Search This Blog

Thursday, December 13, 2012

Lowassa: Iundwe Tume ya Elimu.

WAZIRI Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, amependekeza iundwe Tume ya Elimu itakayokuwa na wataalamu ili kuchunguza na kutathmini, iwapo mfumo wa elimu nchini unaendana na hali ya sasa.

Akizungumza katika mahojaino na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana, Lowassa alisema kuwa ni kosa kusema kuwa mitaala ya elimu nchini haifai, na kuongeza kuwa la msingi ni kuundwa kwa tume hiyo.

“Mimi nasema kuwa, sasa wakati umefika kama taifa kuunda Tume ya Elimu ili kuangalia na kupitia mfumo wote wa elimu, kuangalia mitaala yetu kuanzia elimu ya awali mpaka vyuo vikuu, kuangalia ubora wa elimu hiyo, vitabu gani vitumike, hali ya maisha ya walimu, yaani kwa ujumla tuangalie upya kuhusu mfumo wa elimu yetu,” alisisitiza.

Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli, aliongeza kuwa nchi zote zilizoendelea duniani, zimekuwa zikifanya hivyo, akitolea mfano Marekani, ambako hivi sasa kuna mchakato wa kuangalia elimu inayotolewa kama inaendana na changamoto za karne ya 21.

Alisema kumekuwa na malalamiko mengi miongoni mwa wadau wa sekta ya elimu ya kwamba, mitaala ya elimu nchini haimwandai mwanafunzi kuweza kukabiliana na changamoto za maisha ya karne hii, ikiwa ni pamoja na kuweza kujiajiri.

Alifafanua kuwa, Serikali ya CCM imefanya makubwa sana katika sekta ya elimu, hususan awamu hii ya nne, ambapo kwa mafanikio makubwa imeweza kujenga shule za sekondari katika kata zote nchini.

Katika mkutano wake mkuu wa nane hivi karibuni mjini Dodoma, CCM ilitoa mapendekezo kadhaa miongoni mwao likiwa la kuboresha elimu nchini.

“Mimi nilipata bahati ya kuongoza juhudi hizo za serikali kwa mafanikio makubwa kujenga shule hizo, lakini mafanikio hayo yamekuja na changamoto zake,” alisema.

Lowassa aliongeza kuwa, tume hiyo ikiundwa itaangalia changamoto hizo zote na kutoa mapendekezo ambayo yatajadiliwa na wadau wa sekta hii katika kuboresha mfumo wa elimu nchini.

Miongoni mwa changamoto kubwa zilizojitokeza kutokana na mafanikio hayo ni ubora wa elimu inayotolewa na shule hizo, uhaba wa walimu pamoja na vitendea kazi vikiwemo vitabu na maslahi kwa walimu.

Lowassa ambaye anatajwa kuwa mmoja wa wana-CCM watakaogombea urais mwaka 2015, alisema Tanzania ina bahati ya kuwa na wasomi waliobobea ambao wanaiweza kazi hiyo ya kuangalia iwapo mitaala inayotumika inakidhi haja na matakwa ya karne tuliyonayo

No comments:

Post a Comment