Wassira awapiku vigogo
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January MakambaWaziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uratibu na Mahusiano), Stephen Wassira, ameongoza katika kinyang’anyiro cha kuwania ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa nafasi 10 za Bara.
Habari ambazo hazijathibitishwa rasmi, zinasema kuwa Waziri Wassira ameibuka kidedea kwa kupata kura nyingi kuliko wagombea wenzake 34 katika uchaguzi huo uliofanyika juzi jioni.
Habari zilidai kuwa Wassira aliongoza kwa kupata kura 2,135 na kufuatiwa na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, ambaye amepata kura 2,093, akifuatiwa na Mbunge wa Singida Magharibi, Mwigulu Nchemba, aliyetajwa kupata kura 1,967.
Mwingine ni Martin Shigela, Katibu wa UVCCM Taifa, aliyetajwa kupata kura 1,824, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, aliyetajwa kupata kura 1,805 akifuatiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimtaaifa, Bernard Membe aliyetajwa kupata kura 1,455.
Wengine ni Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. David Mathayo David, aliyetajwa kupata kura 1,414, Mkuu wa Wilaya ya Musoka, Jackson Msome kura 1,207, Katibu Mkuu wa CCM anayemaliza muda wake, Wilson Mkama, ametajwa kupata kura 1,174 na Waziri wa Habari, Vijana na Utamaduni, Dk. Fenella Mukangara, aliyetajwa kupata kura 984.
Waliobwagwa katika uchaguzi huo ni Mbunge wa Nkenge, Assumpter Mshama, Mbunge wa Viti Maalum, Kidawa Hamid Saleh, wabunge wa Afrika Mashariki, Shyrose Bhanji na mtoto wa Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, Mwinyi Abdulah na mtoto wa Waziri Mkuu Mstaafu, John Malecela, William Malecela.
Wengine ni Otieno Peter Baraka, Twalhata Kakurwa, Godwin Kunambi, Salehe Mhando, Innocent Nsena, Hiza Tambwe, Anna Magowa, Christopher Mullemwah, Mwanamanga Mwaduga, Ruth Msafiri, Hadija Faraji, Dk Hussain Abdulrehenan Hassan ,Nicholaus Haule, Nussura Nzowa, Dk. Athuman Mtambo, Fadhili Nkurlu, Tumsifu Mwasamale na Rashid Kakozi.
ZANZIBAR
Kwa upande wa viti 10 vya ujumbe wa Nec Tanzania Visiwani, walioshinda ni Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi, Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mnyaa Mbarawa na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Samia Suluhu Hassan.
Wengine ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha; Waziri wa Fedha wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Omar Yussuf Mzee; Bhaguanji Mansuria, Khamis Mbeto Khamis, Abdulhakim Chasama, Mohamed Seif Khatib na Khadija Aboud.
Walioshindwa ni Abdisalami Issa Khatib, Abdalla Ali Hassan, Dk. Abdalla Juma Sadalla, Mohamed Ahmada Salum, Ali Mohamed Ali, Haji Makame Ali, Ibrahim Khamis Fataki, Moza Jaku Hassan, Nassir Ali Juma, Jecha Thabit Kombo, Mohamed Hassan Moyo, Moudlin. Castico, Khalfan Yakoub Shaha na Rose Joel Mihando, Ali Omar Mrisho na Mariam Omar Ali.
Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, alisema matokeo rasmi ya uchaguzi huo yatatangazwa leo baada ya kura za mwenyekiti na makamu mwenyekiti Tanzania Bara na Visiwani.
“Matokeo ya chaguzi zote yatatangwazwa kesho (leo) mara baada ya uchaguzi wote kukamilika ili kama ni kuimba iyena iyena tuimbe sote,” alisema jana Rais Kikwete.
Wagombea katika uchaguzi huo waliopitishwa na Nec iliyokaa mjini hapa Jumamosi iliyopita kwa nafasi ya uenyekiti alikuwa ni Rais Kikwete, umakamu Bara ni aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama hicho, Philip Mangula na Visiwani ni Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein.
Awali uchaguzi huo wa mwenyekiti na makamu wake wawili ulipangwa kufanyika pamoja na ule wa wajumbe wa Nec.
Katika viwanja vya Kizota walionekana baadhi ya wagombea walioibuka videdea wakishangiliwa na kupongezwa na wanachama wenzao.
Miongoni mwa washindi waliuokuwa wakishangiliwa na kupongezwa jana asubuhi ni Shigela na Wassira.
TUHUMA ZA UAMSHO
Wakati huo huo, baadhi ya wapambe na wajumbe wa mkutano huo wamesikika wakimtuhumu mmoja wa vigogo wa CCM Visiwani kuwa ni miongoni mwa wanachama wa Jumuiya ya Uamsho.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti mjini hapa wakati wakifuatilia maelezo ya wagombea wa nafasi za Nec, baadhi ya wapambe kutoka visiwani humo walisikika wakisema mwanachama wa Uamsho hawezi kupewa nafasi.
“Huyu hapati ng’o ujumbe wa Nec, labda wajumbe kutoka Tanzania Bara wanaweza kutuangusha, lakini huyu hawezi kupata ujumbe kwasababu huyu ni Uamsho anafikiri hatumjui, tunamjua,” alisema mmoja wa wanachama wa chama hicho kutoka Visiwani.
NIPASHE pia ilishuhudia kelele kutoka kwa wajumbe wa Visiwani humo juzi wakati mmoja wa kigogo akitambulishwa katika ukumbi wa mkutano huo zikionyesha kuhusika na kikundi hicho cha Uamsho.
“Kwishnei, Kwishnei, Kwishnei,” walisikika wajumbe kutoka Visiwani wakipaza sauti huku wakiwa wamesimama hadi pale mmoja wa wajumbe hao alipowasihi kuacha kupiga kelele hizo.
Jana wakati mkutano mkuu ukiendelea katika moja la banda la mamalishe, walisikika wajumbe kutoka Tanzania Zanzibar wakipaza sauti zao wakisema, “Uamsho kwishnei, Uamsho kwishnei”.
Wajumbe hao walikuwa wakisema hivyo huku wakionyesha vidole kama wanachinja mnyama katika shingo na kuangua vicheko.
SHIBUDA APIGIA DEBE CCM
Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda (Chadema), amerudia kauli yake ya kuwania urais 2015, huku akimtaja Rais Jakaya Kikwete kuwa meneja wake wa kampeni na Philip Mangula kuwa kwenye dawati la kamati ya ufundi wa kampeni.
Alirudia kauli hiyo wakati alipopata nafasi ya kuzungumza katika Mkutano Mkuu wa CCM akiwa kama mjumbe wa Taasisi ya Mpango wa Bara la Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM).
Hii ni mara ya pili wa Shibuda kutangaza nia hiyo hadharani mbele ya mkutano wa CCM. Mara ya kwanza alifanya hivyo Mei 14, mwaka huu mbele ya Nec ya CCM kwenye semina iliyofanyika Dodoma iliyojadili hali ya utawala bora nchini iliyotolewa na APRM ambapo alisisitiza kuwa atagombea kupitia Chadema.
Kabla ya kuanza kutoa hotuba yake, Shibuda alianza kwa kusema; “Ukienda Usukumani kuomba kura, ukawasalimu kwa salamu ya Mwadela, watafurahi sana.
“Ukienda Kilimanjaro kuomba kura ukawasalimu kwa salamu ya Shimboni, watafurahi sana; ukienda Mbeya ukawasalimu wapiga kura kwa salamu ya Ugonile, watafurahi sana; na ninyi mkisikia mnaambiwa CCM hoyee, mtafurahi sana,” alisema na kuwaacha mamia ya wajumbe wakiangua kicheko.
Shibuda alikishauri CCM kufanya mikutano mingi ya hadhara ili kujibu tuhuma mbalimbali zinazotolewa na vyama vya upinzani badala ya kuviacha vyama hivyo vikieneza mambo ambayo yanakuja kuchukuliwa na wananchi kama ni ya kweli.
“Makosa ya CCM ni nyinyi wenyewe, kwa nini hamfanyi mikutano ya hadhara mpaka aje Rais Kikwete au Waziri Mkuu…vyama vya upinzani vinakuwa na mikutano mingi, lakini ninyi hamfanyi na mnawaacha wananchi bila kuwapa majibu sahihi,” alisema.
Alisema CCM ndiyo mbegu inayozalisha tabia ya kuigwa na vyama vingine, lakini akakitaka kiache kuwa chama kinachototoa mbegu za fitna.
Alisema CCM ni chama tabibu nchini wakati vyama vingi ni sawa na maabara kwa kuwa vinashindana maabara kutafuta ugonjwa.
Aliwataka wazee wa chama hicho huku akimtaja Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, kuacha kukaa kimya huku mambo yakiendelea kuharibika ndani ya chama chao wakisubiri kuwa mambo hayo yatapita yenyewe.
Alisema chama kinachofanya vikao ndio chenye uhai na akasikitika kuwepo kwa mdororo kwa vyama vingine na akavitaka viache kutafuta umaarufu kwenye magazeti bali wajenge mtandao.
“CCM mna mtandao mpana sana nchi nzima…hakuna chama cha upinzani chenye mtandao kama wenu kwa vile havina uwezo,” alisema.
Hata hivyo, alikitaka Chama hicho kufanya kazi chenyewe badala ya kutegemea kifanyiwe na vyombo vya dola.
Alimpongeza Rais Kikwete kwa moyo wake wa uvumilivu katika masuala mbalimbali hali ambayo imesaidia sana kuleta utulivu ana amani iliyopo.
Aliwataka viongozi wa vyama vingine kuwa na hotuba zenye dhamira ya kuleta amani nchini badala ya vurugu.
“Nasikitika sana, CCM ni chama tajiri, chama cha kuigwa Afrika katika ukombozi, ni chama chenye falsafa nzuri na ni shamba darasa la kujisahihisha…lakini itakuwa ni aibu wakiacha utajiri huo ukikwapuliwa na mwewe,” alisema.
Alikitaka kitumie utajiri huo kuwajengea vijana elimu ya uraia ili kwa vijana wote wa Bara na Visiwani.
Alisema wapo ambao watashangaa kumwona kwenye mkutano wa CCM na hao ndio watakaomwita kuwa eti ni msaliti lakini akafafanua kwamba upinzani sio ugomvi.
Alisema hao watakaosema hivyo ndio watukutu kwenye vyama vyao kwani hakuna chama cha siasa ambacho mmoja anaweza kukosa watukutu.
Akijibu baadhi ya hoja hizo, Rais Kikwete, alisema Shibuda ni mtani wa CCM, lakini yapo mambo mazuri ambayo ameyazungumza kama ya kuwataka kufanya mikutano ya hadhara kujibu hoja za wapinzani.
“Ni kweli viongozi wa CCM hatufanyi mikutano ya hadhara, tunaogopa nini, ukiangalia idadi ya mikutano inayofanywa na vyama vya upinzani kwa mwaka ni mingi kuliko inayofanywa na CCM…tukiwaachia wapinzani wanaeneza uongo wananchi watakuja kuuona kuwa ni ukweli, CCM jibuni mapigo, msisinzie,” alisema.
VITUKO VYA WAGOMBEA ZANZIBAR
Katika hali iliyochangamsha ukumbi wa Kizota, juzi ni vituko vilivyojitokeza wakati wagombea wakiomba kura. Kwa upande wa Zanzibar kulikuwa na wagombea 26, lakini kati yao wagombea wawili ndio waliowavunja mbavu wajumbe.
Wagombea hao wakijieleza kwa ajili ya kuomba kura ya kuwania nafasi ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec), kupitia nafasi 10 za Zanzibar, walimvunja mbavu Mwenyekiti wa Taifa wa Chama hicho, Rais Jakaya Kikwete, ambaye hakuweza kujizuia kuangua kicheko pamoja na wajumbe.
Mgombea wa kwanza kufanya hivyo alikuwa Dk. Abdulhakim Chasama, ambaye katika kuomba kura aliwasalimia wajumbe kwa sauti kubwa ya Haleluya akiwa anarudia mara kwa mara na kisha akapiga magoti kwa kile alichoeleza kuwa ni huo ni utaratibu wa kabila lake la Wasukuma.
Alifanya hivyo baada ya kutoa salamu za kawaida za Chama hicho na alipoanza kusalimia kwa kutamka Haleluya ndipo umati wa wajumbe katika ukumbi wa Kizota walioangua kicheko. Katika orodha ya wagombea, Chasama alikuwa namba 5.
Mwingine aliyefuata alikuwa mgombea namba 14 Maghwanji Mansuria, ambaye aliwaacha watu hoi pale aliposema katika CCM hakuna ubaguzi na ndiyo maana yeye akiwa Baniani peke yake kutoka Zanzibar amefanikiwa kupata nafasi ya kugombea Nec.
Tamko lake kwamba yeye ni Baniani peke yake liliwafanya wajumbe kuangua kicheko kilichoendelea mara kwa mara huku watu wakisikika kurudia maneno hayo kuwa ‘baniani peke yangu.’
Kama hiyo haikutosha, pamoja na maneno hayo, aliwaamkia wajumbe wote shikamoo licha ya kuwapo wajumbe wengine ambao ni wadogo kwake kiumri.
Wagombea aliyemaliza kujieleza katika orodha ni Yakub Halfan Shaha, ambaye alisema alipatwa na hitilafu kidogo ya kifua chake na hivyo kufanya sauti yake kuwa ya makwaruzo sana na hivyo kutosikika vizuri.
Aliwaomba wapiga kura kumpa kura za ndio ili kifua chake kiweza kupona.
Aidha kinyang’anyiro cha nafasi hizo kiliwahusisha wagombea wa nafasi mbalimbali wakiwemo waliokuwa mawaziri kwa upande wa Serikali ya Muungano na Zanzibar na wale ambao bado ni mawaziri.
VITUKO VYA WAGOMBEA BARA
Miongoni mwa wagombea waliovunja mbavu ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, baada ya kumaliza kuomba kura alichomoa bango lake na kulionyesha kwa wajumbe.
Bango hilo lilikuwa limeandikwa Lukuvi namba 10 akimaanisha kuwa wamchague mgombea namba 10 katika orodha ya wagombea wa nafasi ya 10 za Nec Bara.
Hali hiyo ilimfanya Rais Kikwete kuangua kicheko huku akisema: “Haya Lukuvi nakutakia kila la heri, leo umetoa mpya.”
Mwingine aliyetoa kituko ni mtoto wa mwanasiasa mkongwe, John Samwel Malecela aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, William Malecela, ambaye alisema: “Mtoto wa tinga tinga lazima awe tinga tinga, hawezi kuwa kibajaji.
Mwingine ni January Makamba, ambaye ni Naibu Waziri Mawasialino, Sayansi na Teknolojia, wakati akiomba kura alisema anao uwezo wa kushika nafasi hiyo kwani hata Rais Kikwete kama angepewa nafasi wa kuwa shuhuda angesema hayo.
WASTAAFU WAUNDIWA BARAZA
Katika hatua nyingine, Mkutano Mkuu umebariki marekebisho ya Katiba ya CCM na sasa viongozi wastaafu wa chama hicho wataundiwa Baraza la Ushauri la Taifa la Viongozi Wastaafu.
Hayo yalisemwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana.
Alisema baraza hilo lilipitishwa na wajumbe wote kupitia kura zilizopigwa jana katika mkutano huo uliaonza juzi katika ukumbi wa Kizota.
“Wajumbe walipiga kura za ndio kuruhusu mabadiliko hayo hata pale mwenyekiti alipohoji kama kuna mjumbe anasema hapana wote hapakuwa na mtu aliyejitokeza,” alisema Nape.
Pia alisema mkutano huo pamoja na marekebisho mengine, uliazimia utaratibu wa kuwapata wajumbe wa Nec kupitia wilayani badala ya mikoani.
Kwa mujibu wa chama hicho, wajumbe wa baraza hilo ni Wenyeviti Wastaafu wa CCM Taifa ambao kwa utamaduni wa CCM huwa pia ndio Marais wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wengine ni makamu wenyeviti wastaafu bara na visiwani, ambao kwa Zanzibar kwa mujibu wa utamaduni wa CCM ndio huwa pia marais wastaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mwenyekiti wa baraza hilo atakuwa ni Mwenyekiti yule aliyewatangulia wenzake kustaafu. Na watakutana pale tu wanapoona ipo haja ya kukutana.
Aprili mwaka jana, Halmashauri Kuu ya chama hicho, ilipitisha uamuzi huo wa kuunda Baraza la Wazee wa chama hicho na hivyo kuifanya mabadiliko ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la 2010 ili kuruhusu kuundwa kwa baraza hilo.
Nape alisema uundwaji wa baraza hilo ni ushauri wa wastaafu wenyewe.
“Wazo la kuundwa kwa baraza hili lilitokana na ushauri wa baadhi ya wazee wenyewe wastaafu wakizingatia wingi na urefu wa vikao husika na si mpango au mkakati wa kuwaengua makusudi wastaafu hao kama inavyodaiwa na baadhi ya wapotoshaji,” alisema.
Alisema kwa kuwaundia baraza la ushauri ni namna nzuri ya kuendelea kutumia busara zao kwa kutumia chombo kinachotambulika kikatiba.
Aidha, wanaweza kuombwa kuhudhuria vikao vya Kitaifa au wao kuomba kuhudhuria kulingana na mazingira na mahitaji ya wakati husika.
Kazi kubwa ya baraza hili ni kushauri chama na serikali zake zinazotokana na CCM na si kudhibiti chama, serikali na viongozi