BAVICHA yaanika hujuma za CCM
BAADHI ya vigogo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kushirikiana na viongozi waandamizi wawili wa CHADEMA wamedaiwa kufadhili vijana wa BAVICHA kuhujumu chama hicho.
Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Taifa wa Baraza la Vijana La CHADEMA (BAVICHA), John Heche, wakati akizungumza na waandishi wa habari kueleza sababu za kuwavua uongozi baadhi ya wanachama wao na kusimamishwa wengine kutokana na usaliti.
Heche, hata hivyo, hakuwataja kwa majina viongozi hao wa CHADEMA akisema kuwa wako nje ya mamlaka ya baraza analoliongoza, ingawa vyanzo vyetu vya ndani vilibaini kuwa ushahidi wa moja kwa moja ulimtaja Mbunge wa Maswa Mashariki, John Shibuda.
Kwa upande wa viogogo wa CCM, Heche alimhusisha moja kwa moja Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira, kuwa nyuma ya watu waliokuwa wakikichafua chama.
Alisema mwaka jana Wasira alikuwa akitoa kauli ya mara kwa mara kuwa mwaka 2013 CHADEMA itakufa kwa kuwa alikuwa anajua kuna watu atawatumia ndani ya CHADEMA kwa ajili ya kutaka kujaribu kufanikisha kauli yake hiyo.
“Sisi tulijiuliza huyu anapata wapi ujasiri wa kusema CHADEMA itakufa wakati ndiyo kwanza inazidi kunawiri? Tukajua mwenye uwezo wa kujua hiki chama kitakufa lini ni mwenyezi Mungu.
“Kumbe mwenzetu alikuwa na watu wake ndani ya chama waliomhakikishia kifo hicho, sasa tumewatimua akaanze upya,” alisema.
Heche alifafanua kuwa hivi karibuni kamati ya utendaji ya BAVICHA ikikutana jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kupokea na kujadili taarifa za utendaji kazi na uhai wa baraza nchi nzima kutoka mikoa yote ya kichama.
Aliongeza kuwa miongoni mwa maazimio ya kamati hiyo yalikuwa ni kupokea na kujadili taarifa ya kamati ndogo ya BAVICHA iliyopewa kazi ya kuchunguza tuhuma za baadhi ya viongozi na wanachama wake.
Baada ya kupokea taarifa hiyo walibaini kuwa baadhi ya viongozi na wanachama wana hatia na kuwachukulia hatua zilizostahili kwa mujibu wa katiba ya BAVICHA.
Alimtaja kiongozi aliyevuliwa madaraka na ambaye pia atakuwa amepoteza sifa ya kuwa mwanachama wa CHADEMA kuwa ni aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wao, Juliana Shonza, huku wanachama wa kawaida waliovuliwa uanachama wa BAVICHA wakiwa Habib Mchange na Mtella Mwampamba.
Wanachama waliopewa onyo ni Gwakisa Mwakasando, Joseph Kasambala ambaye ni mwenyekiti wa BAVICHA mkoa wa Mbeya pamoja na Ben Saanane.
Hata hivyo, Wilson Makala wa Babati, hakuwa miongoni mwa wanachama waliosimamishwa kwa muda kama ilivyoripotiwa kimakosa na gazeti hili.
Heche alisema Shonza katika nafasi yake ya Makamu Mwenyekiti, alikuwa akishirikiana na baadhi ya watu kupanga njama na kufanya usaliti dhidi ya BAVICHA, chama na vijana wenzake wapenda mabadiliko.
Alisema katika mikutano hiyo ya siri kwa manufaa ya CCM, Shonza alikuwa akiwakusanya vijana wanafunzi wa vyuo vikuu mbalimbali waliosimamishwa masomo au kufukuzwa vyuoni ambao ni wanachama wa Shirikisho la Wanachadema wa Vyuo Vikuu (CHASO) na kuwarubuni.
“Juliana alifanya kazi yake hiyo kwa ushawishi wa hongo, ili wakubali kuitisha mikutano na waandishi wa habari, watoe matamko machafu dhidi ya CHADEMA na viongozi wake wakuu, akiwamo Dk. Willibrod Slaa na Freeman Mbowe,” alisema.
Alitaja moja ya mikutano hiyo kuwa ni ile iliyofanyika katika Bar ya Highland Makumbusho na kuwaita viongozi wa CHASO na kuwashawishi kuwa watakuwa na maisha mazuri, watarudishwa vyuoni na kutunzwa vizuri hapa mjini kama anavyoishi yeye endapo wangelikubali kufanya kazi hiyo.
Heche aliongeza kuwa Juliana alishiriki kikao kingine kwa ajili ya kuihujumu CHADEMA cha Desemba 6 mwaka jana katika Hoteli ya MIC kuanzia saa 12 jioni akiwa na baadhi ya wasaliti wengine.
Pia alisema Juliana alikaa na kushiriki vikao vya kuanzisha chama kipya kinachoitwa Chaumma, kushiriki katika makundi yaitwayo Masalia na PM7 ambayo yote yalikuwa na lengo la kuvuruga chama na kuwakosanisha wanachama.
“Kama tutashindwa kuwajibishana wenyewe kwa wenyewe katika makosa yenye ushahidi kama huu basi tutakuwa hatuna sababu ya kupewa nchi mwaka 2015 kwa kuwa hawa wasaliti hawawaathiri Wanachadema tu bali kila Mtanzania mpenda mabadiliko,” alisema
No comments:
Post a Comment