Ewura yazibwaga kampuni za mafuta
|
KESI iliyofunguliwa na kampuni 13 zinazouza mafuta ikiwamo BP
Tanzania Limited dhidi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na
Maji (Ewura), imetupiliwa mbali baada ya kushindwa kuthibitisha hasara
waliyopata kwa bei za mafuta kushuka.
Baraza la Rufaa la Ushindani mbele ya jopo linaloongozwa na Mwenyekiti, Jaji Razia Sheikh na wajumbe wake Dk. M. Bundara na Ali Juma liliitupilia mbali kesi hiyo mwishoni mwa wiki. “Kutokana na mazingira yaliyokuwapo, mdaiwa (Ewura), alifuata sheria katika kutangaza bei mpya ya mafuta, lakini walalamikaji walikaidi kukubaliana na uamuzi huo. “Kwa hiyo, malalamiko yao hayana msingi na jopo linayatupilia mbali na walalamikaji wanatakiwa kuilipa Ewura gharama za kesi,” alisema Jaji Sheikh. Jaji Sheikh akisoma uamuzi huo, alisema Ewura kwa mamlaka waliyonayo walitangaza bei mpya ya mafuta ambayo ilitakiwa kuanza kutumika Agosti 3, 2011 na ilizitaka kampuni za mafuta kuuza mafuta kwa gharama yoyote, lakini isizidi kiasi walichotangaza. Alisema Ewura wakati ikishusha gharama za mafuta ilizingatia vigezo vyote kisheria na maslahi ya wanunuzi, wawekezaji wa mafuta pamoja na serikali. “Hakuna ushahidi wa kuonyesha kwamba Ewura wakati wanapunguza bei ya mafuta hawakuzingatia maslahi ya wawekezaji, wanunuzi na uchumi wa nchi kwa ujumla. “Wakata rufaa wameshindwa kuleta ushahidi wa kuonyesha athari walizopata kutokana na bei mpya, upo ushahidi miongoni mwao waliendelea kufanya biashara na kusambaza mafuta,” alisema. Kampuni zilizofungua kesi dhidi ya Ewura ni BP Tanzania Limited, Engen Petroleum Tanzania Limited, Camel Oil, Oilcom, Total, Gapco, Hass Petroleum, Oryx, MGS, Lake Oil, Moil na Acer Petroleum Tanzania Limited. Ziliwasilisha madai 10 zikidai kwamba wakati wanashusha bei ya mafuta, Ewura walishindwa kuzingatia gharama za kusambaza mafuta nchini, haikujali maslahi yao, ilishindwa kutoa uwiano kati ya wanunuzi, wasambazaji na iliwataka kuuza mafuta kwa hasara. Sheikh alisema Ewura hawakulazimisha wasambazaji mafuta kuuza kwa bei moja, waliwaruhusu kuuza kwa gharama yoyote ya chini kwa ajili ya ushindani wa kiabiashara, lakini wasizidi bei halisi iliyotangazwa ambapo faida ilizingatiwa. Walalamikaji waliwakilishwa na Wakili Fatuma Karume akisaidiana na Madina Chenge wakati Ewura iliwakilishwa na Galeba pamoja na Kabakama. |
No comments:
Post a Comment