Search This Blog

Monday, November 12, 2012

Polisi K’ndoni yadaiwa kumlinda Mzungu




SOPHIA Ngonyani, mama mzazi wa mtoto, Paul Moses (5), anayedaiwa kufa katika bwawa la kuogelea nyumbani kwa raia wa Czech, Peter Silarszky, amelalamikia kituo cha polisi Kinondoni kuchelewesha uchunguzi wa kifo cha mtoto wake alichodai kina shaka ndani yake.

Akizungumza na Tanzania Daima mwishoni mwa wiki, mama huyo alisema mtoto wake alikutwa na mauti Aprili, mwaka huu, na kufungua kesi yenye RB no. 6667/12 ambayo jalada alikabidhiwa mpelelezi aliyemtaja kwa jina la Nehemia Kaay.

Alisema tangu kufunguliwa kwa jalada la kesi hiyo hakuna hatua zozote zilizochukuliwa huku mpelelezi huyo akidaiwa kumlinda Mzungu huyo.

“Mlinzi wa getini katika nyumba hiyo aliniambia wakati wote mtoto wangu alikuwa akicheza na familia hiyo ambayo ina watoto wa umri wa miaka 15, 9, 5, lakini baba wa watoto hao anawakataza kuhojiwa,” alilalamika.

Akielezea kifo cha mtoto huyo, alisema majira ya saa mbili usiku, alipata taarifa za ajali hiyo ya maji ya mwanae, ambapo alipofika nyumbani kwa Mzungu huyo alikuta ameshaopolewa ndani ya maji akiwa amekufa.

Alidai alipohoji sababu za kifo cha mwanae aliambiwa alikutwa amezama ndani ya bwawa hilo, ambapo pia katika tukio hilo alikuta askari wa Kinondoni.

Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyella, kuzungumzia suala hilo, alitaka atafutwe Ofisa Upelelezi Mkoa (RCO) ili kueleza upelelezi wa jalada hilo umefikia wapi.

Alipofuatwa RCO, Salum Ndalawa, aliwaita wapelelezi wawili ambapo mmojawao alidai kuwa ndiye aliyemuopoa mtoto huyo kwenye bwawa, lakini pia alionekana kutokubaliana na mzazi wa mtoto huyo ambaye alipinga kitendo cha mama mfiwa kutaka watoto wa raia wa kigeni kuhojiwa.

Hata hivyo, RCO alieleza kuwa jalada hilo wangelifanyia kazi ikiwa ni pamoja na watoto wa raia huyo kuhojiwa, ili kubaina chanzo cha kifo hicho

No comments:

Post a Comment