Mbunge, Magufuli wampinga Mwakyembe
MBUNGE wa Ilemela mkoani Mwanza, Highness Kiwia (CHADEMA), ameungana na Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, kupinga agizo la Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe kuhusu kufungwa barabara kuu ya Igombe-Kayenze iendayo katikati ya Jiji la Mwanza.Akizungumza kwa simu na gazeti hili jana, Kiwia alisema kauli ya Waziri Mwakyembe kutaka barabara hiyo ifungwe ili kupisha upanuzi wa uwanja wa ndege wa jijini hapa, haina tija kwa wananchi kwani hadi sasa hakuna maandalizi yoyote ya upanuzi yanayoendelea.
Alisema kuwa ili barabara hiyo ifungwe, ni lazima serikali ijenge njia nyingine mbadala kwa ajili ya wananchi, na kwamba ni vema wizara hizo mbili za Uchukuzi na Ujenzi zikalipatia ufumbuzi wa haraka sana suala hilo.
Kauli ya Kiwia imekuja siku mbili baada ya Waziri Magufuli aliyefanya ziara ya siku moja jijini hapa, kupinga agizo la Waziri Mwakyembe ambaye hivi karibuni naye alifanya ziara kukagua mradi huo kisha kuagiza barabara hiyo ifungwe mara moja ili kupisha upanuzi huo unaotarajiwa kuchukua muda wa miezi 24.
"Mimi kama mbunge wa Ilemela, naungana na Waziri wa Ujenzi, Dk. Magufuli kupinga agizo la Waziri wa Uchukuzi, Dk. Mwakyembe kuhusu kufungwa kwa barabara ya Igombe-Kayenze ili kupisha upanuzi wa uwanja, lakini pia nashangaa mawaziri hawa wanakuja bila kunishirikisha mbunge wa eneo husika,” alisema.
Alisema anamwomba Waziri Mwakyembe asimuelewe vibaya kwa kuwa hapingi kauli yake kwa nia mbaya, bali anakataa barabara kufungwa bila kujengwa njia mbadala ya kuwawezesha wananchi kupita.
Kiwia pia alieleza kushangazwa na mgongano huo wa wizara mbili kuhusu barabara hiyo, akisema inawezekana serikali imetenga fedha za upanuzi wa uwanja huo kisha kusahau kutenga bajeti ya ujenzi wa barabara mbadala wakati wa upanuzi.
Kuhusu mkandarasi wa Kampuni ya Beijing Construction Engineering Group (BCEG) aliyepewa kazi ya upanuzi wa mradi huo kuchelewa kuanza kazi kwa mujibu wa mkataba, Kiwia aliitaka Bodi ya Makandarasi nchini (TRB) kwa kushirikiana na serikali kumchukulia hatua za kisheria.
Akiwa jijini Mwanza juzi, Waziri Magufuli alisema licha ya serikali kumlipa mkandarasi huyo zaidi ya sh bilioni 8 kwa ajili ya kazi hiyo, lakini hadi sasa maandalizi yake ni asilimia 30 tu
No comments:
Post a Comment