CHADEMA si kuvaa ‘kombati’
NIMEGUSWA sana na mfululizo wa makala za Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Kabwe Zitto, zinazoendelea kutolewa katika gazeti hili.Katika mfululizo huo, Jumalipili iliyopita aligusia misingi ya chama hicho akisema ‘fuata misingi; Ujenzi wa CHADEMA imara. Humo alijaribu kugusia ni wapi chama hicho kimetoka kiasia hadi kufikia hatua hii ya kuvuma kila kona ya nchi.
Zitto ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Kaskazini, anajaribu kueleza jinsi chama hicho kilipigana na kushiriki chaguzi zote tangu mwaka 1995, lakini kikishirikiana na vyama vingine kwenye nafasi ya urais hadi mwaka 2005 ambapo, Freeman Mbowe, aligombea kiti hicho.
Alisema mazingira hayo ya chama cha tano kwa wingi wa kura katika vyama vyote vya siasa nchini ndiyo mazingira iliyoingia nayo CHADEMA katika uchaguzi wa mwaka 2005.
“Mazingira ya kukatisha tamaa, kwani ujanja mjini haukuwa kwa CHADEMA; bali CUF au TLP na zaidi CCM. Mazingira ya kijana ukisema upo CHADEMA vijana wenzako wanakuangalia jicho la mshangao na hata kuchekwa,” anasema Zitto.
Kwamba hayo ndiyo mazingira ambayo alirithi Freeman Mbowe, kama mwenyekiti wa CHADEMA.
Alianza harakati zake za kuimarisha CHADEMA kwa kukusanya vijana mbalimbali, wanachama na wasio wanachama.
Vijana hao walitoka makundi mbalimbali ya jamii kama wanafunzi wa vyuo vikuu, waandishi wa habari, wanasiasa kutoka vyama vingine na hata vijana wanaharakati katika NGOs na kwingine.
Zitto anasema mwaka 2004 mwezi Machi, Mbowe akachaguliwa kuwa mwenyekiti wa tatu wa CHADEMA, hivyo kuwa na mamlaka zaidi ya kuleta mabadiliko katika chama.
Kwamba wanasiasa wanataaluma wa kila aina nao pia walijiunga na CHADEMA kipindi hicho. “Kuna kipindi tulikuwa tunajiita ‘Real Madrid’ maana tulikusanya ‘mastaa’ wote kutoka vyama vya upinzani.”
Freeman Mbowe aliifanya kazi hii ili kutoa fursa kwa Watanzania wengine kujenga chama imara cha siasa nchini ili si tu kuimarisha demokrasia nchini, bali pia kutoa mbadala kwa chama tawala na hata vyama vingine vya upinzani.
“Utekelezaji wa msingi huu wa chama umelipa. Haikuwa kazi rahisi, bali ni kazi makini yenye ujasiri wa kuepuka kujifanya Mbowe ndiye chama na badala yake kujenga chama taasisi ambapo wanachama wanaweza kusema demokrasia ndiyo CHADEMA.
Kwamba chini ya uongozi wake, Mbowe ameshirikiana na viongozi wenzake kupandisha chama kutoka chama cha tano mwaka 2000 mpaka chama cha pili mwaka 2010.
Zitto ni miongoni mwa vijana na Watanzania waliopata fursa ya kuchangia mabadiliko katika nchi kupitia juhudi hizi za Mbowe, hivyo kuifikisha CHADEMA hapa ilipo leo.
Anasema kuwa chama kilichojaa ufuasi wa watu kitapasuliwa na nyufa za uongo, fitna, chuki, majungu na kujipendekeza. Chama cha misingi ndiyo chama tunachopaswa kujenga na kujivunia nacho.
Ni ujasiri wa kufuata misingi ndiyo unaweza kumfanya kiongozi mwenye timu iliyojaa watu wenye vipawa mbalimbali na uwezo mkubwa wa kuvutia ‘wafuasi’ kama CHADEMA kumudu jahazi na kuliendesha vema.
Nimeanza kwa kumnukuu kaka na rafiki yangu Zitto ili kujenga msingi wa mada yangu leo.
Ninachojaribu kusema ni tofauti ya wanasiasa makini vijana ndani ya chama na wafuasi wanotaka kuonekana ili kukidhi maslahi.
Hoja ya Zitto iko wazi kuwa mafanikio ya kisiasa ni kujitoa kwa kila namna, waweza kudharaurika, kuzushiwa, kutuhumiwa na kutukanwa lakini kama unafanya jambo la msingi kwa manufaa ya wengi, utafanikiwa.
Kwa bahati mbaya, CHADEMA inakoelekea inaanza kuzingirwa na vijana wengi wasio na sifa za misingi alizozieleza ndugu yangu Zitto. Wengi wanaoingia huko wamekata tamaa na mfumo wa utawala wa CCM.
Vijana hawa wa kileo wanaingia CHADEMA kama tumaini, lakini bado wanahitaji kufundwa waijue misingi na maelngo ya chama kuwa si kuvalia ‘kombati’ kutoa matamko kila kukicha na kugombania vyeo na fedha.
Kasoro hii ndiyo imeanza kuwatafuna baadhi ya viongozi wa Baraza la Vijana Taifa la CHADEMA (BAVICHA), hivyo kukubali kutumika kama mawakala wa mafisadi kukihujumu chama chao kwa bei ndogo.
Laiti hawa wangekuwa na misingi anayoileza Zitto wangikuwa nawashinda kwenye mitandao ya kijamii wakijaribu kuandika taarifa za kuwakashifu viongozi wao wakuu kwa kutumia majina ya bandia, badala yake wangekuwa kama Mbunge wa Arusha Mmjini Godbless Lema.
Desemba 30 mwaka jana, niliandika makala yenye nikisema CHADEMA iwafunde BAVICHA mwaka 2013.
Nileleza kuwa mwaka 2012, ulikuwa na hekaheka nyingi kila nyanja lakini nikampongeza Godbless Lema, ambaye kwangu namwona kama mkomavu kisiasa.
Nikasema kuwa laiti CHADEMA ikipata vijana makini 20 kama Lema ikawasambaza mikoani kuwatia wananchi matumaini kuwa ukombozi mpya unawezekana bila kulaghaiwa kwa fedha na kurahisisha kazi ya kueleke Ikulu 2015.
Nilikumbusha jinsi Lema alivyovuliwa ubunge na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha Aprili 5, mwaka huu lakini kwa takribani miezi tisa aliyokaa nje ya Bunge akisubiri uamuzi wa rufaa yake katika Mahakama ya Rufaa Tanzania, alihangaika kukisambaza chama kwa umma.Darasa la Lema limetosha kuwafunda vijana wa CHADEMA kufuata misingi alioieleza Zitto, hivyo kujitathmini na kujipima kama wanaweza kasi ya chama hicho kuwa ni kuwatumikia wananchi bila kutanguliza ubinafsi.
Hizi kasoro tulizozisikia kwa BAVICHA kuwa wanatumiwa na mamluki kukisambaratisha CHADEMA, zinatokana na vijana husika kutokulia kwenye misingi ya uwazi. Hawa wametanguliza ubinafsi na tamaa ya mali na vyeo.
Kumbe iko kila sababu ya Mbowe kuendeleza darasa lake la misingi ya chama ili wafuasi wao wajue kuwa CHADEMA si kuvaa ‘kombati’ na kupayuka kwa kukinzana wenzako.
Anayefanya sarakasi za ajabu kama baadhi ya vijana hao wa BAVICHA waliotimuliwa uanachama, huyo atambue kuwa ndani ya CHADEMA kumbe anakuwa amepotea njia, bora akabaki CCM ili atumike vizuri kuvuruga vuguvugu la mabadiliko.
Wito wangu kwa vijana wapenda mabadiliko walioko ndani ya CHADEMA na vyama vingine, nawasihi watambue kuwa siasa ya leo ni ngumu hasa kwa yule anayeifanya bila kukubali kuwa kibaraka wa watafuta vyeo na madaraka. Tafakari
No comments:
Post a Comment