Search This Blog

Tuesday, October 16, 2012

Mkurabita kutoa elimu ya ujasiriamali



 MPANGO wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (Mkurabita), umejiandaa kutoa elimu ya ujasiriamali katika maeneo yote ambayo wananchi wake wamepatiwa hati miliki za kimila.

Lengo la kutoa elimu hiyo ni kuwajengea wananchi hao uwezo wa kuzitumia hati hizo, kujiletea maendeleo na kupunguza umasikini.

Kauli hiyo imetolewa juzi na Mratibu wa Mkurabita, Seraphia Mgembe wakati akizungumza katika kipindi maalumu cha Televisheni, kilichotangazwa na TBC-1.

Katika kipindi hicho, alikuwa akijibu changamoto mbalimbali zilizotolewa na wananchi mbalimbali mara baada ya kukabidhiwa hati miliki za kimila, kazi inayofanywa na Mkurabita nchini kote.

Mgembe alisema kazi ya ugawaji hati miliki za kimila, ni hatua ya kwanza, ili Watanzania wamiliki mali yenye thamani waitumie kuwa dhamana, wakopesheke na kutumia mikopo hiyo kama mtaji wa kujiletea maendeleo na kuondoa umasikini.

Alisema baada ya kukamilika kwa ugawaji wa hati miliki za kimila, Mkurabita utayazungukia maeneo yote waliyopatiwa hati hizo na kueneza elimu ya ujasiriamali kwa kuwaunganisha na sekta za fedha, ili hati hizo zitumike kubadili maisha yao.

“Kumiliki tu kwa hati miliki hakutakuwa na maana yoyote kama hati hizo zitaishia kuwekwa makabatini, hati miliki itakuwa na maana pale tu itakapogeuzwa dhamana na kutumika kupata mitaji ya kuleta maendeleo.

Mgembe alikuwa akijibu changamoto zilizotolewa na wananchi katika vijiji vya Kindi na Sambarai, ambao mara baada ya kukabidhiwa hati miliki zao za kimila, waliiomba Mkurabita kuwasaidia jinsi ya kuzitumia hati hizo kujiletea maendeleo.

Meneja Urasimishaji wa Mkurabita, Stephen Rusibamayila, alitoa mwito kwa halmashauri zote nchini, kupima maeneo yao na vijiji ili kuunga mkono juhudi za Mkurabita badala ya kuisubiri pekee.

No comments:

Post a Comment