Search This Blog

Tuesday, October 16, 2012

Vurugu zisiendekezwe kwa kisingizio cha kulinda imani.
















AMANI na utulivu ni sifa zinazoitambulisha Tanzania nje ya mipaka na kuzifanya nchi zenye machafuko kuitamani.

Watanzania wamekuwa wakisikia, kusoma na kuona kupitia televisheni, intaneti na njia nyingine za mawasiliano, namna watu duniani wanavyouana, kuharibiana mali na kufanyiana vitendo vya udhalilishaji, kutokana na tofauti za kiimani (kidini), kisiasa na kitamaduni.

Katika vipindi tofauti vya karibuni, tumeshuhudia mamilioni ya watu wakipoteza maisha katika maeneo mbalimbali nje, huku mali zao zikiharibiwa kwa sababu za kiimani ambazo zingeweza kumalizwa bila madhara.

Aidha, kutokana na asili ya kiutawala ya maeneo hayo, nchi nyingi zinazoingia kwenye machafuko na vurugu za kidini, zinaongozwa kwa misingi ya dini, tofauti na Tanzania, inayoongozwa kwa mujibu wa sheria.

Nchini dini zinathaminiwa na kuheshimiwa na Serikali kwa uzito unaostahili, ndiyo maana hakuna mwanadini anayefanyiwamambo mazuri au mabaya kwa sababu ya imani yake au kwa kuwa ni mtu wa dini fulani.

Tunajionea wahubiri kutoka madhehebu tofauti ya dini nchini wakifanya mikutano yao hadharani na kwenye vyombo vya ibada bila kubughudhiwa, hali inayothibitisha kuwa dini zote ni huru nchini.

Lakini, pamoja na uhuru wa kuabudu na kuhubiri, unapofuatilia kwa makini mahubiri ya baadhi ya wahubiri kutoka dini kuu zilizoko nchini - Ukristo na Uislamu, utagundua matumizi mabaya ya maneno yanayokashifu waumini, vitabu vya dini au misingi ya dini wasizoabudu wahubiri hao.

Hata hivyo, kutokana na uelewa wa waumini wa dini zinazokashifiwa, mahubiri ya aina hiyo hayajapata nafasi ya kusababisha mapigano nchini, licha ya ukweli kwamba wahubiri wanayatoa kwa uwazi kupitia vyombo vya mawasiliano ya umma kama redio na televisheni, vinavyotumiwa na wanaowalenga.

Wafuatiliaji wa mahubiri hayo watakuwa mashahidi wangu kwamba yanatoka nje ya mstari na kuvuka mipaka ya mafundisho ya kiimani yanayostahili, kwani isivyotarajiwa, yanabeba maudhui yenye siasa za uchochezi dhidi ya dini nyingine, ambazo kama waumini wake wasingekuwa waelewa, kungezuka machafuko yasiyoelezeka.

Nawapongeza wana dini zote wanaochambua mambo kabla ya kuyachukulia hatua, kwa sababu kufanya kwao hivyo kumeweza kuiepusha nchi na vurugu za kidini zisizo na tija.

Aidha, ninakemea wanaojivisha udini wasiofuata misingi yake kwa lengo la kutekeleza matakwa yao, kwa kuwa wakifanyacho si mapenzi ya Mungu, bali uhalifu unaokwaza utawala wa duniani unaotambuliwa na Mungu pia.

Nasema hivyo nikilenga vurugu zilizotokea Mbagala Ijumaa na kusababisha uharibifu wa mali kama makanisa, vifaa vya kwaya na magari, baada ya habari za mtoto wa miaka 14 kukojolea kitabu cha Korani akitaniana na mtoto mwenzake (12) kulifikia kundi la watu wanaoelezwa kuwa Waislamu, waliokosa uvumilivu na kuvamia kituo cha Polisi Mbagala kumsaka mtoto waliyedai alikashifu imani yao, ili wamwadhibu.

Watu hawa walichafua hali ya hewa kwa jambo dogo na la kitoto, kwa sababu baada ya kumkosa mtoto huyo, waliharibu mali kwa madai ya kulinda imani yao.

Nafikiri walitaka kujaribu kwa vitendo mambo wanayoyaona kwenye televisheni bila kujali madhara, kwa sababu mkasa uliotokea unajieleza wazi kuwa ulihusisha udadisi wa mtoto usio na hila zozote za kidini.

Kwa mujibu wa Polisi Dar es Salaam, mtoto huyo alitaka kuthibitisha kile alichoambiwa na mwenzake kwamba angegeuka panya au nyoka, endapo angekojolea kitabu hicho. Kitendo hicho kilitokana na akili yake ya kidadisi ambayo, Waislamu hao walipaswa kuifikiria na kusamehe badala ya kufanya walichokifanya.

Uchunguzi wa sababu za mtoto huyo kufanya hivyo ndio ulistahili nafasi ya kwanza ili wahusika wapate dawa ya tatizo na wala si kufanya vurugu, kwa kuwa hazitibu ugonjwa ila zinaonesha uwezo mdogo wa baadhi ya watu katika kukabili matatizo. Jiulizeni, atakapoelewa maana ya kilichotokea baadaye mtoto huyo atawaelewa vipi waliohusika na tatizo lililomsibu?

No comments:

Post a Comment