Search This Blog

Tuesday, October 16, 2012

Watuhumiwa kumuua Mgiriki, kupora.

POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imewakamata watu watano wanaotuhumiwa kumuua raia wa Ugiriki na kupora wageni.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum, Suleiman Kova alidai watu hao wamekuwa wakiwaibia watu mbalimbali kwa kuwaburuza chini.

Aliwataja watu hao kuwa ni Peter Sunday (30) na Majid Gido (25) wakazi wa Mbagala Kizuiani, Hamisi Hassani (31) mkazi wa Magomeni Mapipa, Amini Hussin (30) mfanyabiashara wa Kawe Ukwamani na Nicholaus Dismas (30) mfanyabiashara na mkazi wa Kota.

Mgiriki huyo Petroula Chatzi Pantazi (48) aliuawa Septemba 24 mwaka huu baada wa wezi kukwapua begi na kumburuza. Alifariki akipatiwa matibabu katika hospitali ya Aga Khan baada ya kuvujia damu kwa ndani.

Akizungumzia tukio hilo la raia wa Ugiriki aliyekuwa hapa nchini kwa ziara ya mafunzo, Kova alisema watuhumiwa wakiwa na gari aina ya Toyota Gx 100 Saloon walimburuza chini Pantazi aliyekuwa na wenzake 32 waliokuwa wakitembea kwa miguu kutoka Hoteli ya Palm Beach kwenda Kanisa la Madhehebu ya Orthodox.

Kova alidai katika mahojiano na watuhumiwa hao, mtuhumiwa Hamisi alikiri kuhusika na mauaji ya raia huyo wa Kigiriki na kuendesha gari iliyohusika na uhalifu huo ambalo alidai kupelekewa gari hilo na kijana wa kiarabu mkazi wa Magomeni Mapipa.

Kova alisema Polisi pia imekamata magari mawili yenye namba T 407 BSZ Toyota Carina na T 380 AWT Toyota Rav4 zikiwa na namba bandia. Katika tukio lingine, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Temeke, David Misime alisema mtembea kwa miguu ambaye hakufahamika jina lake aligongwa na gari na kufa papo hapo juzi.

Alisema marehemu anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka kati ya 40-45 alikuwa amevaa suruali nyeusi, shati nyeupe na raba nyeupe na mwili wake umehifadhiwa kwenye Hospitali ya Temeke.

Misime alisema Polisi inashikilia gari inayodaiwa kuhusika katika ajali hiyo na dereva Said Korigwa (44) mkazi wa Mbagala Kizuiani huku upelelezi ukiendelea.

No comments:

Post a Comment