Utajiri huu wa Lowassa unatoka wapi?
ANDREW McPHERSON MANDARI Jr
Haya nimawazo yangu binafsi nikiwa natafakari kwa kina juu y nani atakaye kuwa kiongozi wa taifa ili la tanzania lenye nyufa na matatizo ya kutisha kiuchumi,utawala,afya,maendeleo,uzalihaji na utunzani wa rasilimali za taifa ili lililobarikiwa kila aina ya utajiri,Na moja ya hisia zangu nikwa hawa wanao anza sasa kutengeneza mitandao ta kwenda ikulu na kutaka watanzania kuwapa ridhaa ya kuiongoza nchi hii.
Moja ya hisia iliyojikita kwa walio wengi ndani ya nchi, ni kumhusisha Mbunge wa Monduli (CCM) ambaye pia ni Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Ngoyai Lowassa na `utajiri wa kutupwa.’
Wapo wanaoamini kwamba Lowassa ni miongoni mwa matajiri `wasioshikika’ ndani ya ardhi ya Tanzania. Wanaamini hivyo na wataendelea kuamini hivyo.
Wapo wanaoamini kwamba kutokana na hilo, Lowassa anakosa mamlaka na sifa za utumishi wa umma, hasa kushika nafasi kubwa ya uongozi wa nchi.
Katikakati ya hali hiyo, Lowassa anajitokeza, ‘akimwaga’ misaada kupitia hafla tofauti anazoalikwa, zaidi ikiwa kwenye nyumba na taasisi za kidini.
Muda mfupi akitokea ‘mapumzikoni’ baada ya kuachia ngazi, akaandika barua ya kujiuzulu Uwaziri Mkuu, Lowassa ameonekana zaidi ‘akimwaga’ misaada kwa jumuiya za watu.
Si kosa kibinadamu pale aliye nacho kuwasaidia wahitaji, kwa maana ni sehemu ya kujiwekea hazina mbinguni. Wanadamu tunaamini hivyo
Si dhambi kwa kiongozi wa umma kutumia sehemu ya pato lake la ziada, ‘kuwalisha’ masikini. Kwa maana imeandikwa, hilo ni jambo jema, tena jema sana.
Lakini ulimwengu unaotawaliwa na maadili chanya ya utumishi wa umma, ipo haja ya kujiuliza, Lowassa anapata wapi mamilioni ya Shilingi ‘anayoyamwaga’ kwa jumuiya za watu mithili ya mfadhili anayetoka taifa lenye nguvu kubwa ya uchumi duniani?
Nimewahi kushiriki hafla na shughuli tofauti za kibinadamu zilizomhusisha Lowassa, kwa nyakati na maeneo tofauti.
Nimewahi kushirikiana na sehemu ya familia yake katika mambo tofauti. Sina chuki, sina hila, sina inda, sina gubu, sina ghiliba wala ubaya wa aina yoyote dhidi ya Lowassa.
Nikishiriki shughuli zake rasmi, hasa akiwa Waziri wa serikali, niliziona karama za uongozi za Lowassa. Niliuona uwezo wake, ufuatiliaji, ujasiri wa kukabiliana na changamoto nzito na hata kutoa na kufuatilia maagizo.
Vyote katika ujumla wake, alivifanya akiwa mtumishi wa umma, anayepaswa kuyaishi maadili ya utumishi huo, na kuyafanya kuwa sehemu ya taswira chanya, ikiwemo inayohusisha sifa na karama hizo.
Lakini, kuibuka kwake hadharani na ‘kumwaga’ misaada mithili ya mfadhili wa ughaibuni, ama mfanyabiashara anayetoa sehemu ya faida ndani ya uzalishaji wake kiwandani, kunabeba msingi wa kuhoji, Lowassa anazipata wapi fedha hizo?
Anaweza kumiliki vitega uchumi mbalimbali vinavyompatia fedha za ziada, akafikia hatua ya ‘kuzimwaga’ kwa mtindo wa misaada. Akiwa mtumishi wa umma, umma unavijua ili kuondokana na hisia hasi dhidi yake?
Ama kama hana vitega uchumi, bali kutegemea fungu linalotokana na kodi za wananchi, vyanzo vinavyomuingizia mamilioni hayo hayo ni vipi?
Inawezekana akawachangisha marafiki, ndugu na jamaa zake, ikiwa hivyo, ni akina nani? Kwa mfumo na lengo gani? Watu wanajiuliza!
Kwa maana Lowassa si ‘mtu mdogo’ kwa nchi, hivyo kila aina ya jambo analoshiriki lina athari za kitaifa, ikiwemo kubadili na kuzielekeza fikra za umma mpana, kwa kadri ya mazingira na matukio.
Kushiriki kwake kugawa misaada huku watu wakimtambua yumo katika kada ya utumishi wa umma na si mfanyabiashara `aliyekubuhu’ kama Mustapha Sabodo, kunaibua utata. Kunahitaji jawabu.
Lowassa hajulikani kwa kuwa na viwanda vya uzalishaji kama alivyo Said Salim Bakhresa. Hana kampuni za kibiashara kama Aga Khan. Kama vipo basi ni kwa kificho. Ikiwa ni hivyo, inamstahili?
Lowassa anajulikana kuwa mtumishi wa umma, aliyezaliwa mwaka 1953, akifikia ngazi ya Uwaziri Mkuu, alipoteuliwa Desemba 29, 2005, akaapishwa siku inayofuata, kisha ‘kuachia ngazi’ Februari 7, 2008.
Amewahi kuwa waziri tangu wakati wa utawala wa awamu ya pili, chini ya Rais wa wakati huo, Alhaj Ali Hassan Mwinyi.
Mwaka 1995, akajitokeza kuwa miongoni mwa wanachama wa CCM waliotaka kuteuliwa kuwania urais, akishirikiana kwa karibu sana na Rais wa sasa, Jakaya Kikwete, wakati huo wakipachiwa jina la ‘Boyz II Men’.
Hata hivyo, kama ilivyokuwa kwa Kikwete, Lowassa hakuteuliwa, lakini zaidi ikasemekana Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, alishinikiza kuondolewa kwake, kigezo kikiwa ni ‘hafai’ kwa nafasi hiyo.
Unapopitia vyanzo tofauti za taarifa na maelezo yake binafsi, hakuna mahali panaposhawishi kujiridhisha kwamba, kwa nafasi yake anaweza kuwa na uwezo mpana wa ‘kumwaga’ misaada kiasi hicho.
Wapo wanaoweza kuitafsiri makala haya kwa mtazamo hasi dhidi ya Lowassa, lakini nikitambua ‘ukubwa’ wake kwa jamii ya Watanzania, ninashawishika kuamini kwamba maisha na utendaji kazi wake, lazima vinategemea ushauri.
Hivyo wapo washauri wa Lowassa katika maeneo tofauti, ambao bila shaka, miongoni mwao wanamshinikiza kushiriki ‘changia-changia’ inayoibua maswali kwa jamii, anazipata wapi fedha hizo?
Walio wengi wanatambua taswira hasi aliyonayo kwa umma, kiasi cha kufikia hatua ya kujisafisha mara kwa mara, ikibdi kwa kutumia maandiko matakatifu.
Si peke yake, bali hata walio karibu, wale wanaoweza kutambulishwa kama washirika ama ‘wapambe’ wake, wanaifanya kazi ya kulisafisha jina lake.
Lakini jina litasafishika vipi ikiwa bado anashiriki matendo yanayotiliwa shaka, hasa yakihusisha utoaji fedha zilizo mamilioni katika hesabu yake, na ambazo watumishi wengine wa umma hawana uwezo huo?
Walio katika kada ya utumishi wa umma na washauri wao, wanapaswa kujifunza jambo hili, kwamba Watanzania wanahitaji maendelea na suluhu ya matatizo yao vitokane na rasilimali za umma.
Hali hiyo itasaidia kutenganisha utendaji kazi wa watumishi wa hao kwa upande mmoja, na wafadhili kwa upande mwingine. Nchi itasonga mbele zaidi
contact:0712 466109, 0767466109
Email_mcphersonandrews@gmail.com
No comments:
Post a Comment