Mapungufu ya kimahesabu, POAC yashindwa kujadili Shirika la Magazeti.
Mh. Zitto Zuberi Kabwe
Kamati ya kudumu ya bunge ya mashirika ya umma POAC imeshindwa kuendelea na kikao chake kulijadili shirika la magazeti ya serikali la Tanzania Standards News Paper TSN kutokana na kubaini mapungufu mengi hasa ya kimahesabu.
Kikao hicho kimevunjwa wakati wa vikao vya kamati za Bunge vinavyoendelea jijini Dar Es Salaam.
Miongoni mwa mapungufu hayo ni pamoja na kubainika bodi ya shirika hilo kufuta madeni ya zaidi ya shilingi bilioni nne bila kufuata utaratibu wa kimahesabu na makosa ya kihasibu ya zaidi ya shilingi bilioni 19.
Mwenyekiti wa POAC Mheshimiwa Zitto Kabwe alitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari mara baada ya kuvunjwa kwa kikao hicho na kueleza mikakati itakayofuata ikiwa ni pamoja na kuziita baadhi ya idara za serikali Dodoma wakati wa vikao vya bunge kwa ajili ya kujadili namna ya kutatua matatizo yaliyobainika.
Wakati huo huo Jeshi la zimamoto na uokoaji limetakiwa kuwasilisha changamoto zinazowakabili kwa kamati ya kudumu ya fedha za serikali kwa ajili ya kutafutiwa ufumbuzi.
Agizo hilo linatokana na malalamiko yaliyotolewa na jeshi hilo kupitia kwa Kaimu Kamishan jenerali wake Pius Nyambacha wakati lilipoitwa kuhojiwa na kamati hiyo.
Kamati za kudumu za bunge katika vikao vyake zinapata nafasi ya kupitia pamoja na mambo mengine, hesabu za mashirika ya umma, hesabu za serikali za mitaa pamoja na hesabu za serikali kuu
No comments:
Post a Comment