Mramba: BoT iliidhinisha Alex Stewart kuongezwa mkataba kukagua dhahabu.
Aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba
Aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba, ameiambia mahakama kuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ndiyo iliyoidhinisha Kampuni ya M/S Alex Stewart Government Business Assayers kuongezwa mkataba wa kukagua migodi ya dhahabu nchini kwa sababu ya kazi nzuri iliyofanywa na kampuni hiyo katika mkataba wake wa kwanza.
Mramba alidai kuwa mkataba huo ulisainiwa na aliyekuwa Gavana wa BoT, Daudi Balali, kwa niaba ya Benki hiyo na Mtendaji Mkuu wa Alex Stewart Government Business Assayers, Dk. Segule, kwa niaba ya kampuni hiyo.
Alitoa madai hayo wakati akijitetea akiongozwa na Wakili wa Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, Daniel Yona, Elisa Msuya, katika kesi ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara ya Sh. bilioni 11.7 inayomkabili na wenzake wawili.
Mramba alitoa madai hayo mbele ya jopo linaloongozwa na Jaji John Utamwa akisaidiwa na Jaji Sam Rumanyika, Msajili Sauli Kinemela.
Mramba, Yona na Katibu Mkuu mstaafu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Gray Mgonja, walifikishwa mahakamani mwaka 2008.
Inadaiwa kuwa kati ya Agosti, 2002 na Juni 14, 2004, jijini Dar es Salaam, washtakiwa wakiwa watumishi wa umma, walitumia vibaya madaraka yao na kuisababishia serikali hasara ya kiasi hicho cha fedha.
Ilidaiwa kuwa washtakiwa hao waliipatia msamaha wa kodi isivyo halali, kampuni hiyo ya nchini Uingereza.
No comments:
Post a Comment