Jaji Warioba awa mbogo
MWENYEKITI wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji mstaafu Joseph Warioba ameshangazwa na kile alichosema kuwa uongo unaoenezwa na Jukwaa la Katiba Tanzania kuhusu mwenendo wa shughuli za tume hiyo.Akizungumzia mwenendo wa kazi ya ukusanyaji wa maoni kwa ajili ya kuandika Katiba mpya jaji Warioba alisema si kweli kwamba tume hiyo inasuasua na kukosa watu kwenye mikutano yao.
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, tume yake imejipanga kuhakikisha hadi Aprili 26, 2012 Tanzania inapata Katiba mpya kama ilivyoagizwa huku akisisitiza kwamba sheria inawaruhusu kuongeza muda iwapo itawalazimu.
“Mtu yeyote mwenye busara kwa mazingira ya nchi atajua kwamba hatuwezi kuwafikia Watanzania wote… mpaka sasa tumepokea maoni ya Watanzania zaidi ya 500,000.
“Tangu awali tulisema suala la muda ni changamoto lakini tunajitahidi kuhakikisha nchi inapata Katiba mpya kwa muda uliopangwa… sioni ugomvi wao uko wapi.
“Wamesema hatutafika na hatujafika magerezani sijui wanapata wapi haya na sielewi nia yao wanaposema uongo, watu wanajitokeza kwa wingi na tunapata ushirikiano kutoka kwa NGO’s nyingine.
“Tumewahoji mahabusu, watumishi wa magereza na wafungwa, wanaposema hatujafika magerezani eti tunahodhi madaraka si kweli,” alisisiza Jaji Warioba aliyepata kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania na kusema mawazo ya viongozi wa Jukwaa la Katiba yanagombana na sheria.
Jaji huyo alisema awamu ya tatu ya ukusanyaji wa maoni imeanza jana kwa wajumbe wake kuzunguka kwenye mikoa saba ya Tanzania Bara na miwili ya Zanzibar na kufanya idadi ya mikoa kuwa tisa awamu hiyo.
Akiwaeleza waandishi wa habari aliokutana nao ofisini kwake Dar es Salaam jana mwenyekiti huyo alieleza namna watu walivyohamasika na kujitokeza kwa wingi kutoa maoni yao kwa kuzungumza na kuandika.
Alisema kwa awamu mbili wamezunguka mikoa 15 ya nchi na kufanya mikutani 842 ambapo jumla ya wananchi 517,427 walihudhuria mikutano hiyo.
Jaji huyo alisema wananchi waliotoa maoni yao kwa maandishi ni 77,402; waliozungumza ni 29,514; waliotuma ujumbe kwa njia ya tovuti ni 3,577; wakiwemo wanaoishi nje ya nchi.
Wengine ni 2,338 waliotuma maoni yao kwenye facebook, wananchi 2,500 waliandika barua na maoni 670 yalipokelewa kupitia magazeti.
Aliitaja mikoa hiyo kuwa ni Mtwara, Kilimanjaro, Iringa, Singida, Njombe, Rukwa, Tabora, Kaskazini Unguja na Kaskazini Pemba.
Wiki iliyopita Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba, alisema ni ndoto kwa Tanzania kupata Katiba mpya ifikapo Aprili 26, 2014 kutokana na kusuasua kwa ukusanyaji wa maoni kunakofanywa na tume ya Jaji Warioba.
Kwa mujibu wa Kibamba tume hiyo inahodhi madaraka na kushindwa kuwafikia wananchi wote huku ikiendelea kuwabagua watu wa makundi maalum wakiwemo wafungwa, mahabusu, watumishi wa magereza na walemavu
No comments:
Post a Comment