Vikwazo vya maendeleo Mtwara, Lindi vitatuliwe

HIVI karibuni nilikuwa mmoja wa wananchi wazalendo waliotembelea mikoa ya Kusini; Mtwara na Lindi kuona shughuli za nishati na gesi zinazofanywa na Wizara ya Nishati na Madini.
Baada ya kufika, tulitembelea vituo vya kuzalisha umeme kwa njia ya gesi asilia inayopatikana katika mikoa hiyo na machimbo ya madini ya nikeli yanayochimbwa kwa mara ya kwanza nchini kutoka Nachingwea.
Pia tulipata taarifa za ujenzi wa kiwanda kikubwa cha saruji kinachotarajiwa kujengwa Mtwara, uzalishaji wa madini ya chumvi, kituo cha kuzalisha umeme cha Somanga, Lindi na uzalishaji gesi wa Mnazi Bay na mambo mengine.
Ziara hiyo ilitupa fursa ya kushuhudia kwa macho utajiri unaodhihirisha kuwa baada ya miaka kadhaa kutakuwa na uchumi mwingine tofauti na ilivyo sasa katika ukanda huo.
Kwa upande mwingine pamoja na utajiri huo, tulishuhudia pia hali ngumu ya maisha ya wakazi wa mikoa hiyo.
Kwa mfano baada ya Serikali kutoa kibali cha punguzo la bei ya kuunganishiwa umeme kwa mikoa ya Lindi na Mtwara, bado wamekuwa na changamoto ya kupata umeme licha ya punguzo hilo.
Katika punguzo hilo, Wizara ya Nishati na Madini iliahidi gharama za kuunganisha umeme kuwa Sh 99,000 kutoka Sh 455,000 kwa nyumba zilizo ndani ya meta 30 kutoka nguzo ilipo.
Lengo la Serikali ni jema la kunufaisha wakazi wa mikoa hiyo na gesi inayozalishwa kutoka mikoa yao. Changamoto kubwa ya utekelezaji wa ahadi hiyo ni makazi ya wananchi katika mikoa hiyo ambayo yameezekwa kwa nyasi na hivyo kuwa vigumu kuunganishiwa umeme.
Kutokana na changamoto hiyo, kuna uwezekano punguzo hilo litakalositishwa Desemba mwaka huu, kutonufaisha wengi kama ilivyokusudiwa kama watakuwa hawajaboresha majengo yao.
Kwa hiyo, wananchi wa Mtwara na Lindi, watalazimika kuungana na Watanzania wenzao nchini kunufaika na punguzo lingine la kuunganishiwa umeme linaloanza Januari mwakani, ambalo si la chini kama linalokwisha muda Desemba mwaka huu.
Ninawasihi wabunge na wanasiasa wengine wa mikoa hiyo kutafuta njia mbadala ya kusaidia wizara kufikia azma yake kwa wakazi wengi wa mikoa hiyo kunufaika na umeme wa gesi unaozalishwa katika mikoa yao kwa kuwatafutia namna ya kuezeka nyumba zao.
Ni wazi, kuwa wananchi wa mikoa hiyo wanategemea kilimo cha ufuta na korosho ambacho kwa mara nyingi ni cha msimu, hivyo ni vema nyakati za mavuno wawasaidie wananchi kuwa na mikakati ya ujenzi wa nyumba bora zilizoezekwa kwa bati.
Aidha, wananchi wa mikoa hiyo pia wanatakiwa kujiwekea mikakati madhubuti, ili kuhakikisha wanafaidika na rasilimali zilizopo na kujiinua kiuchumi kwa kuchangamkia masuala yanayotolewa kwa ajili yao.
Pia hivi karibuni Wizara ya Nishati na Madini ilibainisha kuwepo mikakati ya wizara hiyo ya kusomesha vijana wa mikoa hiyo katika vyuo vya ufundi (VETA) kuhusu masuala ya gesi na mafuta.
Ninawasihi wakazi wa mikoa hiyo kuchangamkia ofa hiyo mara itakapotangazwa na wanasiasa na viongozi wao kuhamasisha vijana kuichangamkia ili mafanikio ya rasilimali hizo yaonekane dhahiri kwa wananchi wa mikoa hiyo.
No comments:
Post a Comment