Search This Blog

Friday, October 12, 2012

WB yaipatia Musoma bil. 13/-



BENKI ya Dunia (WB) imetoa ufadhili wa zaidi ya sh bilioni 13 katika Manispaa ya Musoma mkoani Mara, kwa ajili ya ujenzi wa barabara za lami na masoko ya kisasa.

Fedha hizo zitatolewa kwa awamu tofauti na kwamba katika awamu ya kwanza manispaa hiyo imepewa dola milioni 2.5 (sawa na sh bilioni 4).

Meya wa Manispaa ya Musoma, Alex Kisurura, aliliambia Tanzania Daima jana kuwa ufadhili huo umetokana na maombi yao kwa benki hiyo.

Alizitaja barabara zitakazojengwa kwa kiwango cha lami katika Jimbo la Musoma Mjini kwa ufadhili huo kuwa ni Nyasho hadi Kamunyonge, Kennedy na Kawawa hadi Mwigobero.

"Kawaida Benki ya Dunia wao wanatoa fedha kwa ajili ya miradi ya barabara. Lakini sisi Musoma tukawaomba fedha hizo tuzitumie pia kujenga masoko ya kisasa. Tunataka ndani ya miaka mitano Musoma iwe mfano wa kuigwa kwa maendeleo. Kama wengine walishindwa, sisi hatutashindwa,” alisema Meya Kisurura.

Alilitaja soko la Nyasho kuwa litakuwa la ghorofa, wakati soko la Nyakato litakuwa la kawaida, lakini la kisasa zaidi, hivyo kusaidia wajasiriamali wengi kufanya biashara zao.

Awali, Mbunge wa Musoma Mjini, Vincent Nyerere (CHADEMA), akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika hivi karibuni, alisema ndani ya muda mfupi alioingia madarakani na kwa kushirikiana na uongozi wa Manispaa ya Musoma wameweza kujenga barabara nyingi kwa kiwango cha molamu.

Alizitaja baadhi ya barabara hizo kuwa ni ile Nyakato, Mwisenge, Mukendo, Bweri, Nyasho, Makoko Zanzibar, Buhare, Bweri, Nyamatare, Kamunyonge, Majengo mapya, Mtakuja pamoja na barabara ya Kigera.

Pia alieleza amefanikiwa kutekeleza ahadi yake ya kugawa televisheni 10 mpya na za kisasa zitakazofungwa katika soko kuu la Musoma, ili kurahisisha upatikanaji wa habari kwa wananchi na wafanyabiashara wa soko hilo.

No comments:

Post a Comment