Viongozi Pwani walalamikiwa kudidimiza maendeleo.
WANANCHI wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Vijijini na Mjini, mkoani Pwani wamewalalamikia viongozi na watendaji wao kwa kushindwa kuwajibika ipasavyo, hivyo kuchangia kudidimiza maendeleo.
Walitoa malalamiko hayo jana mjini hapa walipokuwa wakichangia mdahalo wa kujadili kero mbalimbali wanazokabiliana nazo.
Walisema viongozi hao wamekuwa kikwazo kikubwa katika suala zima la kuleta maendeleo kwa wananchi kutokana na kila mara wanapowahitaji kukutana nao inakuwa vigumu, hivyo kushindwa kuwasilisha kero zao.
Mmoja wa wananchi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mtaa wa Mailimoja, Geofrido Nombo, alisema mbali ya viongozi hao kushindwa kuhudhuria katika midahalo mbalimbali inayoitishwa pia Halmashauri ya Mji wa Kibaha imekuwa ikitekeleza baadhi ya miradi bila kuwashirikisha wananchi.
Nombo alisema katika Kata ya Mailimoja hakuna hata mradi mmoja ulioibuliwa na wananchi na ukatekelezwa, miradi mingi inayotekelezwa ni ile iliyoibuliwa na viongozi, hali ambayo inawakosesha imani wananchi ambao ni walengwa wa miradi hiyo.
Naye Subira Uputure ambaye ni mlemavu wa kusikia, aliiomba serikali ione uwezekano wa kuwashirikisha katika mambo mbalimbali yanayofanyika badala ya ilivyo sasa ambapo wameshindwa kushirikishwa katika mchakato wa maoni ya katika mpya.
No comments:
Post a Comment