Watoto 27 wafanyiwa ukatili Geita
WATOTO wa kike 27 wenye umri chini ya miaka 18, wanadaiwa kufanyiwa ukatili wa aina tofauti mkoani Geita ikiwemo kubakwa na kuozeshwa kwa nguvu na wazazi ama walezi wao.Kwa mujibu wa taarifa ya polisi mkoani hapa kupitia dawati la jinsia na watoto kwa kushirikiana na polisi jamii, matukio hayo yanadaiwa kutokea katika kipindi cha Julai hadi Septemba mwaka huu.
Akisoma taarifa hiyo kwenye maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike Duniani yaliyofanyika juzi katika viwanja vya Mamlaka ya Mji wa Geita, Mwenyekiti wa dawati hilo mkoani hapa, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Halima Shabani, alisema watoto wa kike ndio wanaoathirika zaidi kuliko wa kiume.
Alisema matukio matatu ya ndoa za utotoni chini ya umri wa miaka 18 yameripotiwa na mengine 12 ya kubakwa.
Aidha, alisema watoto wanane walipigwa na kuumizwa vibaya, watatu kuolewa kwa nguvu kutokana na shinikizo la wazazi na walezi na wanne walifukuzwa nyumbani kwao baada ya kugundulika kuwa na ujauzito.
Mrakibu huyo alisema vyanzo vya ukatili huo ni ulevi wa kupindukia, umasikini, mila na desturi, ukosefu wa elimu kwa jamii, wanandoa kutengana pamoja na ukosefu wa sera madhubuti za serikali za kumlinda mtoto katika kupata haki zake za msingi.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Ally Kidwanka, aliyewakilishwa na ofisa utumishi, Jackson Sombe, alisikitishwa na sherehe hizo kuhudhuriwa na watoto pekee bila wazazi wao na hivyo kudhihirisha hawatambui umuhimu wa siku hiyo.
No comments:
Post a Comment