Search This Blog

Friday, October 12, 2012

Mnyika aishtaki Manispaa Kinondoni



MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), ameiandikia barua Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, akiilalamikia Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kwa kushindwa kuwapatia maji wakazi wa Kata ya Goba.

Katika barua hiyo ya Oktoba 10 mwaka huu, Mnyika anayewawakilisha wakazi wa Kata ya Goba anaomba tume hiyo ichunguze na kuchukua hatua dhidi ya waliohusika katika ukiukwaji wa haki za binadamu zilizosababisha wananchi kukosa huduma ya msingi ya maji.

Pia anaiomba tume iwachukulie hatua waliohusika na uvunjaji huo wa haki za msingi na ipendekeze hatua za haraka zinazopaswa kuchukuliwa na wahusika katika kuwanusuru wakazi wa Goba na adha ya ukosefu wa maji.

Katika maombi yake hayo, Mnyika aliiomba tume ipendekeze hatua za ziada zitakazotumiwa na Manispaa ya Kinondoni kwa ajili ya kuiondosha Goba katika kupatiwa huduma ya maji na manispaa hiyo.

Aidha, Mnyika aliomba tume hiyo ichunguze na kupendekeza masuala mengine ya kushughulikiwa na mamlaka zingine zinazohusika, ikiwemo Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA), Wizara ya Maji na Vyombo vya Ulinzi na Usalama kuhusu masuala ya ukiukwaji wa haki za binadamu na uvunjwaji wa misingi ya utawala bora katika miradi ya maji kwenye kata hiyo pamoja na mfumo wa upatikanaji wa maji kwa ujumla.

Alisema tatizo la maji katika Kata ya Goba lina zaidi ya miaka mitano na serikali inatambua hilo, huku Manispaa ya Kinondoni ikiwa haionyeshi jitihada za kushughulikia.

Aliitaka tume iilazimshe Wizara ya Maji, Mamlaka ya Majisafi na Majitaka (DAWASA) na Kampuni ya Majisafi na Majitaka (DAWASCO) kuzingatia kwamba maeneo ya pembezoni ya Dar es Salaam ambayo awali yalikuwa vijiji, sasa ni mitaa yenye wakazi wengi na kwamba yanapaswa kuunganishwa na mtandao wa maji chini ya mamlaka husika

No comments:

Post a Comment