Search This Blog

Tuesday, October 16, 2012

Vigogo Bodi ya Korosho kortini.






TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Mtwara, imewaburuta kortini vigogo wanne wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) wakidaiwa kutumia vibaya madaraka yao kwa kutoa zabuni kinyume cha sheria.

Vigogo hao ambao ni wajumbe wa Bodi ya Zabuni ya CBT, walifikishwa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mtwara, Joseph Fovo kujibu tuhuma zinazowakabili.

Mwendesha Mashitaka wa Takukuru, Eveline Onditi aliwataja washitakiwa ni Ayoub Mbawa (59) ambaye ni Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa CBT, pia Mwenyekiti wa Bodi ya Zabuni; Mariam Chimbyangu (37) Ofisa Manunuzi ambaye pia ni Katibu wa Bodi ya Zabuni ya CBT, Mhandisi Shabani Misuli (52) Meneja wa Mafunzo na Ubanguaji na Mohamedi Hanga ambaye ni Mkurugenzi wa Masoko na Huduma za Mawasiliano.

Onditi alidai kuwa kati ya kipindi cha Novemba 2008 na Mei 2009, watuhumiwa hao wakiwa wajumbe wa Bodi ya Zabuni kwa pamoja wanadaiwa kutumia vibaya madaraka kinyume cha Kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya mwaka 2007 kwa kushindwa kutangaza zabuni.

Onditi alisema pia watuhumiwa wote wanadaiwa kutoa zabuni bila ya kuwapo kwa taarifa ya Kamati ya Tathimini, jambo ambalo ni uvunjaji wa sheria katika utendaji wao wa kazi.

Hata hivyo haikuelezwa mahakamani hapo zabuni hiyo ilihusu nini na iligharimu kiasi gani. Watuhumiwa Mbawa, Misuli na Hanga ndiyo waliopandishwa kizimbani, huku Chimbyangu hakutokea mahakamani hapo, hali iliyoilazimu mahakama kutoa hati ya kukamatwa ili afikishwe kujibu tuhuma zake.

Watuhumiwa wote wapo nje kwa dhamana baada ya kukana mashtaka yanayowakabili hadi Novemba 6, mwaka huu, kesi hiyo itakapotajwa tena


No comments:

Post a Comment