Search This Blog

Friday, October 12, 2012

Lowassa aiteka CCM Arusha


CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Arusha kimehitimisha chaguzi zake jana, huku kambi ya Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, ikishikilia usukani baada ya kushinda nafasi nzito zilizobaki.

‘Watu’ wa Lowassa waliopeta katika uchaguzi wa jana ni pamoja na Hilal Sood aliyeshinda nafasi za Katibu wa Uchumi, Fedha na Mipango na Isack Kadogoo aliyeutwaa ukatibu wa Siasa, Itikadi na Sera.

Aidha Mwenyekiti wa CCM mkoani hapa, Onesmo Ole Nangole, alitumia mamlaka yake kwa mujibu wa katiba ya chama hicho kuteua wajumbe wawili watakaoingia kwenye Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM mkoa ambapo walioteuliwa ni Fabiola Maami na Julius Kalanga ambaye awali aliomba kugombea nafasi ya Katibu wa Uchumi, Fedha na Mipango lakini jina lake lilikatwa.

Akitangaza matokeo hayo, Nangole alisema kuwa kwenye nafasi ya Katibu wa Siasa, Itikadi na Uenezi. Kadogoo aliibuka mshindi kwa kupata kura 41 akimbwaga mpinzani wake, Loota Sanare aliyeambulia kura 27 kati ya 68 zilizopigwa.

Sood aliyewahi kuwa Meneja wa Kanda ya Kaskazini wa Benki ya NMB, alishinda nafasi ya Katibu wa Uchumi, Fedha na Mipango kwa kupata kura 41 huku mpinzani wake, Juma Losine ambaye alikuwa na uhakika wa ushindi kabla ya upepo kubadilikia jana asubuhi, aliambulia kura 21.

Nangole alitangaza majina ya wajumbe watano waliochaguliwa kuingia kwenye Kamati ya Siasa ya Mkoa kuwa ni Paulo Kiteleko, Adamu Chora, John Palangyo, Esta Maleko na Fabiola Deogratius.

Juzi, Nangole alishinda nafasi ya uenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM Mkoa wa Arusha na kumtimulia vumbi mpinzani wake anayesemekana kuwa mfuasi wa Bernad Membe

No comments:

Post a Comment