Friday, October 12, 2012

 Mtandao kutokomeza mimba utotoni wazinduliwa

MTANDAO wa kutokomeza ndoa za utotoni Tanzania (TECMN), umezinduliwa jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kupigania haki za wasichana kuolewa kabla ya umri unaokubalika.

Uzinduzi huo ulifanyika jijini Dar es Salaam jana wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike Duniani yaliyoratibiwa na Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF) katika viwanja vya Mwembe Yanga Wilaya ya Temeke.

Mgeni rasmi katika uzinduzi wa mtandao huo unaojumuisha zaidi ya mashirika 20 alikuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Hellen - Kijo Bisimba.

Akizungumza baada ya uzinduzi huo, Mkurugenzi wa CDF ambayo ndiyo imeanzisha mtandao huo, Koshuma Mtengeti, alisema waliamua kuanzisha mtandao huo ili kuunganisha nguvu na wadau wengi baada ya kuona tatizo la ndoa za utotoni limekuwa kubwa.

Alisema tafiti zinaonesha watoto wengi wanaolewa kabla ya umri unaokubalika kutokana na mila na desturi za baadhi ya wazazi ama uroho wa kutaka mahali.

Alisema kuna umuhimu serikali ikabadili sheria ya ndoa ya mwaka 1971 ambayo inaruhusu msichana kuolewa hata kabla hajafikisha miaka 18.

Mratibu wa mtandao huo, Grace Mghamba, alisema lazima ifike wakati sheria ya ndoa ya mwaka 1971 ibadilike na kumpa mtoto wa kike haki yake kusoma na kuolewa kwa wakati mwafaka.

Naye Kijo Bisimba alisema wasichana wamekuwa wakinyimwa fursa mbalimbali kwa kudhani kuwa hawawezi kumudu kama walivyo watoto wa kiume.

Alisema baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwakatisha masomo watoto wa kike kwa kutaka mahari, jambo linalowakosesha haki zao.

No comments:

Post a Comment