Search This Blog

Sunday, October 28, 2012

UVCCM wakemewa

• Nape awatetea adai kuchapana ni kawaida

SIKU moja baada ya vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), kuchapana hadharani kupinga viongozi wao wapya wakidai uchaguzi wao ulitawaliwa na rushwa, baadhi ya viongozi wa dini wameta hatua zaidi zichukuliwe kukomesha rushwa inayozidi kushika mizizi.

Wao viongozi wa dini walikemea rushwa huku wakitaka pia nyumba za ibada ziheshimiwe badala ya kutumiwa kama majukwaa ya kisiasa na baadhi ya watu.

Akizungumza katika Kanisa la Christian Misssion Fellwoship la jijini Dar es Salaam kwenye ibada ya Jumapili iliyokuwa maalumu kwa ajili ya kuombea amani, Askofu Mkuu wa kanisa hilo, Dk. Mgulu Kilimba, alisema kitendo cha vijana hao kutwangana makonde kinaonyesha hakuna mafanikio ya kukabiliana na tatizo la rushwa.

Alisema serikali na watawala wamekuwa wakilaani na kukemea ubaguzi wa dini, rushwa na ufisadi bila kuwepo kwa mafanikio ndiyo maana taifa linashuhudia vijana wakitwangana kutokana na kushamiri kwa matendo ya rushwa.

“Hii yote ni vita ya kiroho. Chuki na rushwa ni roho ya shetani na inapaswa kukemewa na viongozi wa dini huku watawala wakitakiwa kuchukua hatua ili kukabiliana na tatizo hilo linalozidisha chuki kwa jamii,” alisema.

Alisema kuwa kutokana na matatizo hayo, kanisa hilo limechukua hatua ya kufanya ibada maalumu ya kuombea taifa amani iliyohusisha maombi kutoka makabila 12 ambapo waliomba kwa lugha zao pamoja na kuimba wimbo wa taifa kwa ajili ya kusisitiza amani.

Huku akisoma maandiko kutoka katika kitabu kitakatifu cha Biblia 1Timotheo 2:1-2 ‘Basi, kwanza kabisa, naagiza kwamba dua, sala, maombezi na shukrani zitolewe kwa ajili ya watu wote: kwa ajili ya wafalme na wote wenye mamlaka, ili tupate kuishi maisha ya utulivu na amani, tukimcha Mungu na kuwa wenye heshima kwa kila njia.’

Kuhusu nyumba za ibada, Dk. Kilimba alionya viongozi wa kidini kuhakikisha kuwa nyumba za ibada zinatumika kwa ajili ya mahubiri ya neno la Mungu na kuepuka kutoa mahubiri ya kisiasa yanayochangia kuwepo kwa vurugu.

Alisema kuwa viongozi wa dini wanaaminiwa na jamii inayowazunguka iwapo watatoa neno lolote linaweza kujenga nyufa na kujitokeza kwa chuki.

Dk. Kilimba alisema kuwa iwapo amani itaondoka matajiri na walio na fedha watalazimika kukimbia na kuwa wakimbizi katika nchi nyingine huku maskini wakikosa mahali pa kukimbilia na kuishia kuuawa hivyo ni muhimu kuitunza na kuilinda amani kwa gharama zozote.

Alisema amani hiyo ni tunu iliyotoka kwa Mungu ambapo waasisi wa taifa hili akiwemo hayati Julius Nyerere waliiacha na inapaswa kuenziwa.

Naye, Mchungaji wa Kanisa la Mikocheni B Assembilies of God, Dk. Getrude Rwakatare, alisema kuwa ibada ya Jumapili imetumika mahsusi kwa ajili ya kuombea taifa amani.

Alisema kuwa ni muhimu Watanzania wakaishi kwa kusameheana na kuondokana na makundi ili taifa liendelee kujivunia kuwa kisiwa cha amani.

“Manung’uniko hayajengi na wala hayasaidii tuondoe kunyoosheana vidole ili tuzidi kuijenga nchi yetu na taifa liendelee kuwa kimbilio la nchi nyingine,” alisema.

Aidha mchungaji Niku Kiungu kutoka nchini Marekani, alisema kuwa Mungu ataendelea kulibariki taifa hili kwa kuwa hata wimbo wa taifa umeanza kubariki mataifa mengine kwanza.

Nape awatetea UVCCM

Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema kuwa Watanzania hawapaswi kushangazwa na kitendo cha vijana wa UVCCM kuchapana makonde juzi hadharani kwani tukio hilo si la kwanza kutokea kwao.

Akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu, Nape alisema ugomvi wa juzi katika makao makuu ya umoja huo jijini Dar es Salaam ni mambo yanayowakuta vijana wengi katika maeneo mbalimbali na kwamba kinachotakiwa ni namna ya kuutuliza.

“Mimi niko Mwanza, sijapata taarifa sahihi hivyo siwezi kukupa tathmini yangu, lakini tambua haya yalianza enzi za kina John Guninita, hata mimi na Nchimbi tulishawahi kugombana mwaka 2003 kwa sababu ya umoja huo, cha msingi ni kuangalia nini kitafanyika baada ya tendo hilo,” alisema Nape.

Alisema wakati wa kina Guninita kanuni za uchaguzi zilifuatwa na bado kulitokea hali ya kutoelewana na kusisitiza kuwa hata marehemu baba yake Moses Nnauye akiwa kiongozi wa jumuiya hiyo, walishachapana kwa bakora kwa ajili ya kuweka mambo sawa.

Aliongeza kuwa anasikitishwa na hali ya vijana wa chama hicho kukosa uvumilivu hata kufikia hatua ya kuvamiana mwilini na kupigana na kwamba chama kitakaa baada ya kupata taarifa kamili na kisha kutoa tamko lake juu ya tukio hilo.

No comments:

Post a Comment