
BAADA ya kusambaa kwa picha zao za nusu uchi katika mitandao mbalimbali ya kijamii na kwenye vyombo vya habari, wasanii wa filamu nchini Wema Sepetu na Aunt Ezekiel wamejitokeza kuomba radhi kwa wananchi juu ya picha hizo.
Wakizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Idara ya Habari (Maelezo) Dar es Salaam jana, wasanii hao nyota walisema wanaomba radhi kwa Wizara ya Habari Vijana, Utamaduni na Michezo na Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) pamoja na wadau wote wa tasnia hiyo, waelewe kuwa hata wao wameumizwa na picha hizo kwani hawakukusudia kupigwa picha hizo wakiwa hivyo.
Wasanii hao walipigwa picha hizo wakiwa kwenye tamasha la Fiesta Morogoro na Dodoma mapema mwezi uliopita.
Kwa upande wake Aunt alisema ameona ni muhimu kuomba radhi kwa Watanzania kwa kuwa ni kitendo cha aibu na hasa kwa kuzingatia yeye ni kioo cha jamii hivyo kuna baadhi ya mashabiki wake wanafuata vitu anavyovifanya.
“Hiki kitu kimeniumiza sana na ndio maana leo hii tuko mbele yenu kuomba radhi kwa watu wote, kwa kuwa sisi ni kioo cha jamii na inatutegemea tuweze kuielimisha lakini hatukupiga zile picha kwa kusudi,” alisema Aunt.
Licha ya picha hizo kuwa ni matokeo ya uvaaji wa nguo fupi, Aunt alisema ataendelea kuvaa nguo hizo ikiwa kazi yake itamtaka kufanya hivyo, kwa kuwa kazi yake inamfanya abadilike kila mara.
Kwa upande wa Wema ambaye amewahi kuwa Miss Tanzania mwaka 2006, amewaomba radhi Watanzania hasa wanawake wenzao kuwasamehe kwa kitendo hicho na kuahidi kuwa jambo hilo halitajirudia tena na kuwaomba waliosambaza picha hizo kwemye mitandao waziondoe kwani zinazidi kupotosha jamii.
Hata hivyo hiyo si mara ya kwanza kwa Wema kupigwa picha akiwa amevaa nusu uchi, katika tamasha la Fiesta Morogoro mwaka jana alifanya tukio kama hilo.
“Baada ya kuomba radhi tunaomba vyombo vya habari visitumie tena hizo picha na kuziondoa katika mitandao yao kwa sababu tunaamini hazileti mafunzo yoyote katika jamii zaidi ya kupotosha,” alisema Wema
No comments:
Post a Comment