Wawekezaji wa nje wadai hawapati faida.
Wawekezaji binafsi katika sekta ya afya nchini, wamesema kwamba wamekuwa wakiendesha biashara hiyo kwa hasara, hali inayowasababisha wawekezaji wa nje kukwepa uwekezaji wa aina hiyo kutokana na kutopata faida.Mmoja wa wawekezaji hao ambaye ni Mkuu wa Chuo cha Sayansi ya Afya (KAM College) cha Kimara Jijini Dar es Salaam, Dkt. Kandore Musika, alisema wamekuwa wakiendesha huduma hizo kwa hasara huku serikali ikishindwa kabisa kuwaunga mkono.
“Serikali inachoangalia kwetu ni makosa tu, lakini inashindwa hata kutusaidia katika kuhakikisha jitihada tunazofanya katika kuhakikisha tunaongeza wataalamu wa afya nchini kuwa ni endelevu,” alisema Dkt. Musika.
Kwa mujibu wa Dkt. Musika, Tanzania ni moja ya nchi zinazoendelea ambazo zina uhaba mkubwa wa madatari.
Alisema uwiano uliopo wa daktari mmoja kuhudumia wagonjwa 25 kama ilivyoelekezwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) ni tofauti kwani kwa Tanzania daktari mmoja anahudumia wagonjwa zaidi ya 200.
Dkt. Musika alisema jitihada zinazofanywa na wazawa katika kuhakikisha idadi ya wataalamu wa afya inaongezeka ni lazima ziungwe mkono na serikali na wadau wote wa sekta hiyo.
Chuo cha KAM chenye uwezo wa kuchukuwa wanafunzi 300 kwa sasa, kinatarajia kufanya upanuzi ili kuchukuwa wanafunzi 1000.
Kwa sasa chuo hicho kinatoa cheti na diploma ya taalunma ya utabibu na maabara.
Dkt. Musika aliyaeleza hayo wakati wa maadhimisho ya siku ya wadau wa sekta ya afya ya chuo hicho ambapo malengo ya kutenga siku hiyo ni kujadili changamoto zinazoikabili sekta hiyo ikiwa ni pamoja na kupata ufumbuzi wake
No comments:
Post a Comment