Search This Blog

Saturday, October 27, 2012

Magufuli aisuka upya TEMESA


WAZIRI wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, amesema kuwa amefanya mabadiliko makubwa na kuweka sura mpya katika uongozi wa Kitengo cha Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) ili kuwa na watendaji wenye umakini mkubwa.

Magufuli alifichua siri hiyo jana, baada ya kutia saini mkataba wa ujenzi wa daraja la Kilombero na barabara zake katika hafla iliyofanyika makao makuu ya Wakala wa Barabara nchini (Tanroad) jijini Dar es Salaam.

Alisema kufuatia malalamiko na hujuma mbalimbali za watendaji alizokuwa akisikia na kuzifanyia uchunguzi, hivi karibuni atatangaza majina ya watendaji wapya ambao tayari wameshachaguliwa na kwamba anaamini watamsaidia katika utendaji.

“Niwaambie tu TEMESA kuna mabadiliko makubwa sana, yaani nimefanya ‘reshuffle’ kubwa, tunataka watendaji wenye umakini na nitasaidiana nao katika kazi, maana hata kuyakamata magari ya watu waliyoweka namba zao binafsi nitashirikiana nao pia,” alitamba Magufuli.

Mbali na TEMESA, Waziri Magufuli alitamba kuwa kuna mabadiliko yatafanyika kutokana na kutangazwa upya kwa nafasi za kazi za watendaji mbalimbali katika vituo vya mizani.

Alifafanua kuwa, alishawahi kusema kuwa mizani kunanuka rushwa hivyo nafasi zimetangazwa, kwa wale watakaoonekana kuwa wasafi watabaki endapo wataomba, lakini wala rushwa wataondolewa.

“Awali nilisema 80% ya watendaji wa mizani wamejaa rushwa tupu na nikatoa maagizo baada ya siku mbili yakafanyiwa marekebisho, na mkurugenzi ametangaza nafasi mpya kwa mikoa yote na hata ukiangalia kwenye mtandao wa wizara utaona hizo nafasi,” alisema.

Akizungumzia kuhusu ujenzi wa daraja la Kilombero, alisema litajengwa na Kampuni ya China Railway 15 Bureau Group Corporation ya China ambayo ilishinda zabuni kwa gharama ya sh bilioni 62.8 ikiwa ni pamoja na kodi ya ongezeko la thamani (VAT).

Alisema muda wa ujenzi wa daraja hilo utakuwa ni miezi 24, huku akimtaka mkandarasi huyo kufanya kazi kwa mujibu wa muda uliopangwa na si vinginevyo.

No comments:

Post a Comment