Search This Blog

Thursday, November 8, 2012

Hoja ya mabilioni ya Uswisi kujadiliwa leo



















Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe

Hoja nane za wabunge zitawasilishwa leo ikiwamo ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, inayohusu Watanzania walioficha fmabilioni ya fedha nje ya nchi.

Mkurugenzi wa Idara ya Shughuli za Bunge, John Joel, alisema hoja nne kati ya nane zitawasilishwa leo na kuwa kila mbunge atapewa nusu saa ya kuwasilisha.

Wengine watakaowasilisha hoja zao ni Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) ambaye hoja yake ni ya ugawaji wa ardhi na Mbunge wa Nzega (CCM), Dk. Khamis Kigwangala (CCM), ambaye atawasilisha hoja yake kuhusiana na sekta ya madini.

Mbunge mwingine aliyepewa nafasi ya kuwasilisha hoja binafsi ni Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia (NCCR Mageuzi) ambaye atazungumzia kiwango cha elimu.

Kesho, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema), atawasilisha hoja binafsi inayohusiana na upatikanaji wa maji safi na salama katika Jiji la Dar es Salaam.

Alisema Mnyika alitakiwa kwenda kusoma kauli iliyotolewa bungeni jana na Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, kwanza ili kuangalia mapungufu yaliyopo na kisha kuyawasilisha kesho.

Hoja nyingine ni ya kukuza ajira kwa vijana itakayowasilishwa na Kigwangalah na ya Mwenendo wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) ambayo itatolewa na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema).

Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM), Mwigulu Nchemba, naye atakuwa na hoja akiitaka serikali kuleta muswada wa Sheria ya kuanzisha Mfuko wa Elimu ya Juu.

Wakati huo huo, wabunge wamelalamikia kutowasilishwa kwa ripoti mbalimbali bungeni.

Walitoa malalamiko yao katika semina ya kujadili Tathmini ya kanuni za Bunge Toleo 2007, iliyofanyika jana.

Chanzo cha habari kutoka ndani ya kikao hicho, kilisema kuwa wabunge hao walitoa mfano wa ripoti ambazo hazikuwasilishwa bungeni kuwa ni ile ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo na ile ya Brigedia Jenerali Mstaafu Hassan Ngwilizi.

Wabunge hao walisema si jambo zuri kwa kuwa ripoti hizo ni mali ya Bunge na si mali ya Spika, hivyo wabunge wanahaki ya kuzifahamu.

Pia wabunge walilalamikia muda wa kuchangia bungeni kuwa ni mdogo na hivyo kutotoa fursa pana kuchangia hoja zinazowasilishwa bungeni.

Aidha, habari kutoka ndani ya kikao hicho zilisema pia wabunge hao walilamikia kuhusiana na utaratibu wa maswali ya papo papo kwa Waziri Mkuu ambao umekuwa ukiwafanya wabunge kuamka asubuhi sana kuwahi nafasi za kuuliza maswali.

Pia pande zote mbili za wabunge wa Chama cha Mapinduzi na wa upinzani kwa nyakati tofauti zilimshutumu Spika kwa upendeleo.

Wabunge wa upinzani walisema wakati mwingine Spika amekuwa akikwepa kuwapa nafasi ili kuikingia kifua serikali isibanwe.

Chanzo hicho kilisema Spika Anne Makinda, aliwataka wabunge kutumia kanuni kulalamika na kwamba kila kitu kitakwenda sawa.

No comments:

Post a Comment