Sunday, October 21, 2012

TRA yakanusha malalamiko ya wafanyabiashara Dar

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imekanusha malalamiko ya baadhi ya wafanyabiashara wa jijini la Dar es Salaam kuhusu kupandishiwa kodi kiholela na kukaguliwa bila utaratibu.

Akizungumza na NIPASHE jana, Afisa Msaidizi huduma kwa wateja, Shariff Isihaka, alisema Mamlaka ina utaratibu wa kutoza kodi na kufanya shughuli za ukaguzi kwani wamegawa maeneo husika ili kufanikisha kazi hizo.

Alisema kwa kuzingatia bajeti ya fedha ya mwaka, Mamlaka hutoza kodi kutokana na mabadiliko ya bajeti hiyo alisema kwa mfano, bajeti ya mwaka 2011/2012 wafanyabiashara wenye mauzo yasiyozidi shilingi millioni nne kwa mwaka hawatozwi kodi, wakati mauzo yanayozidi milioni nne na yasiyozidi milioni saba na nusu hutozwa kiasi cha sh. 100,000 ambacho ni kiwango cha chini.

Aidha, alisema wametenga maeneo matatu kama mikoa kwa jiji la Dar es Salaam ambayo ni Ilala, Temeke na Kinondoni ili kurahisisha shughuli zao.

“Tumefungua kituo cha huduma kwa wateja ili kusikiliza maoni, malalamiko na mambo yote yanayohusu kodi kwa ujumla ili kuepusha usumbufu kwa wateja wetu,” alisisitiza Isihaka.

Kwa upande wao wafanyabiashara hao ambao hawakutaka kutajwa kwa majina walitoa malalamiko hayo baada ya NIPASHE kufika maeneo yao ya biashara wameonekana kukosa imani na Mamlaka hiyo hata baada ya kufahamishwa juu ya tamko la Mamlaka.

Hata hivyo, Afisa wa Mamlaka hiyo alitoa wito kwa wateja kuwasiliana na Mamlaka husika ili kutatua matatizo yao kuliko kuendelea kulalamika bila kutoa taarifa hali ambayo haisaidii kutatua matatizo hayo

No comments:

Post a Comment