MFUMO WA UCHAGUZI KATIKA JAMHURI YA MUUNGANO
Mfumo wa uchaguzi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania utafuata misingi ifuatayo:
1. Kila raia wa Jamhuri ya Muungano aliyetimiza umri wa miaka kumi na nane atakuwa na haki ya kupiga kura na kugombea nafasi yoyote ya uongozi wa kuchaguliwa katika Jamhuri ya Muungano.
...
2. Haki ya kupiga kura na kugombea kuchaguliwa katika nafasi yoyote ya uongozi haitafungwa na masharti yoyote yanayohusu uanachama wa chama cha siasa au mahali pa kuzaliwa kwa mgombea husika.
3. Mamlaka husika zitaweka utaratibu wa kisheria wa kuwawezesha watu wenye haki ya kupiga kura lakini wanaishi nje ya Jamhuri ya Muungano au walioko chini ya usimamizi wa vyombo vya kurekebisha tabia za wahalifu kutimiza haki yao ya kupiga kura.
4. Chaguzi zote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zitafanyika chini ya usimamizi wa Tume huru ya Uchaguzi ya Tanganyika na Tume ya Uchaguzi Zanzibar.
5. Tume huru ya Uchaguzi ya Tanganyika itakuwa na Wajumbe wafuatao:
(a) Wajumbe kumi na tano watakaopendekezwa na vyama vya siasa vyenye uwakilishi katika Bunge la Tanganyika kwa kufuata uwiano wa Wabunge katika Bunge;
(b) Wajumbe watatu watakaopendekezwa na vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu lakini ambavyo havina uwakilishi katika Bunge la Tanganyika;
(c) Mjumbe mmoja atakayependekezwa na Chama cha Mawakili wa Tanganyika;
(d) Mjumbe mmoja atakayependekezwa na taasisi zisizokuwa za kiserikali;
(e) Mjumbe mmoja atakayependekezwa na vyama vya kitaaluma vya taasisi za elimu ya juu zinazotambuliwa na mamlaka ya ithibati ya Tanganyika;
(f) Wajumbe wawili watakaopendekezwa na taasisi za kidini;
(g) Wajumbe wawili watakaopendekezwa na Tume huru ya Utumishi wa Mahakama ambao watakuwa majaji wastaafu wa Mahakama ya Rufani ya Tanganyika.
6. Wajumbe wa Tume huru ya Uchaguzi watachagua Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Tume kutoka miongoni mwao, ili mradi Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti watakuwa ni watu wenye sifa ya kushikilia madaraka ya Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanganyika.
7. Wajumbe wa Tume huru ya Uchaguzi hawatashikilia madaraka ya Mjumbe wa Tume kabla uteuzi wao haujathibitishwa na Bunge la Tanganyika.
8. Tume huru ya Uchaguzi itakuwa na mamlaka ya kuteua mtu yeyote mwenye sifa kuna Mkurugenzi wa Uchaguzi na Mtendaji Mkuu wa Tume.
9. Tume huru ya Uchaguzi itakuwa na mamlaka ya kuteua watendaji wake yenyewe katika ngazi zote kuanzia ngazi ya taifa, Jimbo, Wilaya na katika Majimbo ya uchaguzi. Wasimamizi wa uchaguzi katika ngazi ya majimbo, majimbo ya uchaguzi na wilaya watakuwa ni watumishi wa Tume huru ya Uchaguzi wakati wasimamizi wasaidizi na wasimamizi wa vituo watakuwa watu walioteuliwa na Tume kwa utaratibu wa wazi na kwa vyovyote vile hawatakuwa watu walioko katika Utumishi wa umma;
No comments:
Post a Comment