Search This Blog

Friday, October 12, 2012

Magereza wahujumu wafungwa



JESHI la Magereza Mkoa wa Mwanza, limeingia katika tuhuma za kuwatumikisha wafungwa waliopo gerezani kwa manufaa binafsi ya viongozi wakuu wa jeshi hilo mkoani humo.

Wakizungumza na Tanzania Daima Jumamosi, baadhi ya wafungwa katika Gereza Kuu la Butimba mkoani humo, waliwataja vigogo wawili wa magereza hayo (majina tunayo) kuwa vinara wa mpango huo.

Walisema vigogo hao wanawatumia wafungwa kulima bustani iliyofichwa kwa jina la ‘mradi wa gereza’ na kuuza kuni mitaani.

Imedaiwa kuwa, kuni zinazokusanywa huuzwa kwa wachoma matofali mkoani Mwanza na mamalishe, huku mboga zikiuzwa katika masoko ya jiji hilo na kwamba mahindi yanayofikishwa jijini Mwanza kutoka mkoani Shinyanga kwa ajili ya chakula cha wafungwa, yanakwapuliwa na baadhi ya viongozi wa magereza wa mkoa huo.

Ufisadi mwingine unaodaiwa kufanywa na mmoja wa vigogo hao, ni pamoja na kushindwa kutoa huduma zinazotakiwa kwa wafungwa wenye mahitaji maalumu, yaliyothibitishwa na daktari.

“Kuna wagonjwa wa ukimwi na wengine wanaotakiwa wapate lishe maalumu kwa ajili ya kuboresha afya zao, lakini hawahudumiwa licha ya serikali kutenga fungu la fedha,” kiliongeza chanzo chetu.

Aidha chanzo hicho kilidai kuwa, wafungwa wa gereza la Butimba wananyimwa haki ya kupewa barua za kukata rufaa hadi watoe fedha kwa askari wa gereza hilo, hali waliyoeleza kuwa inachangia kwa kiasi kikubwa mlundikano wa wafungwa gerezani.

Mkuu wa Magereza jijini Mwanza (RPO), Raphael Molel, alipohojiwa na Tanzania Daima Jumamosi, alikanusha tuhuma hizo, lakini akadai kuwa askari waliofukuzwa kazi ndio kiini cha maneno hayo.

Molel alisema ni kweli wanapata mahindi kutoka mkoani Shinyanga na kwamba yanatumika kwa matumizi ya wafungwa, huku akibainisha suala la kuni kuwa ni tatizo katika Jiji la Mwanza hali inayowafanya waombe kuni za watu katika maeneo yanayoonekana.

Alisema kama wapo askari wanaofanya hivyo, hilo litakuwa ni tatizo la askari mmoja mmoja na halihusishi uongozi wa jeshi, huku akikanusha kuwepo kwa fungu la kuwahudumia wafungwa wenye mahitaji maalumu kutoka serikalini.

“Kama uko hapa Mwanza njoo ofisini kwangu, lakini ukumbuke maneno hayo ni ya askari waliofukuzwa kazi,” alisema Mollel.

No comments:

Post a Comment