Search This Blog

Tuesday, October 16, 2012




TFF wamenipa gari bovu -Kocha Stars





Kim Poulsen


KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars Kim Poulsen amesema hana usafiri wa kumuwezesha kwenda mikoani kuangalia mechi za Ligi Kuu ya Soka ya Tanzania Bara.

Kim aliiambia HabariLeo jana kuwa gari alilopewa na Shirikisho la Soka nchini (TFF) ni la zamani na hivyo haliwezi kumudu safari za nje ya Dar es Salaam.

“TFF wanajua kuwa natakiwa kwenda mikoani kuangalia ligi, lakini usafiri wangu hauniwezeshi kufika huko, hata hivyo kila nikiongea nao wanasema kuwa wanalishughulikia,” alisema Kim.

Kim alisema kuwa hata hivyo ameona mechi nyingi za Ligi Kuu zinazochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam na kuongeza kuwa kuna umuhimu wa yeye kuanza kutoka nje ya Dar es Salaam kufuatilia ligi na kubaini nyota wa timu ya Taifa.

“Gari nililonalo ni bovu haliniwezeshi hata kufika Tanga, lakini kuna umuhimu wa kwenda mikoani kufuatilia ligi,”alisema Kim.

Alipoulizwa kuhusu soka la Zanzibar, Kim alisema tayari ameandika mapendekezo ya kwenda huko na kwamba tayari TFF imepitisha mapendekezo yake ambapo atapata fursa ya kuona mechi mbili Unguja na mechi moja Pemba.

Kim alisifu kikosi cha sasa cha Taifa Stars kuwa ni bora kwa sababu kinaundwa na zaidi ya wachezaji watano waliotokana na mfumo wa soka la vijana.

Alijigamba kuvuka rekodi ya kuiwezesha timu Taifa Stars kucheza kwa mara ya pili fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 2015 kutokana na ubora wa kikosi chake cha sasa ambacho anaendelea kukijenga.

“Naamini kuwa timu yangu ya sasa nitaweka rekodi ya kuiwezesha Taifa Stars kucheza fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 2015 kutokana na ubora wa timu yangu,”alisema Kim.

Kim alisema walikaribia kufuzu kwa fainali za mwaka huu lakini bahati haikuwa yao kwani walitolewa kwenye mikwaju ya penalti na timu ya Taifa ya Msumbiji baada ya kutoka sare ya bao 1-1 kwenye dakika 90 za mchezo huo

No comments:

Post a Comment