Search This Blog

Monday, November 12, 2012

Familia ya Kikwete yamwokoa Membe

• Mawaziri sita wapeta, Mukama aponea tundu la sindano



LICHA ya Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, kuwaeleza wajumbe wa Mkutano Mkuu kuwa haungi mkono kundi lolote ndani ya chama katika mbio za urais 2015, mkewe Salma na mwanaye Ridhiwan, wametajwa kuongoza kampeni za kumnusuru Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe.

Wakati matokeo rasmi ya uchaguzi wa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (NEC), kupitia kapu maalum yakitarajiwa kutangazwa leo, matokeo ya awali yanaonyesha kuwa mawaziri sita wameibuka washindi, huku Katibu Mkuu wa chama hicho, Wilson Mukama, akiponea tundu la sindano.

Hata hivyo, juhudi za kada maarufu na Mjumbe wa Baraza Kuu (UVCCM), Hussein Bashe, kupiga kampeni za kumwangusha Membe, zimeshindwa kufua dafu baada ya Salma na Ridhiwan Kikwete kuingilia kati dakika za majeruhi na kuokoa jahazi lisizame.

Bashe ambaye anatajwa kuwa mfuasi wa kundi la Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, juzi aliibua madai mazito dhidi ya Membe akimtuhumu kwa unafiki, hivyo kuwataka wajumbe wa mkutano mkuu unaoendelea mjini hapa, wasimchague kwa madai kuwa hafai kuwa kiongozi.

Baadhi ya vigogo wa CCM ambao pia ni wajumbe wa mkutano mkuu, walisema kuwa ushindi wa Membe umechangiwa sana na juhudi za mke wa Rais, Mama Salma na Ridhiwan Kikwete na hatimaye kada huyo anayedaiwa kuutaka urais 2015, kushika nafasi ya sita ikipata kura 1,455.

“Bila Mama Salma na Ridhiwan, Membe angeanguka vibaya maana walihaha sana kumwombea kura kwa wajumbe,” alisema moja wa wajumbe wa NEC.

Hata hivyo ushindi wa Waziri Membe umewagawa wajumbe wengi, huku mahasimu wake kisiasa wakimbeza kwamba amezidiwa na vijana wadogo.

Akizungumza na gazeti hili jana mjini hapa, Bashe ambaye alipiga kampeni kwa nguvu kumwangusha Membe, alisema hakufurahishwa na ushindi wa Membe kwani hakutaka awemo kwenye orodha ya washindi kumi bara.

“Lakini nimefurahi kwa sababu kazidiwa kwa kura hata na watoto wadogo. Shigela, Januari, Mwigulu, wote wamemzidi kwa kura, ila ana bahati ya kuwemo,” alisema Bashe.

Habari kutoka ndani ya chumba cha kuhesabia kura, zilidokeza kuwa mbali ya Membe, mawaziri wengine walioibuka kidedea ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira, aliyepata kura 2,135 na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, ameshika nafasi ya pili kwa kura 2,093.

Katibu wa Uchumi na Fedha, Mwigulu Nchemba, ameshika nafasi ya tatu kwa kunyakuwa kura 1,967 wakati Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana (UVCCM), Martin Shigela, ameibuka na nafasi ya nne kwa kura 1,824.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, amekuwa wa tano akiwa na kura 1,805 huku Waziri wa Maendeleo ya Mifugo, Mathayo David, akikamata nafasi ya saba kwa kura 1,414.

Matokeo hayo yasiyo rasmi, yanaonyesha pia Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Msome Jackson, ameshika nafasi ya nane kwa kura 1,207 wakati Katibu Mkuu wa CCM, Mukama, akishika nafasi ya pili kutoka chini kwa kura 1,174 na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara akiambulia nafasi ya kumi akiwa na kura 984.

Walioangukia pua katika uchaguzi huo ni mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Shy-Rose Bhanji, mbunge wa Nkenge, Assumpter Mshama, Otieno Peter Baraka, Twalhata Ally Kakurwa, Godwin Kunambi, Innocent Nsena na Richard Tambwe.

Wamo pia Anna Magowa, Christopher Mullemwah, Salehe Mhando, Fadhili Nkurlu, Tumsifu Mwasamale, William Malecela, Rashid Kakozi, Luteni Kanali, Dk. Kesi Mtambo, Nicholaus Haule na Nussura Nzowa.

Wengine walioambulia patupu ni Hadija Faraji, Dk. Hussein Hassan, Mwanamanga Mwaduga na mbunge wa zamani wa Muleba Kaskazini, Ruth Msafiri.

Kwa upande wa Zanzibar, hadi jana kamati inayosimamia uchaguzi huo ilikuwa ikiendelea kukamilisha kazi ya kuhesabu kura.

Hata hivyo waliojitosa kuwania nafasi kumi za NEC kutoka Tanzania Bara ni Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, mbunge wa Uzini, Mohamed Seif Khatib, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi, Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dk. Abdallah Juma Sadallah na Waziri wa Fedha, Omar Yussuf Mzee.

Wengine ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.

Wapo pia Kidawa Hamid Saleh, Abdisalaam Issa Khatib, Khadija Hassan Aboud, Abdalla Ali Hassan, Mohamed Ahmada Salum, Abdulhakim Chasama, Ali Mohamed Ali, Haji Makame Ali, Ibrahim Khamis Fataki na Moza Jaku Hassan.

Wengine ni Nassir Ali Juma, Jecha Thabit Kombo, Khamis Mbeto Khamis, Mohamed Hassan Moyo, Bhaguanji Mansuria, Moudline Castico, Yakoub Khalfan Shaha, Rose Mihambo, Ali Omar Mrisho na Mariam Omar Ali.

No comments:

Post a Comment