Wednesday, January 9, 2013

Magufuli amsimamisha kazi mkandarasi Tabora

WAZIRI wa ujenzi, John Magufuli ametangaza kumsimamisha kazi mkandarasi wa kampuni ya Progressive Constructions Ltd - Higleig Joint Venture anayejenga barabara ya Songea – Namtumbo – Kilimansera hadi Matemanga.

Magufuli alifikia uamuzi huo jana wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa miradi minne mikubwa iliyozinduliwa na Rais Jakaya Kikwete ambayo inajengwa kwa kiwango cha lami mkoani Tabora.

Magufuli alisema kuwa Mkandarasi Progrissive ameshindwa kutekeleza kazi kwa mujibu wa mkataba, hivyo amesimamishwa huku vifaa vyake vikizuiliwa.

Aidha Rais Kikwete alizindua ujenzi wa miradi hiyo ikiwa ni pamoja na barabara ya Nzega – Puge – Tabora yenye urefu wa kilometa 114.9 inayounganisha mji wa Nzega na makao makuu ya mkoa huo ambao unaunganisha Tanzania na nchi jirani za Uganda, Rwanda na Burundi Rais Kikwete alisema kuwa Serikali katika mkoa huo inatekeleza jumla ya miradi mikubwa ya barabara minne yenye urefu wa kilometa 293.9 pamoja na mradi wa ujenzi wa daraja la Mbutu.

Naye Mtendaji Mkuu wa Tanroads Injinia Patrick Mfugale, alisema mradi huo unagharimu kiasi cha sh. bilioni 135 na unajengwa na Kampuni za ‘China Communications Construction Company Ltd (CCCC) kwa sehemu ya Nzega-Puge yenye urefu wa km 58.8.

“Huku kampuni ya ‘Sinohydro Corporation Ltd’ inajenga sehemu ya Puge – Tabora yenye urefu wa km 56.10 zote za kutoka nchini China zinazosimamiwa na Kampuni ya ‘SMEC International (PTY) Ltd’ ya Australia,” alisema.

Alisema mradi mwingine uliozinduliwa ni ujenzi wa sehemu ya barabara inayotokea Itigi mkoani Singida kupitia Tabora hadi Urambo ambayo inaenda hadi Kigoma.

“Pia barabara nyingine iliyozinduliwa ni kuanzia Nyahua kupitia Tabora hadi Ndono yenye urefu wa kilometa 127 ambayo inajengwa na makandarasi wawili kwa gharama ya Sh. bilioni 151,” alisema.

Alisema kuwa barabara hizo zitaondoa kilio cha wakazi wa eneo hilo cha kukosa mawasiliano yenye uhakika kwa njia ya barabara za kuwaunganisha na mikoa mingine jirani.

No comments:

Post a Comment