanaohamia mijini kutafuta riziki.
Tafiti mbalimbali zinaonyesha inakadiriwa ifikapo mwaka 2020 zaidi ya asilimia 70 ya vijana watakuwa wamehamia mijini. Namna pekee ya kutatua kadhia hiyo ni kuifanya mitaala yetu kutoa elimu kutokana na mazingira husika ili kujenga ujuzi na stadi za kazi za kutosha kwa vijana wetu kuyamudu mazingira yao.
Na huu ndiyo msingi madhubuti wa kujenga ujasiriamali ili tuweze kupata, warina asali wazuri, wafugaji bora, wavuvi hodari, wakulima wenye maarifa ya kutosha na wachimbaji madini wadogowadogo wenye maarifa ya kutosha juu ya athari na faida na namna bora ya kujilinda na hatari wakiwa kazini.
Huu ndiyo msingi wa kutengeneza mtaala usiohodhi (De- centralized curriculum) kwa maana ya kwamba elimu itolewe kulingana na mazingira na mahitaji ya jamii husika ili vijana waweze kuyamudu mazingira yao pindi wanapokosa fursa ya kuendelea na masomo ya sekondari. TAFAKARI.
No comments:
Post a Comment