TIC yawapa changamoto wawekezaji.
KITUO cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimetoa changamoto kwa wawekezaji wa hapa nchini kuimarisha ushirikiano na wenzao wa China kwa faida ya nchi zote mbili.
Wito huo ulitolewa na Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa TIC, Beatrice Chonjo jijini Dar es Salaam katikati ya wiki hii wakati wa mkutano kati ya wafanyabiashara kutoka Jimbo la Tianjin la nchini China na wenzao wa hapa nchini.
“Tunahamasisha wafanyabiashara wa humu nchini kujenga mahusiano ya kibiashara na hawa wenzao kutoka katika jimbo hili, tutakuwa tayari kusaidia pale patakapohitajika,” alisema.
Ujumbe huo ulihusisha watu 32 ambao waliwakilisha kampuni 17 katika sekta mbalimbali.
Alifafanua zaidi na kusema mbali na kufaidika kibiashara, wafanyabiashara hapa nchini wanaweza kufaidika kwa kujifunza masuala ya teknolojia na mbinu bora za biashara na za kisasa kutoka China ambayo imepiga hatua kubwa kimaendeleo.
Naibu Katibu Mkuu wa Baraza la Biashara la Tanzania na China, Pan Lei, alisema ushirikiano kati ya nchi hizo ni wa muda mrefu na kwamba hauna budi kulindwa.
Alisema mahusiano bora ya kibiashara kati ya nchi hizo ni njia nzuri ya kuimarisha mahusiano kati ya wafanyabiashara wa Tanzania na wale wa kutoka Tianjin, China.
Afisa mwandamizi wa Ubalozi wa Jamhuri ya Watu wa China hapa nchini, Jijun Fu, alisema kwamba uhusiano kati ya Tanzania na China ni wa muda mrefu.
Alisema nchi hizo zote zina lengo moja la kuendeleza uchumi wao kwa maslahi ya mataifa hayo na kusema katika miaka mitano iliyopita, China imeipatia Tanzania mkopo wa dola bilioni 1.5 za Marekani kwa ajili ya miradi mbalimbali kama ule wa kujenga Uwanja wa Ndege Zanzibar na bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment