Search This Blog

Thursday, December 13, 2012

Mrithi wa Milovan huyu hapa

KOCHA mpya wa mabingwa wa soka Tanzania Bara, Simba, Mfaransa Patrick Liewig, anatarajiwa kutua nchini leo tayari kuanza kazi ya kukinoa kikosi hicho, imefahamika.

Liewing anashuka kuchukua mikoba ya Mserbia, Milovan Cirkovic, ambaye uongozi wa Simba uliamua kusitisha naye mkataba baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara.

Kuja kwa kocha huyo, kutamaliza uvumi wa atakayechukua mikoba ya Milovan. Hivi karibuni ilidaiwa Mmalawi Kinnah Phiri atapewa majukumu hayo.

Habari za uhakika kutoka ndani ya Simba zinaeleza kwamba, Liewig mwenye shahada ya ukocha, alikuwa akifanya kazi Club Africain ya Tunisia kama Mkurugenzi wa Ufundi, Meneja na pia Meneja wa timu ya wachezaji wa kulipwa.

Kiongozi mmoja wa Simba ambaye hakupenda kutajwa jina lake, aliliambia gazeti hili kwamba, mara baada ya kutua nchini, kocha huyo atasaini mkataba ambako atakuwa akilipwa mshahara wa dola 5,000 za Marekani kwa mwezi.

Aliongeza kuwa, kocha huyo anatarajiwa kuwasili na mshambuliaji kutoka nchini Cameroon, ambaye amependekeza asajiliwe Simba kutokana na ubora alionao.

Kocha huyo ambaye kwa sasa makazi yake yapo nchini Ivory Coast, alizaliwa Oktoba 10, 1950 nchini Ufaransa, ambako pia aliwahi kucheza soka ndani na nje ya nchi hiyo kati ya mwaka 1971 na 1985.

Pia amepata kushiriki kozi mbalimbali za ukocha, ikiwemo ya makocha wakuu, iliyoandaliwa na chama cha soka cha Ufaransa, stashahada ya juu kwa timu za kulipwa na stashahada ya juu kwa vyuo vya soka, ambayo iliendeshwa na aliyekuwa Kocha wa timu ya taifa ya Ufaransa wakati huo, Gerard Houllier.

Aidha, kocha huyo amewahi kufundisha katika shule ya soka ya PSG kuanzia mwaka 1989 hadi 1999, ambako alikuwa akiwajibika katika timu za U-16, U-18 na U-20.

Akiwa PSG, Liewig amefanya kazi chini ya makocha Tomislav IVIC, Henri Michael, Artur Jorge, Luis Fernandez, Ricardo Gomez, Alain Giresse na Philippe Bergeroo.

Mwaka 1999 – 2001, alikuwa meneja wa chuo cha soka cha klabu ya Al wahda ya Abu Dhabi, ambapo aliziongoza klabu za vijana chini ya miaka 18 na 21, kabla ya mwaka 2001 - 2003 kuwa kocha mkuu wa timu za watoto na vijana Falme za Kiarabu.

Mwaka 2004–2009, aliwahi kutumika katika klabu mbalimbali nchini Ivory Coast, ikiwemo Asec Mimosas, huku pia akitunukiwa tuzo ya ukocha bora nchini humo.

Kocha huyo, pia aliwahi kufanya kazi na timu ya taifa ya Misri ‘The Pharaos’ na klabu ya Al Ahly ya nchini humo na klabu mbalimbali nchini Tunisia, Ufaransa, Brazil, Malaysia na Argentina

No comments:

Post a Comment