Pinda: Uchumi wa Tanzania utakua maradufu
WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, amesema uchumi wa Tanzania utaendelea kukua maradufu kutokana na mifumo bora ya uwekezaji iliyopo, hali itakayosaidia pia kushindana katika soko la Afrika Mashariki.Pinda alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa duka la kusambaza bidhaa za Beko kutoka Uturuki, zikiwemo televisheni, friji na majiko ya umeme.
Alisema fursa muhimu ndizo zinazovutia wawekezaji kuja nchini na pato la nchi kuendelea kukua maradufu.
Alisema mara zote Tanzania imekuwa katika kutafuta masoko na wawekezaji, hivyo kuzinduliwa kwa duka hilo ni ishara kuwa nchi imepiga hatua kwenye maendeleo.
“Uwepo wa Beko ni matunda bora ya serikali yetu… rais wetu alitembelea Uturuki na alikutana na rais wao huko na kuhimiza wawekezaji kuja nchini. Hii ni moja ya matunda ya ushirikiano katika kukuza uchumi,” alisema Pinda.
Aidha, Pinda aliishauri Kampuni ya Modern Holdings (EA) Limited, inayosimamia bidhaa za Beko nchini na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kufungua maduka mengi zaidi nchini.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kampuni hiyo, Anselm Minja, alisema bidhaa za Beko zitapatikana nchini kote kwa kufungua maduka sehemu mbalimbali kama walivyoombwa na Pinda.
No comments:
Post a Comment