Kesi ya Mzee Mwinyi sasa yafikia patamu
Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi
Mpelelezi Deusdenis (43) katika kesi ya ya wizi wa zaidi ya Sh. milioni 37 za Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, amedai mahakamani kuwa baada ya kuwahoji wapangaji wa nyumba za Mwinyi, alibaini kuwa mshtakiwa alizitumia fedha hizo kwa matumizi yake binafsi badala ya kuzikabidhi kwa mwenye nyumba (Mwinyi).
Mpelelezi huyo ambaye ni shahidi wa sita wa upande wa mashtaka katika kesi hiyo, alitoa madai hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi, Genivitus Dudu, anayesikiliza kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.
Mshtakiwa katika kesi hiyo ni Abbdalla Mzombe anayekabiliwa na kesi ya wizi wa zaidi ya Sh. milioni 37 baada ya kuaminiwa na Mwinyi kusimamia na kukusanya kodi ya nyumba zake mbili zilizopo Mikocheni B na Msasani jijini Dar es Salaam.
“Julai 12, mwaka huu niliitwa na bosi wangu Inspekta Filbert akaniagiza nimhoji mshtakiwa ambaye alikuwa mahabusu ya Kituo cha Polisi Oyesterbay, nilimhoji akanieleza kwamba alikusanya kodi kutoka kwa wapangaji wanne aliowapangisha kwenye nyumba ya Mikocheni na alifanyia ukarabati na zilizobaki alimkabidhi Mzee Mwinyi,” alidai shahidi huyo na kuongeza:
“Lakini Mzee Mwinyi amekanusha kupokea fedha kutoka kwa mshtakiwa… pia mshtakiwa alipokea Sh. milioni 19.8 kwa awamu kutoka kwa mpangaji wa nyumba ya Msasani, zote alizitumia kwa matumizi yake binafsi badala ya kumkabidhi mmiliki wa nyumba hizo,” alidai Deusdenis wakati akiongozwa na wakili wa serikali Charles.
Mshtakiwa alikiri kwamba aliingia mikataba na wapangaji kati ya Juni mwaka 2011 na Juni 2012 na kuwa fedha alizozipata anaamini amezitumia kwa matumizi yake binafsi.
Agosti 21, mwaka hu,u Mzombe alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza akidaiwa kwamba kati ya Januari 2011 na Julai 2012 katika maeneo ya Mikocheni Dar es Salaam, akiwa mfanyakazi wa Ali Hassan Mwinyi aliiba Sh. 17,640,000 alizokusanya kodi katika nyumba namba 481 plot A eneo la Mikocheni kwa ajili ya kodi mwaka 2011/2012 na 2012/2013 alizotakiwa kuzikifikisha kwa Mwinyi, lakini hakufanya hivyo.
Mshitakiwa pia anadaiwa katika kipindi hicho maeneo ya Msasani Village, aliiba Sh. 19,800,000 alizokusanya kodi katika nyumba namba 55 block C Msasani Village kwa ajili ya mwaka 2011/2012 na 2012/2013. Mshitakiwa alikana mashitaka na yuko ndani kwa kukosa dhamana
No comments:
Post a Comment