Monday, November 5, 2012

Vigogo CHADEMA waswekwa rumande


DIWANI wa kata ya Kirumba, jijini Mwanza, Dan Kahungu (CHADEMA), na katibu wa chama hicho wilaya ya Ilemela, John Anajus, wamewekwa maabusu kwa kosa la kukaidi amri halali ya mahakama, iliyozuia uchaguzi wa meya na naibu wake katika manispaa hiyo.

Mbali na viongozi hao Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, imeagiza kukamatwa na kufikishwa mahakamani Mkurugenzi wa Oganaizesheni wa CHADEMA Taifa, Benson Kigaila, na aliyekuwa Meya wa Jiji la Mwanza, Josephat Manyerere kwa kosa hilohilo.

Amri hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi mkoani Mwanza, Angelo Rumisha, kufuatia kesi namba 69/2012 iliyoko mahakamani hapo dhidi ya watuhumiwa sita kutoka chama hicho, ambapo alisema mara baada ya wote kukamatwa mahakama itatoa hukumu yake kwa pamoja.

Akitoa amri hiyo, Rumisha alisema mahakama haiwezi kutoa adhabu kwa baadhi ya watuhumiwa na kwamba agizo la kutaka wakamatwe Manyerere na wenzake ni kutaka mahakama iheshimiwe, mara inapotoa amri zake halali kwa mujibu wa sheria za nchi.

Kupitia kesi hiyo namba 69/2012, Rumisha aliwataja wengine wanaotakiwa kukamatwa na polisi kisha kufikishwa mahakamani hapo mbali na Kigaila ni Katibu Mwenezi wa chama wilaya ya Ilemela, Kalod Majura.

Awali ilidaiwa mahakamani hapo na wakili wa upande wa mlalamikaji, Salum Magongo, kuwa watuhumiwa wote kwa pamoja walishiriki kikao cha kutangaza uamzi wa kumfukuza udiwani, Henry Matata wa CHADEMA (kata ya Kitangiri), kabla pingamizi lililokuwa limewasilishwa mahakamani na diwani huyo halijatolewa uamzi.

“Mteja wangu Henry Matata aliweka pingamizi mahakamani baada ya kamati ya utendaji ya CHADEMA kutangaza kumvua uanachama kinyume cha taratibu. Lakini watuhumiwa wote wa kesi hii walishiriki kuvunja sheria kwa kumtangaza kumfukuza udiwani,” alidai wakili Magongo.

Wakili huyo aliendelea kudai kuwa kwa kufanya hivyo washtakiwa hao walipuuza amri halali ya mahakama iliyotolewa Septemba 15, mwaka huu, kinyume cha sheria na taratibu.

Hata hivyo, hakimu Rumisha aliamuru diwani Kahungu na Anajus waende mahabusu katika gereza la Butimba, hadi hapo watuhumiwa wengine watakapokamatwa na kuhukumiwa kwa pamoja

No comments:

Post a Comment